Serikali imetangaza kuokoa kiasi cha Sh15.4 bilioni katika kipindi cha kuanzia Machi hadi Aprili 24 ambacho kingelipwa kwa watumishi hewa 8,236 ambao wamebainika hadi sasa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Angela Kairuki aliliambia Bunge jana kuwa kazi ya kuwasaka watumishi hewa bado inaendelea nchini kote.
Alisema watumishi hao wamebainika katika maeneo mbalimbali na kati yao 1,614 ni wa Serikali Kuu na 6,624 wa Serikali za Mitaa.
Waziri alisema kuwapo kwa watumishi hewa kumewafukuzisha kazi maofisa 56 na taratibu za kuwafungulia kesi mahakamani zinaendelea ikiwamo kutakiwa kulipa hasara yote ambayo waliisababisha.
Alisema mapambano dhidi ya watumishi hewa ni endelevu ili kukomesha tabia hiyo inayolitia hasara taifa.
“Mheshimiwa Rais alitangaza siku za hivi karibu na mtaona nami natangaza leo idadi ikiwa juu kuliko aliyotangaza Rais na vyombo vingine vitaendelea kutangaza maana tuko kwenye kazi kila siku,” alisema Kairuki.
Alitaja changamoto kubwa katika wizara yake ni kuwa ni tofauti ya mishahara kwa wafanyakazi ambayo inaonekana ni kubwa kati ya mtu wa chini na wa juu yake, jambo alilosema Rais ameamua kulisimamia ili kulipunguza.
“Tofauti ya mishahara ni kubwa, kuna baadhi ya maeneo mtu anatakiwa kupokea mshahara wa miezi 50 au 30 ili aweze kumfikia mwenzake mwenye mshahara mmoja tu,” alisema Kairuki.
Kuhusu suala la ajira, alisema katika mwaka wa fedha wa 2016/17, Serikali imepanga kuajiri watumishi 71,496 kuanzia mwezi huu na akawataka waajiri kuacha kuwahamisha watumishi endapo hakuna fedha za kuwalipa.