Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), mkoa wa Dar es Salaam kimelaani kauli iliyotolewa na Mbunge wa CCM, Goodluck Mlinga ya kuwa ili wanawake wapate nafasi ndani ya chama hicho lazima waitwe 'baby' neno linalo maanisha kutumiwa kimapenzi.
Hivi karibuni akichangia mjadala wa Wizara ya Katiba na Sheria Milinga alitoa kauli hiyo iliyoibua mtafaruku Bunge hadi kusababisha wabunge wa wanawake wa Ukawa kutoka nje ya ukumbi huo baada ya kunyimwa mwongozo na Naibu Spika Dk Tulia Ackson.
Akizungumza jana nje ya eneo la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), akiwa na viongozi wenzake walipokwenda kuchangia damu Katibu wa Chadema Dar es Salaam Henry Kilewo alisema wamesikitishwa na kauli hiyo ilitolewa na mbunge alipewa dhama na kuaminiwa wananchi.
Alifafanua kwamba, ili uwe mbunge wa viti maalumu ndani ya Chadema kuna hatua nne za kupitia ikiwamo wanawake wenyewe kuchaguana ngazi ya wilaya kupitia Baraza la Wanawake la Chadema hivyo siyo rahisi kuwa na kitu kama hicho cha uhusiano wa kimapenzi.
"Kauli kama hizi zinapaswa kukemewa na kukomeshwa kwani zinawadhalilisha wanawake wote Tanzania. Lakini cha ajabu nimeshangaa hata wenzetu upande wa pili CCM wamekaa kimya bila kutoa kauli ya kukaripia," alisema Kilewo.
Alisema Chadema mkoa wa Dar es Salaam, inaungana na wabunge wa wanawake wa Ukawa kupinga kauli hizo za kiuni zilizotolewa na mbunge huyo wa Ulanga Mashariki aliyepigiwa kura wananchi mbalimbali wakiwamo wanawake.
Kuhusu suala la damu Kilewo aliwataka Watanzania wote kujijengea tabia ya kuchangia damu ili kuokoa maisha ya Watanzania wengine waliolazwa katika hospitali na vituo vya afya mbalimbali nchini.
"Chadema Dar es Salaam, tumeonyesha mfano tunaviomba vyama vingine viige mfano huu ili tuwasaidie watu wenye mahitaji ya damu,"alisema Kilewo.
Kwa mujibu wa Kilewo zaidi ya wanachama 40 wakiwamo viongozi wa Chadema mkoa huo wamechangia damu na kwamba mchakato huo utakuwa kila baada ya miezi watakuwa wakitoa msaada huo wa damu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Ruth Molel alisema wabunge wa viti maalumu wa Chadema wanaoteuliwa wote na wanataalumu zao na hawabahatishi kupata nafasi hizo kama Mlinga anavyodhani.
"Nimeumia nilivyosikia kauli hii ikitolewa na kijana yule ambaye ni kama mwanangu, kiukweli hajatutendea kina mama. Inaonyesha jinsi gani bado ana fikra za mfumo dume" alisema Molel.
Ofisa Habari wa MNH,Neema Mwangomo alisema kwa siku hospitali hiyo inahitaji damu kwa wastani uniti 80 hadi 100 lakini zinazopatikana ni 40.
Hata hivyo, Mwangomo aliwashukuru viongozi Chadema kwa moyo wao na kuwataka Watanzania wengine kujitokeza kutoa damu katika hospitali hiyo.
huna jipya vijembe bungeni ni kawaida na wananchitumezoea na kuho kutoka bungeni hakututishi ukweli ubnauuma
ReplyDeleteUkweli unauma kama njaa piippooozzz PWAAAAAAA
ReplyDelete