Gazeti hilo lilieleza kuwa leseni hiyo ilitolewa na Ofisa Madini Kanda ya Ziwa, Mhandisi Juma Sementa, yenye uhai wa miaka Saba na kwamba upatikanaji wa leseni hiyo haujawaridhisha wadau kadhaa wa ardhi na mazingira kwani mbali na sheria ya kuzuia uchimbaji madini ndani ya maeneo ya hifadhi nchini, wadau wengine hawakuhusishwa katika upatikanaji wake.
Wizara inapenda kutoa taarifa kuwa, wilayani Meatu kuna hifadhi ya Maswa (Maswa Game Reserve) na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika eneo la Makao (JUHIWAPOMA) ambapo Jumuiya hiyo ilipitisha Mpango wa Kanda za Matumizi ya Rasilimali kwa mwaka 2015-2017 na kutenga eneo la Gururum lenye ukubwa wa kilomita 16.5 sawa na asilimia 2 ya eneo lote, kama kanda ya uchimbaji madini baada ya madini ya shaba kugundulika katika eneo hilo.
Katika eneo hilo la Gururum mpaka sasa jumla ya viwanja 82 vya uchimbaji mdogo wa madini (PML) vimetolewa ambapo kwa sasa hakuna shughuli zozote za uchimbaji zinazoendelea hadi tathmini ya uharibifu wa mazingira (EIA) itakapokamilika ambayo ipo katika hatua ya uwasilishwaji.
Hivyo tunautaarifu Umma kuwa mpaka sasa hakuna mgodi katika hifadhi ya Mwiba na kwamba leseni za uchimbaji mdogo wa madini zimetolewa katika eneo lililorusiwa tu kwa ridhaa ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika eneo la Makao (JUHIWAPOMA).
Tunawaasa waandishi wa habari kuhakiki taarifa wanazotoa katika vyombo vya habari kwa kuwasiliana na wahusika wanaotajwa katika habari husika ili kuepuka kutoa taarifa potofu kwa Umma.
IMETOLEWA NA WIZARA YA NISHATI NA MADINI
18 APRILI, 2016