HUDUMA ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka imeanza rasmi jana jijini Dar es Salaam huku yakilalamikiwa na watumiaji wakiwemo baadhi ya watu waliokuwa na msamaha wa kusafiri bila kutoa nauli, ambao sasa hawatambuliwi na mfumo mpya.
Utaratibu uliokuwa umezoeleka awali wa askari wa polisi, jeshi, magereza na walimu kutolipa nauli kwenye usafiri wa daladala, umeonekana kugonga mwamba chini ya mabasi hayo. HabariLeo ilishuhudia mwalimu ambaye alikataa kutaja jina lake akitaka mwongozo wa kutolipa nauli kwa kuwa yeye ni mwalimu.
“ Mama mfumo huu haumtambui mwalimu, askari,” alimjibu mmoja wa wahudumu wa UDA-RT aliyekuwa akihakiki tiketi za abiria kabla ya kupanda basi.
Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UDA-RT, David Mgwasa alisema mwongozo uliotolewa na Sumatra, unamtambua mwanafunzi pekee ambaye anatakiwa kulipa Sh 200, wengine wote wanatakiwa kulipa nauli.
Mbali na walimu, askari, pia watu wenye ulemavu ambao walikuwa hawalipi nauli kwenye daladala, kwenye mfumo wa mabasi yaendayo haraka wanatakiwa kulipa.
Mambo mengine yaliyolalamikiwa ni mfumo wa ukataji tiketi, ambao unadaiwa kusababisha foleni ndefu huku wahudumu wakiwa hawana chenji, jambo lililosababisha baadhi ya watu kulipa kiasi kikubwa cha fedha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya abiria walisema walilazimika kukaa zaidi ya daika 20 vituoni kutokana kusubiri chenji na wengine kuamua kuacha fedha zao.
“Nimetoa Sh 1,000, nimepewa tiketi na kurudishiwa Sh 200 na kuwa hana Sh 150. Hapa inaonesha nimesafiri kwa Sh 800. Nauli hii ningeitumia kupanda daladala na kuzunguka nalo ili nipate kiti, ningepandia upande wa pili ningetumia Sh 500,” alisema Kasum Swakala, mkazi wa Ubungo Bonyokwa. “Nina haraka na siwezi kuipata hiyo 150 ambayo hawajanipa katika chenji yangu, inabidi tu kuondoka ili kuwapisha wengine lakini hali hii inatuumiza sana na siyo sawa kwa sababu kesho siwezi kurudi kuwadai chenji yangu,” alisema.
“Nimetoka Mbezi na kulipa 400, nimefika hapa wanasema hawana cheji kama nataka nilipe 800, siwezi kulipa kiasi hicho naenda kupanda daladala.”
Dada mmoja ambaye awali alimuuliza mwandishi eneo la kukatia tiketi baada kushuka na basi la Mbezi. Meneja Uhusiano wa UDA-RT, Deus Bugaywa alikiri kuwapo changamoto ya chenji na kusema asubuhi walikuwa na chenji nyingi ambazo ziliisha haraka hivyo kuleta usumbufu kwa baadhi ya abiria.
Mkazi wa Mbezi, Laurence Msuya alilalamikia hatua ya kukata tiketi mara mbili na kusema imesababisha usumbufu kwao kwa kupoteza muda. Wakala wa kukatisha tiketi katika kituo cha Mbezi alilalamikiwa kuchelewa kufika kwa jambo lililozidisha msongamano.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya UDA-RT, David Mgwasa alisema hali hiyo itaondoka pale mfumo wa kadi utakapoanza kufanya kazi.
“ Wananchi tuliwafundisha namna ya kutumia kadi, na siku moja kabla Serikali ikazuia matumizi yake, sasa tunasubiri maamuzi ili tuanze kuuza. Tulijua wananchi wangekuwa na kadi na wale wachache ambao ni wanafunzi na wale wanatumia mara moja moja ndio wangetumia tiketi za karatasi,” alisema Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), John Shauri alisema mfumo wa tiketi za kadi uko katika hatua za mwisho na mazungumzo. “ Ilikuwa ni lazima tuanze tiketi za karatasi, kwani tutakuwa na mifumo miwili inayofanya kazi hii ya tiketi za karatasi na kadi, mambo yakiwekwa sawa kadi zitaanza kutumika,” alisema.
Changamoto nyingine katika huduma hiyo iliyofanywa na baadhi ya wakala wa kukatisha tiketi kuzongwa au kutakiwa kutoa ufafanuzi ni pamoja na abiria kupewa tiketi za wanafunzi wakati wamelipa nauli ya watu wazima. Baadhi ya abiria walijikuta wakikata tiketi nyingine kutokana na za awali kuisha muda wake.
Hali hiyo ilitokana na wakazi hao kukata tiketi na kwenda kwenye shughuli zao nyingine na walipofika kituoni na kukuta muda wake umeisha walilazimika kukata nyingine.
“Awali walisema hizi tiketi unaweza kupandia basi wakati wowote lakini nashangaa leo nimekata tiketi nikaamua kwenda kwenye shughuli nyingine. Nimerudi hapa wakati tiketi inakaguliwa ikagoma kusoma kwa madai kuwa muda wake wa matumizi umeisha,” alisema mmoja wa wakazi wa Kimara Mwisho.
Akijibu hoja hiyo, Mgwasa alisema tiketi za karatasi zinatakiwa kutumika kwa safari moja na kuwa zinadumu kwa saa mbili kabla ya kuisha muda wa matumizi na ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi kukata tiketi pale tu wanapotaka kusafiri.
Tiketi zilizokuwa zikitolewa na mawakala wanaohusika zilikuwa hazina maelezo ya nauli waliyolipa abiria zaidi ya kuonesha tarehe, muda uliokata, kituo ulichokatia jambo ambalo liliwafanya abiria kuhoji na kuona ni ujanja wa kupoteza mapato ya serikali.