Ripoti ya CAG Yawaweka Kikaangoni Vigogo wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD)

Ripoti iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Musa Juma Assad imezichanganya Hospitali ya Taifa Muhimbili na Bohari ya Dawa (MSD), huku Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akihitaji maelezo ya kina kuhusu mkanganyiko huo.

Ummy ameitaka MSD kuandika maelezo ya kina kwa maandishi, kuhusu vifaa vya Sh2 bilioni ambavyo viko njiani kwenda Muhimbili kwa miaka minne sasa, kabla wizara yake haijatoa tamko rasmi.

Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu  jana alisema bohari haina mzigo wowote ulio njiani kuelekea Muhimbili bali imekuwa ikisambaza dawa zake nchi nzima.

Bwanakunu alisema tatizo lililojitokeza ni mfumo wa kompyuta ambao unaonyesha mzigo upo njiani, hivyo muamala katika kompyuta unavyoshindwa kukamilika, mzigo lazima uonekane upo njiani.

“Mwaka 2012 tulibadilisha mfumo wa kompyuta kutoka wa awali mpaka tunaotumia sasa, hivyo kuna miamala ilihitaji kubadilishwa, mwaka huu tulifanya zoezi la kukamilisha baadhi na si kwa Muhimbili pekee kwa mfano kuna mzigo unatoka MSD Ubungo kwenda Muleba ukifika kule mtu anashindwa kuingiza kwenye mfumo kwamba umepokelewa,” alisema Bwanakunu.

Alifafanua kwamba majibu ya MSD kwa CAG yalieleza kuwa walitengeneza timu ya uchunguzi na baadhi ya watu walichukuliwa hatua, “nimeshachukua hatua za haraka baada ya kupata hiyo ripoti, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wale ambao hawakujaza hiyo miamala tulishawachukulia hatua, hakuna mali iliyopotea MSD.”

Taarifa zaidi zinaeleza kwamba kuna ripoti ya Muhimbili ambayo inaonyesha katika vitabu kwamba kuna mzigo ambao Muhimbili iliununua kutoka MSD, lakini haujafika, lakini Bwanakunu alipoulizwa alisema hakuna vitabu vinavyoonyesha kuwa Muhimbili inadai vifaa tiba na dawa MSD.

Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema kwa taarifa alizonazo mpaka sasa CAG alifanya ukaguzi katika vitabu vya MSD na si wao na alipouliza vifaa viko wapi alijibiwa kuwa vinakwenda MNH.

Alisema kuwa Watanzania wawe na subira na kwamba watapewa majibu kesho (leo), baada ya Muhimbili kupekua kwa kina vitabu vya mwaka 2012, ili kujiridhisha iwapo vifaa vilipokelewa au havikuwahi kununuliwa Muhimbili.

“Hiyo ripoti tumeiona leo Jumanne. Hayo mambo yametokea mwaka 2012 huwezi kuwa na jibu la kila kitu, kesho tunataka tukapitie hiyo ripoti kwa sababu ni ukaguzi wa MSD, tukaangalie vitabu hivyo vifaa vilifika?” Alisema Museru.

Naye Waziri Ummy Mwalimu alisema katika ripoti hiyo kuna hoja mbili ambazo ni MSD na TFDA, huku akifafanua kwamba amezungumza na Mkurugenzi wa MSD lakini hajaridhika na majibu na kumtaka aandike maelezo ya kina.

“Nimetaka maelezo ya maandishi kutoka kwa MSD na TFDA kuhusu ripoti ya CAG tumekubaliana na Katibu Mkuu walete maandishi ndiyo tutatoa msimamo rasmi wa wizara, kwa upande wa MSD ndiyo maana tuliweka pembeni wale wakurugenzi wanne sababu ya changamoto hii ambayo CAG amekutana nayo,” alisema Ummy.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad