Mheshimiwa Rais Wanaodhani Wako Juu ya Sheria ni Wengi Sana...Soma Kisa Hichi

MIAKA michache iliyopita, wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ambayo imeshapita, kuna jambo moja lilinishangaza sana.  Jambo hili lilimhusu Waziri wa Serikali hiyo na mlinzi wa benki.
Kilichotokea ni kwamba Mheshimiwa Waziri alikwenda kwenye mashine ya kutolea fedha, maarufu kama ATM, huenda kwa ajili ya kutoa fedha.  Akiwa ndani ya kile chumba akaanza kuzungumza na simu. Akazungumza na simu kwa muda mrefu, hali iliyosababisha wateja waliokuwa wakiisubiri huduma hiyo kuanza kulalamika na kumlazimu mlinzi kumuomba Waziri awapishe wateja wengine waweze kupata huduma.

Hilo halikumfurahisha Waziri yule na badala yake akaanza kumwuliza mlinzi kama anajua yeye ni nani, kwa kuwa yeye kama Waziri ana mambo mengi ya maana na alikuwa akizungumza na simu muhimu.  Kwa huyo Waziri, suala la kuzungumza kwenye chumba cha ATM na kuwanyima fursa wateja wengine kama yeye kuipata huduma waliyokuwa wakiihitaji kwa wakati, halikuwa tatizo kabisa.

Sakata la Mheshimiwa Waziri na mlinzi wa benki liliripotiwa kwenye vyombo vya habari na bahati mbaya mwisho wake ulikuwa wa kusikitisha, kwani mlinzi alifukuzwa kazi kutokana na kutimiza majukumu yake.  Baadhi ya watu walipiga kelele, lakini hakuna kilichotokea.  Sana sana, baba wa watu akabaki bila kazi, huku akiwaza ataitunzaje familia yake iliyokuwa ikimtegemea.
Sasa juzi hapa hali hiyo imejirudia tena.  Safari hii, hata hivyo, imemhusisha Mke wa Mheshimiwa Waziri mwingine, ambaye alibishana na askari wa usalama barabarani aliyekuwa akitimiza majukumu yake ya kazi kwa kumweleza makosa ya barabarani aliyoyatenda.  Badala ya kusikiliza makosa yake na kuadhibiwa kwa kadiri ya matendo yake, mke huyu aliitumia karata yake ya kupitia mgongo wa mumewe na kutoa kauli za kuudhi zisizofaa kwa yule askari.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi kirefu sana, mambo yanaelekea kubadilika na wale waliokuwa wakidhani wapo juu ya sheria, wanakumbushwa tena kwamba Tanzania sio ya kwao peke yao.
Taarifa zinasema kwamba Rais John Pombe Magufuli ameamuru askari wa usalama barabarani aliyekuwa akifanya kazi yake na kuishia kutolewa maneno yasiyofaa na Mke wa Waziri, apandishwe cheo.  Vilevile, ameshamuonya Waziri na Mke wake kuhusiana na tukio hilo, kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Binafsi, taarifa hiyo imenifurahisha sana.  Tuseme tu ukweli kwamba Tanzania ilikuwa nchi ya ajabu sana.  Ilikuwa na matabaka makubwa sana kiasi cha watu kuzungumzia kutaka hata kukimbilia kuishi nje ya nchi, kutokana na kujiona hawathaminiwi, huku wengine wakitamba mitaani na kufukuzisha watu kazi kana kwamba wao ndio wamiliki halali wa nchi hii.

Tanzania ilifika mahali ambapo huyu askari wa usalama barabarani ambaye Rais ameamua kumpandisha cheo, angekuwa katika hali ngumu sana.  Kwanza angetafutiwa zengwe, kisha angehamishwa kituo cha kazi na kupelekwa kijijini huko kwenye kitengo cha kawaida kabisa.  Wale aliowaudhi, wangehakikisha kwamba jamaa harudi tena mjini, na anasahaulika kabisa.
Lakini yote hii ni kutokana na ulimbukeni wa kada fulani kudhani wako juu ya sheria na hawatakiwi kuguswa, huku sie akina yakhe tukiendelea kulipa faini halali na wakati mwingine kuadhibiwa na askari mwenye hasira za kutendwa na watu wa aina ya Mke wa Waziri.
Lakini pamoja na taarifa njema hizi tulizozisikia mwishoni mwa wiki, bado tuna safari ndefu sana.  Bado wapo watu wanaodhani wako juu ya sheria, hawatakiwi kuguswa na wanaruhusiwa kufanya chochote wanachojisikia kukifanya kwa kuwa wao ni wao na hawawezi kulinganishwa na Watanzania wengine.

Katika hili, naomba nizungumze na Mheshimiwa Rais na kumweleza maajabu ya Tanzania, ambayo bado hayajaandikwa kwenye Kitabu cha Guinness Book of Records.
Mheshimiwa Rais, hivi unafahamu kwamba kwenye nchi hii mtu akiwa na gari lenye nembo za Serikali, kama vile STK, huwa anavunja tu sheria za barabarani na haulizwi chochote?  Ataona watu wote tupo barabarani, tumesimama kwenye foleni, tunasubiri nafasi yetu ifike ili tuendelee na safari, lakini yupo radhi kupita hata njia za pembeni za watembea kwa miguu na hataguswa.  Eti ile nembo tu ya STK inamfanya awe juu ya sheria.

Mheshimiwa Rais, wapo pia hawa wengine ambao wanadhani kwamba kutokana na vyeo walivyonavyo, vyeo ambavyo aidha wewe ama watangulizi wao mmewapa, basi hata wakifika maeneo ya huduma za umma, kama vile hospitali, hawahitaji kufuata utaratibu wa kusimama kwenye foleni kama sisi wengine tufanyavyo.  Watafika, watawaona mmesimama, watapitiliza bila kuwasemesha huku wakiwa wamekunja nyuso zao kwa hasira na ukijaribu kuhoji, watakuuliza “unajua mimi ni nani?”  Hawa pia wanadhani wako juu ya sheria.

Mheshimiwa Rais, wapo pia wale ambao wanajiona wapo ‘grade’ ya juu zaidi.  Hawa hufikia mahala pa kutumia magari ya umma, magari ambayo sisi tunayalipia kodi ili yanunuliwe, yakarabatiwe na yajazwe mafuta, lakini wao kuamua kuyatumia kwa mambo yao binafsi.  Magari haya yatakwenda sokoni kununua mchicha na vitunguu, yatapaki saluni kumsubiri ‘mama’ ajiweke vizuri na yatapaki baa kusubiri bosi apate mapumziko ya kutosha, hata kama ni hadi usiku wa manane.  Yaani sisi tunakatwa kodi ili wao watumbue maisha, kwani wanadhani kwamba wako juu ya sheria.

Mheshimiwa Rais, wapo na wale ambao hata tukiwa kwenye foleni za benki, basi wao wataingia na kupitiliza ili wahudumiwe kwanza, kana kwamba wengine tuliosimama pale ni milingoti ya TANESCO na hatuna mambo mengine ya kufanya. Ukihoji, utasikia: “kwani wewe hujui mimi ni nani?  Nina mambo muhimu ya kitaifa ya kufanya.”  Unabaki unajiuliza, hivi kumbe kuna watu na WATU.  Kwa kila kitu, wao wapo juu ya sheria.

Naomba tu niseme kwamba hali hii ilikera kiasi kwamba tukaizoea na ndio maana hata Mke wa Waziri alipotoa maneno yasiyofaa kwa askari wa usalama barabarani, hakuna aliyejua kwamba askari yule angepandishwa cheo na Waziri kuonywa.  Sana sana, tulikuwa na uhakika kwamba hili litasambazwa sana kwenye mitandao ya jamii, huku wale wanaotukana askari kwamba wanachokitaka ni rushwa tu, wakiendeleza kauli hizo za kuudhi.

Watu walijiona kwamba wao ndio Watanzania halisi na wengine ni wa kusingiziwa.  Watu walijiona kwamba wao ndiyo pekee wenye haki miliki ya nchi.  Watu walijiona kwamba wao wako juu ya sheria. Mheshimiwa Rais, naomba nikuhakikishie kwamba watu hao bado wapo wengi…
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. KWELI KABISA,TUNASHUKURU HALI HIYO INAANZA KUBADILIKA SASA.HUKO KWENYE MAJUMBA YA STAREHE WATOTO WA WAKUBWA WAMETUNYANYASA SANA,
    JAMAA ANAKUNYANG'ANYA MKE HIVIHIVI ETI KISA NI MTOTO WA WAZIRI MBAYA ZAIDI UKIBISHA UNAONYESHWA MGUU WA KUKU.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad