Wagombea Urais 11 CCM Wapewa Kazi Serikalini

Rais John Magufuli amemteua Mathias Chikawe kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan.

Huu ni mwendelezo wa kuwakumbuka kwa kuwapangia majukumu ya kitaifa baadhi ya makada wa CCM waliopambana naye katika mbio za kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Kabla ya kupangiwa kituo hicho cha kazi, Chikawe aliteuliwa kuwa balozi Februari 15, mwaka huu sambamba na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi wa Taifa (NSSF), Dk Ramadhani Dau na Dk Asha-Rose Migiro.

Chikawe, ambaye ameanza kutekeleza majukumu yale tangu Aprili 13, alikuwa miongoni mwa makada 38 wa CCM waliochukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM.

Makada waliokumbukwa

Makada wengine waliokumbukwa katika Serikali ya Magufuli ni Profesa Sospeter Muhongo, Dk Harrison Mwakyembe, January Makamba, Mwigulu Nchemba, Dk Khamis Kigwangalla, Balozi Augustino Mahiga na Dk Asha-Rose Migiro.

Ukimuondoa Dk Migiro anayesubiri kupangiwa kituo cha kazi baada ya awali kuteuliwa kuwa balozi, waliobaki kwa sasa wanamsaidia Rais baada ya kuwateua kuwa mawaziri.

Baada ya kuapishwa, Rais Magufuli, alimteua Dk Mahiga kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kitaifa.

Dk Mwakyembe, aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Akamteua Makamba kuwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Wengine ni Luhaga Mpina aliyemteua kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Khamis Kigwangwalla (Naibu Waziri Afya, Maendeleo, Jinsia, Wazee na Watoto), Mwigulu Nchemba (Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi). Rais Magufuli alimteua pia Profesa Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini.

Makada visiwani

Kwa upande wa visiwani Zanzibar, makada waliopambana na Magufuli kupitia CCM na wameteuliwa na Rais Ali Mohamed Shein kushika nafasi za uongozi kwenye Serikali yake ni Balozi Amina Salum Ali na Balozi Ali Karume, ambao wote waligombea nafasi za urais wa Tanzania.

Akitoa maoni yake kuhusu uteuzi wa Magufuli, mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Kessy alisema: “Kugombea nafasi kama hiyo siyo kuwa maadui, mbona hata Rais mstaafu Kikwete (Jakaya) aliwahi kufanya hivyo,”alisema.

Mwingine aliyeunga mkono hatua ya Rais ni mwanasheria maarufu nchini, Profesa Abdallah Safari aliyesema Rais ana haki ya kumteua mtu yeyote anayemuona anaweza kumsaidia katika uongozi.  

Chanzo:Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad