Athumani Machupa Aishauri Timu ya Simba Kukubali Kununuliwa na Mfanyabiashara Mohamed Dewji

Mchezaji wa zamani aliyewahi kutamba na klabu ya Simba na timu ya taifa ya Tanzania Athumani Machupa amevunja ukimya na kuamua kufunguka juu ya mwenendo mbovu wa klabu yake ya zamani.

Machupa amekuja juu pia kuhusu fukuzafukuza wachezaji inayoendela kwenye klabu hiyo ya Msimbazi kwasababu yeye pia ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kusimamishwa na kufukuzwa kwenye klabu hiyo.

Nyota huyo aliyekuwa mwiba kwa magolikipa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupasia nyavu, ameishauri pia klabu hiyo kumkabidhi timu MO  kama wanataka mafanikio ya mpira na biashara.

“Simba ndiyo klabu niliyoichezea toka nikiwa mtoto mpaka nakuwa Machupa, mimi ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa klabu ya Simba nadhani watanzania wengi wananifahamu. Kwasasa naishi Sweden ambako pia nafanya shughuli zangu huku nikiendelea kucheza mpira”.

“Klabu ya Simba imefanya vibaya msimu huu kutokana na kuongozwa kimazoea, klabu ya Simba ni kubwa na yenye hadhi barani Afrika lakini kwa sasa haijafanya vizuri katika medani zote kwa muda mrefu nyumbani na kimataifa”.

“Sidhani kama tumekaa chini na kujiuliza lakini upande wa uongozi nafikiri kila tunapofanya vibaya wanadhani tatizo linakuwa kwa wachezaji, lakini je, tatizo ni wachezaji? Na kama tatizo ni wachezaji kwanini wawe na wachezaji wenye matatizo?”

“Swali la pili, je uongozi upo sahihi? Kama uongozi haupo sahihi wachezaji hawawezi kuwa katika hali nzuri na kucheza kwa kiwango kizuri, kwasababu sasahivi mchezo wa mpira ni biashara. Ili ufanikiwe katika soka la kisasa ni lazima uwekeze pesa nyingi, ndiyo maana matajiri wengi duniani wanataka kununua timu kwasababu wanajua mpira ni biashara”.

“Klabu ya Simba inamatatizo ya kufukuzafukuza wachezaji, mimi pia nimewahi kufukuzwa Simba, wapo wachezaji wengine wengi ambao tayari wamewahi kufukuzwa  na kusimamishwa Simba. Mimi niliamua kuachana na Simba baada ya mkataba wangu kumalizika mwaka 2007”.

“Simba ya sasahivi haitakiwi kuongozwa hivi inavyoongozwa, Simba ya sasahivi haitakiwi kuwa na presha ya kufungwa inapokutana na timu kama Ndanda”.

“Simba inahitaji kupata mafanikio lakini sidhani kama viongozi waliopo madarakani wanajua wapenzi, wanachama na mashabiki wanataka nini”.

“Ukiangalia katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, wachezaji wengi wametoka Simba kwenda Yanga na siyo Yanga kwenda Simba, sidhani kama kuna wachezaji 5 au 6 waliotoka Yanga kwenda Simba”.

“Kessy kabla ya kuhamia Yanga alisimamishwa na uongozi wa Simba, unasimamishaje mchezaji kutokana na makosa ya uwanjani ? Inawezekana mchezaji hayupo sawa kisaikolojia kwasababu kuna baadhi ya mambo hajatimiziwa. Mchezaji mkataba wake unamalizika, kwanini msikae meza moja mkazungumza hata kama hamtofikia makubaliano basi mmnaachana vizuri. Lakini labda hatujui pengine alifanya makosa makubwa”.

“Tunaelekea kujiandaa na msimu mpya, viongozi waliopo madarakani wanamawazogani ? wana nini cha kuwaambia wanachama ?  Timu yetu imefanya vibaya kwa sababu gani?”

“Mambo ya kusimamisha na kufukuza wachezaji hadi lini ? Kama mchezaji ni mtovu wa nidhamu mtoeni hata kwa mkopo akacheze kwenye timu nyingine. Tubadilike, tujifunze kwa wenzetu maana tunafatilia vilabu vya nje basi tujifunze kutoka kwao pia”.

“Kama inawezekana, wampe timu MO  kwasababu hawampi timu bure, haichukui Simba na kuipeleka kwao Singida. MO ni mfanyabishara mkubwa barani Afrika na hakuna mtu ambaye ukimwelezea habari ya MO na Simba atakua haelewi kitu”.

“MO ni mwana Simba na anataka kuwekeza kwenye klabu yake anayoipenda tangu akiwa mtoto na anatoa pesa zake, mpeni timu aipeleke panapostahili kwasababu anajua mpira, anajua bishara na anajua Simba inatakiwa ifike wapi.Viongozi kaeni chini mzungumze na wanachama muwaeleze faida na hasara za kumpa timu MO”
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. HAJI MANARA SIMSIKII KABISAA,AU KAACHA KUWA MSEMAJI WA SIMBA?

    ReplyDelete
  2. ACHA TU WAISOME NAMBA WAJAA LAANA HAWA.
    1.YANGA
    2.AZAM

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad