Mhe. Mongella ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye kikao cha kujitambulisha kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ambapo taarifa za awali zilionesha kutokea kwa wizi wa komputa moja iliyofungwa kwenye chumba cha mifumo ya komputa ambayo ndio hutumika kuandaa malipo mbali mbali ya halmashauri.
“OCD kesho nitakwenda kanisani asubuhi, ikifika saa 8.00 mchana nataka taarifa niikute mezani kwangu, vinginevyo hatutaelewana", amesema Mongella na kuongeza sisi tunajua nini chakufanya kama kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa lakini na wewe tumia mbinu zako kuweza kubaini wapi ilipo kompyuta hiyo.
Akizungumza kando ya Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri, Kaimu Mhazini wa Halmashauri hiyo, Baraka Munuo alidai kupokea taarifa za kupotea kwa Komputa hiyo kutoka kwa afisa TEHAMA wa halmashauri ya Ukerewe.
Katika hatua nyingine mkuu wa mkoa wa Mwanza, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kupitia mafaili na kubaini watumishi waliofanya kazi katika kituo hicho kwa muda mrefu, jambo ambalo Mkuu wa Mkoa amedai linachangia watumishi kufanyakazi kwa mazoea.
”Mkurugenzi nakuagiza pitia mafaili ya watumishi ili kubaini wote waliokaa katika kituo hiki kwa muda mrefu. Haiwezekani mtu amekaa hapa miaka ishirini na moja halafu uniambie kwamba atakuwa na maarifa mapya, hapana" alisema Mongella na kuongeza, Sasa nakuagiza pitia mafaili yao na kama kuna mtumishi aliye kaa kwa zaidi ya miaka kumi atafutiwe kituo kingine.
Wakati huo huo, MSAKO ulioanzishwa na Rais John Magufuli wa kutokomeza tatizo la wafanyakazi hewa katika utumishi wa umma, umeendelea kuibua mazito, ambapo mkoani Kilimanjaro, Benki ya CRDB imejikuta ikitoa mkopo kwa waliokuwa wafanyakazi hewa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Helga Mchomvu aliyasema hayo akidai kuwa, yamegundulika baada ya Serikali kuunda kamati za uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh milioni 500 katika halmashauri hiyo.
Kabla ya kuibuka kwa kisa hicho kinachoonesha namna wafanyakazi hewa alivyokuwa wakiibia nchi, hivi karibuni mkoani Singida, Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Imani Nyamangaro, alipandishwa kizimbani akidaiwa kujilipa mishahara ya wastaafu 57, yenye thamani ya Sh milioni 29.4.
Mbali na mhasibu huyo, Rais Magufuli alipokuwa mapumziko kijijini kwake Mlimani, katika Wilaya ya Chato mkoani Geita, alieleza kisa kingine kilichoshitua jamii kuwa katika Mamlaka ya Mapato (TRA), kulikuwa na mtumishi mmoja ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya watu 17.
Akizungumza jana, Mchomvu alidai kuwa watumishi watatu wa halmashauri hiyo; wawili wa Idara ya Utumishi na mmoja Mchumi, walikopa katika Benki ya CRDB Sh milioni 35.2, kwa kutumia majina ya wafanyakazi hewa.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mkuu Idara ya Utumishi na Utawala, Gudila Mashele, Ofisa Utumishi Daraja la Kwanza, Faraja Ndatu na Mchumi Daraja la Pili, Isaiah Bayege. Kutokana na tuhuma hiyo iliyoibuliwa na kamati hizo za uchunguzi, Mchomvu alisema Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Hai, limewafukuza kazi watumishi hao.
CHANZO: Habarileo