MAWAZIRI wa Serikali ya Awamu ya Tano wamewajia juu wabunge wa upinzani na wananchi wanaovishutumu kila mara vyombo vya ulinzi nchini na kuwataka kuacha kuvihusisha vyombo hivyo na masuala ya kisiasa.
Mawaziri hao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.
Wamewataka wananchi na hususani wabunge wa vyama vya upinzani, kutambua kuwa vyombo hivyo vya ulinzi ambavyo ni pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Polisi wajibu wake mkubwa ni kulinda mipaka ya nchi na usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza wakati wa mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara inayoshughulikia Muungano na Mazingira, Dk Mwinyi alisema haijawahi kutokea na wala haitotokea jeshi kutumika kisiasa.
Alisema Jeshi la Tanzania limekuwa likitekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria iliyojiwekea pamoja na za kimataifa na wala hata siku moja haliwezi kutumika kwa ajili ya kutumiza malengo ya kundi fulani.
“Jeshi letu lina sifa ya kimataifa ya ulinzi wa amani, dunia kote tunasifika kwa weledi, kulinda amani na mipaka yetu. Haijawahi kutokea wala haitotokea jeshi kujiingiza kwenye shughuli za kisiasa,” alisisitiza Dk Mwinyi.
Alisema tangu mjadala wa makadirio ya bajeti hiyo uanze, baadhi ya wabunge hususani wabunge wa upinzani wamekuwa wakilitupia shutuma nzito jeshi na vyombo vya dola kwa ujumla kuwa limetumika vibaya kwenye uchaguzi wa Zanzibar na chaguzi nyingine.
Aliwataka wabunge hao pamoja na wananchi wanaovilaumu mara kwa mara vyombo hivyo vya dola kumuogopa Mungu kwa kutoa madai ya uongo dhidi ya vyombo vyao vya ulinzi na usalama.
Alisema madai kuwa jeshi hilo limetumika na kuandikisha wananchi kwenye kambi zao za jeshi visiwani Zanzibar si ya kweli na kama kuna mwenye ushahidi auwasilishe ili ukweli ujulikane.
Dk Mwinyi alisema amesikitishwa na madai ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu masuala ya Muungano, Ally Abdallah Saleh kwamba Zanzibar imetekwa na jeshi la Tanganyika kana kwamba nchi iko katika vita.
“Naomba nikujibu kwanza ili ufahamu kuwa hakuna jeshi la Tanganyika, jeshi ni moja na ni la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Naomba nimuelimishe kazi kubwa za jeshi ni ulinzi wa mipaka, ulinzi wa amani na kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia au vyombo vingine vya ulinzi na usalama inapohitajika kufanya hivyo,” alisema.
Alisema inapotokea matukio makubwa kama shughuli ya uchaguzi, duniani kote si Tanzania pekee, majeshi yote yanakuwa tayari kukabiliana na hali yoyote na ndio maana askari wake wanakuwa kwenye sare za kombati.
Kuhusu madai ya kambi hiyo ya upinzani kuwa Jeshi limekuwa likitumika kulazimisha Muungano, Dk Mwinyi alisema JWTZ ni kielelezo cha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane mwaka 1964, jeshi ni moja na kamwe halijawahi kulazimisha utawala, ila lipo hadi Zanzibar kwa sababu ya kulinda mipaka ya Tanzania, na Zanzibar ni sehemu ya Tanzania.
“Tangu mwaka 1964 jeshi lina vikosi vyake Zanzibar na siku zote vikosi hivi huwa na silaha, sasa tuna haja gani ya kupeleka wanajeshi na silaha wakati miaka yote vyote viko huko? "Alihoji Dk Mwinyi.
Naye Naibu Waziri Masauni alisema hoja kwamba jeshi lilitumia mabavu Zanzibar na askari walikuwa ni wengi si ya kweli.
Alisema kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, kila kituo cha uchaguzi kinahitajika angalau askari wawili wakati Zanzibar kulikuwa na vituo vya uchaguzi zaidi ya 3,000 na askari waliopo visiwani humo ni 5,000.
Alisema kwa hali ilivyokuwa askari wa Zanzibar walikuwa hawatoshi kwani wangesambazwa wote wasingetosha kuweka ulinzi na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu na usalama.
Kuhusu madai kwamba Katiba imekiukwa, aliutaka upande wa upinzani kujiuliza kati ya madai yao ya kumtaka Rais John Magufuli aingilie mamlaka ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) au Polisi kulinda raia na mali zao, kipi ni uvunjifu wa Katiba.
Alifafanua kuwa majukumu ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kulinda usalama wa raia na mali zao hivyo bila kujali cheo au utajiri wa mtu yeyote endapo atavunja sheria atachukuliwa hatua za kisheria.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alisema uchaguzi wa Zanzibar ulikamilika kwa usalama na kwamba pamoja na malalamiko ya vichochoroni kuhusu uchaguzi huo, hakuna hata mmoja aliyefungua kesi kupinga matokeo mahakamani.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ni ruhusa mtu asiporidhika na matokeo ya uchaguzi, kufungua kesi ya kuyapinga, lakini tangu uchaguzi huo umalizike hakuna mtu kutoka jimbo lolote visiwani humo aliyefungua kesi.
Naye January alisema kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, Mahakama Kuu ya Zanzibar ndio pekee yenye uwezo wa kusikiliza na kuamua masuala yote yanayohusu uchaguzi wa Zanzibar.
VYOMBO vya Majeshi Tanzania Kuusishwa na Siasa Yazua Balaa....Mawaziri Waja Juu
1
May 04, 2016
Tags
JWTZ itakuwa huko kwa suala la ulinzi na usalama hivyo hakuna cha kuzuia. Wanataka lisiwepo hili wafanye nini?
ReplyDelete