Upinzani Wamtega Rais Magufuli....Watumia Njia Mbadala Bungeni Kukumbushia Uuzwaji wa Nyumba za Serikali, Wadai MV Dar es Salaam Ni Jipu Lililoiva


Kambi ya Upinzani imelizidi maarifa  Bunge na kurejesha sakata la kuuzwa nyumba za Serikali ambalo juzi lilisababisha kiti cha Spika kuagiza yaondolewe maneno yanayomtaja Rais katika hotuba ya maoni mbadala.

Juzi, Kamati ya Kanuni za Bunge ilihariri hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ikiondoa maneno yanayomtaja Rais John Magufuli na badala yake kuweka neno Serikali kwenye sakata la uuzwaji nyumba za Serikali.

Kamati hiyo pia iliondoa suala la mkataba wa Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises, rushwa, mauaji ya wanasiasa, mwenendo wa Rais na Bunge kulinda wahalifu, jambo lililomfanya msemaji wa kambi hiyo, Godbless Lema kukataa kusoma hotuba yake.

Lakini jana katika hotuba ya kambi ya upinzani kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, mbunge wa Vunjo, James Mbatia alilirejesha sakata hilo akieleza kuwa ni muda sahihi kwa Rais John Magufuli kurekebisha kasoro zilizojitokeza wakati akiwa waziri ili kurejesha imani katika jamii.

Mbali na sakata hilo, pia Mbatia alizungumzia sakata la kivuko cha Mv Dar es Salaam ambacho kinatakiwa kifanye safari kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, akikielezea kuwa “ni jipu ambalo limeiva kwa viwango vyote na sasa linatakiwa litumbuliwe mara moja”.

Suala la Mv Dar es Salaam liliungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Zitto alisema kuwa hoja ya kivuko hicho lazima ichukuliwe hatua ili iaminike kuwa kuna nia ya dhati ya kupambana na ufisadi nchini.

“Naona suala hili linakwepwakwepwa, hivyo litolewe maamuzi,” alisema Zitto.

Pia mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema suala la Mv Dar es Salaam kuwa iko chini ya kiwango, liliwahi kusemwa na mbunge wa upinzani lakini Serikali ikakataa.

Hata hivyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) amesema ukweli katika ripoti yake. “Hili suala inabidi liangaliwe kwa kuwa kuna watu wanahitaji kutumbuliwa hivyo hao watu waangaliwe,” alisema Selasini.

Akisoma hotuba ya maoni mbadala ya kambi ya upinzani, Mbatia alisema wakala wa majengo nchini ndiye muhusika mkuu katika kuhakikisha nyumba za Serikali zinakuwa katika hali nzuri kwa watumishi wa Serikali kuishi.

“Katika muktadha huo, kambi ya upinzania inalikumbusha Bunge kwamba kati ya mwaka 2002 mpaka 2004 Serikali iliuza nyumba 7,921 na mpaka mwaka 2008 ilikuwa imejenga nyumba 650 tu,” alisema Mbatia.

Alisema katika biashara hiyo ya kuuza nyumba zilizokuwa mali ya Tamisemi, Serikali ilipata Sh252 milioni lakini sasa inahitaji kusaka zaidi ya mara mbili ya kiasi hicho kujenga nyumba za fidia.

Mbatia alisema Serikali ingetumia Sh677.6 milioni kujenga nyumba mpya ili zirejeshwe Tamisemi.

“Kwa vile hata wale waliouziwa nyumba hizo, kuna taarifa kati yao wapo walioziuza na kujipatia faida kubwa kinyume na mikataba ya mauzo hayo, kambi ya upinzani inapendekeza wanyang’anywe nyumba hizo kwa kukiuka mikataba na malengo ya mauzo.”

Mbatia alisema kumbukumbu rasmi za Bunge zinaonyesha Serikali ilitoa taarifa kuwa kamati iliundwa kuchunguza mchakato wa mauzo ya nyumba hizo na ilitarajiwa kumaliza kazi Februari 2007, lakini hadi leo hakuna taarifa iliyotolewa na Serikali na kuitaka Serikali ya Awamu ya Tano izirejeshe.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad