Akizungumza katika mahojiano maalumu hivi karibuni, Tendwa ambaye kitaaluma ni mwanasheria alisema: “Mambo anayoyafanya Rais Magufuli tangu aingie madarakani yanakubalika na wananchi anaowaongoza pamoja na nje ya mipaka ya Tanzania.”
Alisema ushahidi wa kukubalika kwa Magufuli nje ya Tanzania ni kuwapo kwa mijadala isiyokoma katika mitandano ya kijamii, ikionyesha kumuunga mkono na kukubaliana na mtindo wake wa kufanya kazi.
“Ndiyo maana unasikia huko nchi jirani wakizungumza kuwa nao wakimpata Magufuli wao watafurahi...hii ni hatua nzuri, maana anakubalika na anaungwa mkono na idadi kubwa ya watu kutoka sehemu mbalimbali,” alisema.
Alisema uchapaji kazi wake ndiyo uliosababisha Serikali ya Uganda kuingia makubaliano ya ujenzi wa bomba la mafuta, yanayochimbwa Uganda na kuletwa Tanzania kwa ajili ya kusafirishwa nje.
“Hata kuhusu makubaliano ya ujenzi wa bomba la mafuta kati ya Uganda na Tanzania, kama mnakumbuka awali Uganda walitutenga wakaona Kenya ndiyo wanastahili, lakini sasa wamerudi, hii ina maana wanaona kuna matumaini makubwa kutokana na utawala wa awamu ya tano kufanya kazi inayotakiwa hasa,” alisema.
Alisema hata wapinzani wanakubaliana na kasi ya utendaji wake wa kazi, kiasi cha kukiri kuwa Rais Magufuli anatekeleza yale matakwa ya wananchi ambayo ndiyo misimamo yao.
“Jamani wakati wa kufanya kazi kwa mazoea umekwisha, na hivyo ndivyo ambavyo sisi wengine tulilelewa na kufundishwa tangu zamani. Hapa katikati ilikuwa unaweza kumtuma mtu kitu, lakini kisifanyike kwa wakati, bila kupewa sababu zinazoeleweka…hizi ni zama zingine kabisa,” alisema.
Aliyataja baadhi ya mambo mazuri yanayofanywa na Rais Magufulu kuwa ni kukemea ufisadi na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma huku akisema yalikuwa yakisimamiwa na Baba wa Taifa (Mwalimu Nyerere) wakati wa utawala wake.
“Moja ya hotuba za mwalimu alisema, wajibu wa Serikali ni kukusanya kodi, na ndicho anachokifanya Rais, na huu ndiyo mwelekeo wa kisiasa na kiuchumi tunaouzungumzia sasa,” alisema na kuongeza kuwa kwa sasa watu wanalipa kodi jambo litakalosaidia kuinua uchumi na kuliletea taifa maendeleo.
Alisema hali hii ikiendelea hivyo, taifa litatulia na wananchi watafanya kazi na kuachana na ile hali ya kuandamana na kudai madai mbalimbali, kwa kuwa tayari Serikali iliyopo inaonekana kuwapatia kile wanachokitaka.
“Wananchi wanachotaka ni maendeleo yao, na hilo linaonekana wazi, dosari zilizopo ndizo zilizosababisha watu waandamane na wawe na malalamiko yasiyokoma, haya yanaelekea kupatiwa ufumbuzi,” alisema Tendwa.
Rais na demokrasia
Mbali na sifa ya kuchapa kazi na kujenga uchumi wa nchi, Tendwa alimtaja Rais Magufuli kama kiongozi anayeheshimu utawala wa sheria na kusimamia demokrasia.
Alisema kitendo cha kukemea ucheleweshaji wa upatikanaji wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ni ishara kuwa ni muumini mzuri wa haki na demokrasia.
Hivi karibuni, Rais Magufuli aliagiza kufanyika uchaguzi wa Meya wa Dar es Salaam baada ya kuwapo kwa ‘figisufigisu’ za kumpata.
Kufanyika uchaguzi huo kuliwezesha kumuweka madarakani Diwani wa Kata ya Vijibweni, Kigamboni, Wilaya ya Temeke, Charles Isaya wa Chadema. Isaya alichaguliwa kushika wadhifa huo baada ya kupata kura 84 huku aliyekuwa mgombea wa CCM, Yenga Omari, akipata kura 67.
Tendwa alisema: “Kitendo cha kukemea ucheleweshaji wa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam na kuwaeleza wazi CCM kukubali kushindwa, ile ni demokrasia, na mmeona, Jiji lina Serikali sasa, na Serikali yenyewe ni ya chama cha upinzani.”
Alivitaka vyama vya siasa visidorore na badala yake viendelee kufanya kazi yao ya kuisimamia Serikali, ambao ndiyo wajibu wao kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia staili ya Rais Magufuli ya kutumbua majipu, alisema ni vizuri watendaji wa Serikali wanapoyatumbua hayo majipu, wazingatie sheria na taratibu na vile vile wasiwaonee watu.
“Lakini taratibu za sheria pia zifuatwe yaani wanaotumbuliwa wapate nafasi ya kusikilizwa, watu wapewe muda unaotosha ili wajieleze, siyo kumwambia mtu nataka mpaka leo saa saba uwe umeniletea majibu… hii siyo sahihi, inapaswa mtuhumiwa apewe muda na nafasi ya kutosha ili ajieleze kwa sababu ni haki yake ya msingi kusikilizwa, hii ndiyo sehemu ya uchunguzi,” alisema.
Bomoa bomoa
Akizungumzia uamuzi wa Serikali wa kubomoa nyumba za wananchi zilizojengwa katika maeneo hatarishi na zile za waliovamia maeneo ya wazi, alisema kazi hiyo ilikuwa na umuhimu wake kwa usalama wao wenyewe.
Alisema bomoabomoa ilikuwapo tangu enzi za Makamba (Yusuph) akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam na Serikali iliwataka waliojenga mabondeni wabomoe, lakini wakakaidi huku wakijua ni hatari kwa usalama wao na watoto wao.
“Serikali iko sahihi, yale ni maeneo hatarishi, huwezi kuruhusu mtu akaishi katika maeneo hatarishi hata kidogo, kwahiyo Serikali imechukua majukumu yake ambayo ilipaswa kuyatekeleza miaka mingi iliyopita”
Alisema kutokana na umuhimu wa suala lenyewe, ndiyo maana mashirika yanayotetea haki za binadamu hayakusema lolote kuhusiana na suala hilo.