Majipu Mapya Tume ya Uchaguzi naTanesco Yaibuliwa Bungeni


Ripoti ya mwaka ya Mamlaka ya Udhibiti wa Umma (PPRA) imewasilishwa bungeni mjini Dodoma ikibainisha majipu katika utoaji wa zabuni katika baadhi ya mashirika na taasisi za umma ikiwamo Tume ya Uchaguzi na Tanesco.

Ripoti hiyo ya tathimini kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 iliyotiwa saini na mwenyekiti wa bodi, Balozi Dk Martin Lumbanga iliwasilishwa juzi na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashantu Kijaji, ikibainisha ukiukaji wa taratibu za zabuni, harufu ya rushwa na kupuuzwa kwa ushauri wa mamlaka hiyo.

Ununuzi wa BVR

Katika ripoti hiyo mamlaka hiyo inabainisha majipu kwa kutofuatwa kwa kanuni katika zabuni ya ununuzi wa vifaa vya kuandikisha wapiga kura (BVR).

Imeelezwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilipotangaza zabuni hiyo ya Dola 78.9 milioni (Sh 169.6 bilioni) kampuni ya SCI Tanzania Limited ilishinda zabuni hiyo lakini ikalalamikiwa.

Katika malalamiko yake, kampuni ya Safran Morpho ambayo pia iliomba zabuni hiyo, ilikata rufaa ikisema haikuridhishwa na mchakato mzima ulivyoendeshwa na SCI Tanzania Limited kushinda.

Baada ya kushughulikia rufaa, Mamlaka ya Rufaa ya Manunuzi ya Umma (PPAA) ilibaini kuwa SCI Tanzania Ltd haikuwa na uzoefu uliotakiwa, fedha, ufundi wala uwezo wa kuzalisha na ikaiagiza NEC kuanza mchakato wa zabuni upya.

Badala ya kutekeleza uamuzi huo, NEC iliwakaribisha tena wazabuni wote ambao walishindana katika zabuni iliyofutwa na vifaa vya kampuni ya Lithotec Export vilionekana kufanya kazi vizuri.

Ripoti hiyo inasema NEC iliamua kutumia utaratibu wa chanzo kimoja (single source) na kusaini mkataba na kampuni hiyo ya Afrika Kusini ya kusambaza BVR 10,500 zenye thamani ya Dola za Marekani 89 milioni (Sh191.3 bilioni), ikiwa ni ongezeko la Sh21.7 bilioni za awali.

Mbali na hilo, baadhi ya maofisa wa NEC walishiriki katika timu ya uthamini kwenye bodi ya zabuni na vikao vya majadiliano, hali iliyosababisha mgongano wa maslahi.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhan alipoulizwa alisema sheria ya manunuzi ya umma inaruhusu kupatikana mzabuni kwa njia ya ‘single source’ na kwamba hawakuwa wamevunja sheria yoyote na BVR 8,000 zilinunuliwa na watu wakapiga kura.

“Ni kweli PPAA walipoona mapungufu walitwambia turudie mchakato upya na sheria inaruhusu mzabuni mmoja kulingana na mazingira, hatukuwa kinyume cha sheria,” alisema Kailima.

Majipu Rahco

Katika hatua nyingine, PPRA imebaini madudu katika zabuni ya kuboresha Reli ya Kati iliyofanywa na kampuni ya Rahco, ambayo haikuwa katika mpango wa manunuzi kwa mwaka 2014/2015.

Mamlaka hiyo inadai mkurugenzi mkuu wa Rahco alijitwalia madaraka yote ya kuwa mamlaka ya uidhinishaji wa bajeti na yale ya bodi ya zabuni na kuidhinisha matumizi ya fedha.

Meneja mkuu wa manunuzi wa Rahco, alitoa ushauri sahihi kwa mkurugenzi huyo mwendeshaji lakini ushauri wake haukuzingatiwa na matokeo yake alibanwa na mkurugenzi huyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bodi ya zabuni ya Rahco haikushirikishwa kabisa katika mchakato huo wa zabuni ambapo kampuni ya CRCC and Integreted Communication zilipewa zabuni.

Jukumu la kuita wazabuni na kuwapa zabuni hiyo lilifanywa na mkurugenzi mwendeshaji wa Rahco pekee bila kushirikisha bodi ya zabuni, taarifa hiyo inabainisha.

PPRA imeeleza katika taarifa hiyo kuwa hakuna ushahidi wowote wa nyaraka kuonyesha ni kwanini mkurugenzi huyo aliivunja bodi ya zabuni iliyokuwepo na kuteua nyingine kabla ya muda wake kwisha.

Mamlaka hiyo imependekeza mkurugenzi huyo, Benhadard Tito afike mbele ya Bodi ya wakurugenzi ya Rahco kujieleza ni kwanini alikiuka kwa makusudi sheria ya manunuzi ya umma.

Vilevile mamlaka hiyo inaagiza bodi ya wakurugenzi kumchukulia hatua mkurugenzi huyo huku ikipendekeza suala hilo lipelekwe Takukuru ili kuchunguza uwepo wa mazingira ya rushwa.

Mamlaka hiyo ilipendekeza Rahco ijulishwe kuwa zabuni kati yake na makampuni hayo ni batili na ianzishe mchakato upya na pia kulipeleka suala hilo kwa mkurugenzi wa upelelezi (DCI) kwa uchunguzi zaidi.

Hata hivyo, Tito na mwanasheria wa Rahco, Emmanuel Massawe na mwakilishi wa kampuni ya RothChild Proprietary Ltd ya Afrika Kusini, Kanji Mwinyijuma wameshtakiwa kwa makosa tofauti na hilo la PPRA.

Tito ameshtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka na kula njama na kuisababishia Serikali hasara ya Dola 527,540 za Marekani.

NHIF na kampuni ya China

PPRA inabainisha kuwa zabuni ya Sh8.1 bilioni ilitolewa kinyume cha taratibu na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kampuni ya China Wuyi Co. Ltd.

PPRA inasema NHIF kupitia barua yake ya Agosti 28,2014, iliitaka mamlaka hiyo kufanya uchunguzi katika mchakato wa zabuni hiyo ikishuku kuwapo kwa mchezo mchafu.

Baada ya uchunguzi, PPRA ilibaini kuwa timu ya wathamini ya NHIF ilikosea kwa kupendekeza kampuni hiyo ipewe zabuni kwa sababu ilikuwa imefungiwa na Benki ya Dunia kufanya shughuli za manunuzi kuanzia mwaka 2009 hadi 2017.

Kutokana na makosa hayo, PPRA imemtaka ofisa aliyehusika kusaini zabuni hiyo kujieleza kwanini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kukiuka sheria kwa kuipa zabuni kampuni iliyozuliwa kushiriki manunuzi ya umma.

Pia mamlaka hiyo imependekeza kuchukuliwa kwa hatua kwa timu ya uthamini kwa kushindwa kubaini mapungufu hayo na hatua kama hizo pia zichukuliwe kwa bodi ya zabuni ya NHIF.

Tanesco na zabuni ya mafuta

Mbali na suala hilo, mamlaka hiyo pia imemtaka mwenyekiti wa bodi ya zabuni ya Tanesco kujieleza kwanini asichukuliwe hatua kwa kuiingiza kampuni ya Camel Oil (T) Ltd katika zabuni wakati iliondolewa kwa kukosa sifa.

Kampuni hiyo pamoja na Oryx Oil Company Limited ziliingizwa katika zabuni ya ununuzi wa mafuta mazito (HFO) kwa ajili ya mashine za kuzalisha umeme za kampuni ya IPTL.

Ripoti hiyo inafafanua kwamba shehena ya kwanza ya lita milioni 9 zenye thamani ya Sh12.4 bilioni zilinunuliwa kutoka kampuni ya BP na shehena ya pili ya lita milioni 16 yenye thamani ya Sh21.2 bilioni ikanunuliwa kutoka Puma.

Hata hivyo, PPRA imebaini mapungufu ikiwamo kutokuwapo kwa barua ya ushindi wa zabuni iliyotumwa kwa BP na pia hapa kuwa na hati ya makabidhiano (delivery note) kama ushahidi.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa kampuni ya BP ililipwa kwa kuegemea mzigo uliopakiwa wa lita 8,979,000 lakini shehena iliyoshushwa katika mitambo ya IPTL ilikuwa lita 9,970,106, ikiwa ni lita 991,106 zaidi.

Mamlaka hiyo ilibaini kuwa kutokana na zabuni hiyo, BP ililipwa Sh12.4 bilioni kwa hati ya malipo namba 58 VC 1100081 ambayo ilionyesha malipo hayo yalizidishwa kwa Sh42.4 milioni
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad