MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amecheza kwa dakika 45 tu, timu yake KRC Genk ikifungwa mabao 2-1 na KV Oostende katika mchezo wa Ligi ya mchujo Ubelgiji kufuzu michuano ya Ulaya usiku wa Jumamosi Uwanja wa Schiervelde mjini Roeselare.
Samatta alitolewa baada ya kipindi cha kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Mgiriki Nikolaos Karelis, wakati huo Genk inaongoza 1-0 kwa bao la Mbelgiji Thomas Buffel aliyefunga dakika ya 25.
Lakini akiwa benchi, Samatta aliishuhudia Genk ikifungwa mabao mawili kipindi cha pili la kwanza na Mzimbabwe Knowledge Musona dakika ya 71 na la pili na Jordan Lukaku dakika ya 90 na ushei.
Samatta leo amecheza mechi ya 14 tangu ajiunge na Genk akitoka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na TP Mazembe pamoja na kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
Katike mechi hizo, ambazo saba tu ndiyo ameanza, mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam, amefunga mabao nne, moja katika kila mechi Genk ikishindia 2-1 ugenini dhidi ya wenyeji SV Zulte-Waregem, 4-0 na 4-1 dhidi ya KV Oostende na 3-2 dhidi ya Club Brugge mchezo wa kwanza.