Wakati wataalamu wa uchumi na sheria wamepinga utaratibu wa bei elekezi ya sukari, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), imesema haina vibali vinavyosubiriwa na wafanyabiashara wa bidhaa hiyo.
Pia, wachumi hao wamekosoa kamatakamata ya wanaodaiwa kuficha sukari, baada ya Rais John Magufuli kuagiza vyombo vya dola viwakamate na kuigawa bure kwa wananchi sukari inayokatamwa .
Kuhusu bei elekezi, wachumi hao walipinga utaratibu uliotangazwa na Bodi ya Sukari (SBT), kwamba bei ya sukari itakuwa Sh1,800 kwa kilo moja.
Hoja ya bei elekezi pia, ilipingwa na Profesa wa Uchumi, Ibrahim Lipumba kwamba si kazi ya Serikali kupanga bei, na kuhoji hata bei iliyotangazwa haijulikani ni kwa mauzo ya jumla kutoka kiwandani au kwa wateja wa rejareja kwenye maduka ya mitaani.
Akizungumza katika kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa na ITV juzi usiku, Mtafiti wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Haji Semboja aliitaka Serikali kuacha soko ndiyo liamue bei.
Dk Semboja alionya hatua ya Serikali kuweka bei elekezi, kwamba kutakimbiza wawekezaji katika sekta ya sukari na kuwaumiza wakulima wa chini, wanaotegemea miwa kupata kipato chao.
“Ili tutatue tatizo hilo, itabidi wadau washirikishwe. Jukumu la Bodi ya Sukari kwa sasa ni kuratibu tu mfumo, siyo kuweka bei elekezi. Ni kama Ewura (Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Maji) wanavyofanya, kama Tanesco hivi karibuni walipendekeza wenyewe, ikazungumziwa na wadau mpaka Ewura wakaipitisha,” alisema.
Dk Semboja alisema licha ya viwanda vilivyopo kuzalisha kiasi kidogo kuliko mahitaji, bado kodi ya bidhaa imechangia bei kupanda.
Hata hivyo Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Suleiman Nyakulingwa alimpinga Dk Semboja, akisema bei elekezi imetokana na utafiti uliofanywa na kwamba Serikali imeshusha kodi ya sukari.
“Kodi ya Serikali ilikuwa asilimia 100, lakini Serikali imepunguza hadi asilimia 25 ili kupunguza gharama za uzalishaji na ununuzi wa sukari ili mwananchi wa kawaida aipate katika bei inayokubalika,” alisema Nyakulingwa.
Akifafanua jitihada za Serikali, Nyakulingwa alitoa mfano wa kontena 70 zilizotolewa bandarini kwa msaada wa kampuni binafsi ya Ticts iliyopunguza gharama za kutoa mzigo jumla ya Dola za Marekani 448,880.
Judith Kapinga kutoka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) alikosoa operesheni ya ukamataji na utaifishaji wa sukari akisema ni kinyume cha sheria.
“Kuna sheria nyingi zinazodhibiti bidhaa kama sukari, kwa mfano Sheria ya Makosa ya Uhujumu uchumi ya mwaka 1984 inatoa mwongozo wa kushughulikia makosa hayo, siyo tu kutaifisha sukari,” alisema na kuongeza:
“Sheria hiyo inasema, baada ya mahakama kujiridhisha kwamba kuna mazingira ya kuhodhi sukari, Inspekta wa Polisi anaweza sasa kuendelea kuanzia hapo…
“Siyo tu unapotuhumiwa kuhodhi sukari, basi inaweza kutaifishwa hapo hapo na kusambazwa. Kuna taratibu za kisheria zinazoelezea mazingira ya kuhodhiwa sukari nini kifanyike.”
Mkuu wa Sheria na Mashtaka wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Donasian Kessy alisema kinaachofanyika ni kubainisha wafanyabiashara hao na kuwachunguza.
“Katika zoezi zima linaloendelea, tumeanza kubainisha kama kuna watu wanahodhi hiyo bidhaa. Kama unavyoona bidhaa imekutwa kwenye maghala na nyingine imekutwa bandarini ikisubiri taratibu za forodha ili itoke,” alisema.
TFDA yakana
TFDA imetoa tamko kwamba haina vibali vyovyote vinavyosubiriwa na wafanyabiashara waliodai kwamba sukari yao iko kwenye maghala kwakuwa inasubiri vibali toka kwao.
Akizungumza jana Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa TFDA, Gaudensia Simwanza alisema utaratibu wa kutoa vibali huanzia bodi ya sukari ambayo huangalia uhaba katika soko na ndiyo inatoa ruhusa kwa wafanyabiashara kuingiza nchini.
Alisema muda wa kutolewa kwa vibali hivyo unategema na uchunguzi wa ‘parameter’ mbalimbali za kupimia, kwani kibali hakitolewi papo hapo, lakini kwa kipindi hiki hakukuwa na mtu aliyesubiri kibali.
“Kumbuka kulikuwa na tatizo la sukari na Rais Magufuli aliagiza watafutwe walioficha sukari, sisi tunahusika na vibali na hakukuwa na vibali vilivyokuwa vikisubiriwa, hata kama alishapatiwa kibali cha TFDA sisi hatukutoa ili afiche sukari,” alisema Simwanza.
Alisema TFDA inaendelea na uchunguzi wa sampuli za sukari iliyokamatwa kama wanavyopewa maelekezo kuzichunguza sukari hizo.