Usiyoyajua Kuhusu Bia ya Tanzania Iliyopachikwa Jina la Utani la ‘Ukawa’

 “Nipatie Ukawa hapo”, “lete Ukawa chapu chapu” hayo ni maneno utakayoyasikia siku hizi ukiingia baa mbalimbali za mtaani jijini Dar es Salaam.

Mbali na maneno hayo pia utawasikia vijana wakisema, “Naenda kujiunga, najiunga cha buku (Sh1, 000) halafu nakuja”. Kama huelewi wanachozungumza wanywaji hao, unaweza kujiuliza Ukawa ni nini au mtu anapoenda kujiunga anajiunga na nini.

Ukisikia baa watu wanasema leta Ukawa basi ujue hiyo ni bia aina ya Pilsner Lager na ukisikia mtu anaenda kujiunga ujue basi anaenda kunywa bia aina ya Eagle Draught, ambayo wateja hukinga glasi kwenye mtungi maalumu.

Kwa nini inaitwa Ukawa?
Watumiaji wa kinywaji hicho wanaeleza kwamba ni kutokana na gharama yake kuwa nafuu na ndiyo maana inaitwa jina hilo ambalo ni maarufu kutokana na Umoja wa Katiba ya Wananchi, unaojumuisha vyama vinne vya upinzani vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Wanaeleza kuwa kutokana na Ukawa sera yao kuwa ni mabadiliko na maisha nafuu kwa wananchi na Pilsner inauzwa Sh1,500 tofauti na bia nyingine zenye ujazo sawa zinazoanzia Sh2,300 na kuendelea, wanaona imekuwa nafuu kubwa kwao na ndiyo maana wakaiita Ukawa.

“Hii bia bwana ni nzuri na ni nafuu, yaani hawa jamaa wametufaa sana na ndiyo maana tunaiita Ukawa kwa kuwa inatia matumaini kwa kutupunguzia gharama za unywaji,” alisema Kiongozi Njau alipokuwa akijipatia bia ya yake ‘Ukawa’.

Njau na wenzake ambao walikuwa wamejaza chupa za Pilsner mezani huku wakipiga kelele na kueleza furaha yao kuwa bei hiyo ya Sh1,500 ambayo ni rahisi kuimudu inawapunguzia mzigo wa kunywa vinywaji ambavyo havina kiwango.

Ilianzaje kuitwa Ukawa?
Njau alisema wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana mmoja wa wagombea wa Ukawa, mkoani Kilimanjaro aliingia baa na kutaka kuwanunulia kinywaji watu waliokuwapo katika baa hiyo.

“Sasa huyo jamaa akajiuliza hawa wako wengi nitawanunulia bia ipi ambayo haina gharama sana, ndiyo akanunua Pilsner zikawekwa mezani, basi wanywaji wakaanza kuimba Ukawa, Ukawa, Ukawa, ndiyo ikawa hivyo tena hadi leo inaitwa Ukawa,” alisema.

Victor Temba, mnywaji mwingine wa bia hiyo alisema, “ukiwa na Sh10,000 unakunywa Ukawa zako sita na unabakiwa na ‘buku’ (Sh1,000) au ukiwa na Sh5,000 unakunywa zako tatu na ‘jelo’ (Sh500) linabaki la nauli, unataka nini tena?

Alisema wameiita Ukawa kwa kuwa ni bia ambayo wananchi wanaweza kumudu kuinunua.

“Sijui hicho kiwanda kilifikiria nini? Yaani kimeileta wakati muafaka kama vyama vya Ukawa vilivyojiunga na kutupa matumaini wakati wa kampeni,” alisema Temba.

Mmoja wa wauzaji wa bia hiyo eneo la Mabibo External jijini Dar es Salaam, Dickson Mwarabu alisema Ukawa inanyweka na watu wa ngazi tofauti tofauti.

“Ninauza Ukawa kama sina akili nzuri, inapendwa kwa kuwa ni nafuu na iko vizuri. Mimi mwenyewe huwa naipiga ikifika jioni. Hainitii hasara katika faida ninayopata kila siku,” alisema Mwarabu.

Ofisa uhusiano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ambayo ndiyo inazalisha Pilsner, Abass Abraham alisema bidhaa hiyo imesajiliwa kwa jina la Pilsner, hivyo kama watumiaji wameamua kuipa jina lao ni sawa, lakini kisheria na kibiashara jina la bidhaa hiyo litabaki kuwa Pilsner.

Alisema bia hiyo inauzwa Sh1,500 na inatengenezwa kwa asilimia 100 na malighafi za ndani.

“Tunajivunia ubora na ladha ya Pilsner. Ni bia pekee Tanzania inayotengenezwa kwa kufuata utaratibu ulioanzia Jamhuri ya Czech mwaka 1840,” alisema Abraham.

Wanaojiunga je?
Wakati wateja wa SBL wanafurahi na Ukawa, wenzao wa Tanzania Breweries Ltd (TBL) wanafurahia “kujiunga” kwa kunywa bia ya Angle Draught inayouzwa Sh500 kwa glasi.

Vinnie Msewa alisema kuwa kutokana na bia hiyo kuuzwa kwa kupimwa, wanaweza kupata kipimo cha Sh500 kwenda juu, hivyo ni rahisi kwao kuimudu.

“Naenda kujiunga kaka baada ya hapo nitapiga Ukawa mbili mambo yanakuwa poa,” alisema.

Hata hivyo wauzaji wa bia hiyo hawakupenda kuzungumzia jinsi wanywaji wanavyojiunga kwa kupata vipimo vya kinywaji hicho.

Meneja Masoko wa TBL, Fimbo Butallah alisema bia hiyo huzalishwa na kuwekwa kwenye mitungi ambayo imeondoa gharama ya kuweka kwenye chupa, ndiyo maana wanywaji huweza kuipata kwa bei rahisi.

“Tulifanya utafiti tukagundua watu wengi wanatamani kunywa bia, lakini hawana uwezo wanaishia kunywa vinywaji visivyo halali kama gongo,” alisema Butallah.

Alisema baada ya utafiti huo waliamua iwe inauzwa kati ya Sh600 kwa glasi ya ujazo wa mililita 300 na kwa mililita 500 ni Sh1,000 jijini Dar es Salaam ambako kwa mtu hupata kinywaji hicho kwenye glasi kwa gharama nafuu.

“Imewasaidia watu kuacha kunywa vinywaji visivyo halali. Tumewaangalia watu wenye kipato cha chini. Bia hii inatengenezwa asilimia 100 na mtama unaolimwa hapa Tanzania,” alisema.

Wenye Ukawa wanasemaje?
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene akizungumzia suala la bia hiyo kuitwa Ukawa alisema, “Kwanza inaeleza kuwa Ukawa inaongoza na CCM inatawala kwa kuwa ukiongoza watu unaishi kwenye mioyo na akili zao.” Alisema Ukawa ilipofikia leo iko kwenye mioyo ya watu na akilini mwao.

“Kwa namna wananchi walivyokata tamaa, wamepata matumaini na Ukawa kwa kuwa iko mioyoni mwao. Inaonyesha Ukawa iko juu.”

Makene alisema ni watu kutafuta uhafadhali wa mambo katika maisha. “Tunafurahi kuwa kuonwa sisi ndiyo tumaini lao yaani wanaona Ukawa ndiyo wenzao.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad