Waziri wa Ardhi,Nyumba na Makazi William Lukuvi Aziponda Nyumba Zinazojengwa na NHC,PPF

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema hakuna taasisi ya Serikali wala binafsi nchini iliyojenga nyumba za bei nafuu.

Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali imekusudia kuanzisha Sheria ya Mamlaka ya Kuratibu Shughuli za Ujenzi, itakayodhibiti bei za nyumba nchini.

Akizungumza jana katika mkutano na wajenzi kuhusu kusudio hilo la Serikali kuanzisha sheria na mamlaka hiyo, Lukuvi alisema taasisi zote zinazotumia wimbo wa nyumba za bei nafuu, hazisemi ukweli.

Alitoa mfano wa nyumba zilizojenga na Mifuko ya hifadhi za jamii na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na mashirika mengine binafsi na kudai ni za gharama nafuu kwamba zinauzwa bei inayoanzisha Sh milioni 50 na kuendelea. Alisema bei hiyo si nafuu hata kidogo kwa Watanzania walio wengi.

Kutokana na changamoto hiyo, Lukuvi alisema Serikali imetafuta wabunifu wa kujenga nyumba ya bei nafuu na kupata Kituo cha Social Business, kilichopo Babati mkoani Manyara wanaojenga nyumba ya vyumba viwili vya kulala kwa Sh milioni 15.

“Hebu fikiria kwa nyumba ya vyumba viwili huko Babati wanajenga kwa gharama hiyo wakati Dar es Salaam vifaa vyote vinapopatikana wanajenga kwa Sh milioni 50 na hapo Mtanzania wa kawaida atalipa kwa miaka 30 ya uhai wake wote,” alisema.

Kuhusu Sheria na Mamlaka ya Kudhibiti Ujenzi, Lukuvi alisema itakamilika mwaka huu kwa ajili ya kulinda wamiliki, wapangaji na Serikali kukusanya mapato yake.

 Alisema ni lazima kuwe na mfumo na sheria wa kusimamia wajenzi kwani wanasababisha kwa kiwango kikubwa miji kutopangika huku serikali za mitaa zikishindwa kukusanya mapato yake.

Lukuvi alisema ni lazima eneo hilo la ujenzi lisimamiwe kwani duniani kote ndiyo linalotumika kutakatisha fedha chafu.

Kuhusu watakaoshindwa kujenga nyumba za gharama nafuu, Lukuvi alisema pia wataweka haki za wapangaji hasa mijini kwani wanaandaa sera ya makazi na nyumba ili mpangaji awe na sheria inayomlinda.

Alisema kwa sasa mjenzi anapangisha nyumba kwa gharama kubwa hata kama haina baadhi ya vitu, hivyo lazima alipe gharama kulingana na ubora wa nyumba inayofanana na thamani ya fedha kwani wapangaji wengi wanalipa kulingana na anachotaka mlipaji.

Alipoulizwa kuhusu kodi kubwa kuchangia gharama za nyumba kuongezeka, Lukuvi alisema taasisi nyingi bado hazijajishughulisha na kutafuta teknolojia za ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, badala yake zimekuwa zikilalamika kodi za Ongezeko la Thamani (VAT) pamoja na kodi nyingine.

Alisema kama taasisi hizo zitafuata teknolojia katika nchi zilizoendelea, zitajenga nyumba za gharama nafuu ambazo kila Mtanzania anaweza kumudu.

“Bado nawapa changamoto, wasilete visingizio vya kodi, watafute teknolojia zilizopo huko duniani. Bado hakuna taasisi inayoniridhisha,” alisema.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Nehemia mchechu na jopo lake Ni majipu

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad