Kijana Lucas John (32) anayeishi Kijiji cha Ngombezi, wilayani Korogwe, Mkoa wa Tanga, anaugulia maumivu nyumbani kwao akiwa kitandani baada ya kupata ulemavu wa kudumu kwa kukatwa miguu na mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana.
Kabla ya kukumbwa na mkasa huo, kijana huyo ambaye ni mlemavu na mwenye kuzungumza kwa shida kutokana na kushindwa kutamka maneno vyema, alizoeleka kuonekana mitaani Korogwe mjini akiomba fedha kwa wasamaria wema zilizosaidia familia yake kujikimu.
Mama wa kijana huyo, Herieth Mndolwa alilielezea Uwazi kwamba Lucas ni yatima baba yake alifariki kwa ajali na hivyo kulazimika kuishi naye katika mazingira magumu baada ya kutokuwa na kazi wala kipato cha kuwawezesha kupata mlo wa kila siku.

Nyumba anayoishi Kijana Lucas John.
Alisema kuwa mwanawe alitoweka nyumbani tangu Mei 4, mwaka huu, hali iliyompa wasiwasi kutokana na ukweli kuwa haikuwa kawaida ya Lucas kutokurejea nyumbani kwao hatua iliyosababisha kutaka kujua alikokwenda.
Katika jitihada za kujua ni wapi kijana wake alielekea, Herieth alisema kwamba alilazimika kuomba msaada katika Kanisa la Pentekoste anakosali ili kumuombea kwa Mungu ambapo ibada ilifanyika na siku chache baadaye ndipo alipofanikiwa kupata taarifa juu ya kijana wake huyo.
Hata hivyo, mama huyo ambaye tukio hilo analihusisha na imani za kishirikina alieleza kuwa alipata taarifa za kijana wake huyo kuwepo Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo na kulazimika kwenda kumuona na kudai kuwa alimkuta akiwa amekatwa mkono wa kulia, mguu wa kushoto na unyayo wa kulia.
Kwa mujibu wa mama huyo, baada ya kumkuta mwanaye katika hali hiyo alilazimika kwenda polisi kujua kilichojiri na kueleza kuwa taarifa alizozipata polisi zinadai kuwa kijana huyo aligonga treni na kwamba aliokotwa relini kauli ambayo ilimuumiza sana na kuacha maswali kwake.
Kutokana na taarifa hizo aliamua kudai viungo vya mwanaye lakini polisi walimjibu kuwa vilibebwa na kunguru jambo ambalo hakukubaliana nalo na kutaka apewe maelezo zaidi kuhusiana na viungo hivyo.
“Polisi waliniambia mama usijaribu kufuatilia tukio hili ni baya kwani mwanao amegonga treni na kisheria anatakiwa kushitakiwa kwa kuligonga treni na wakanishauri niondoke kabla sijakamatwa, nikakimbilia nyumbani bila kupata viungo vya mwanangu,” alisema Herieth.
Aidha, aliongeza kuwa utata mwingine ni wa maelezo ya Lucas ambayo yanapingana na taarifa ya polisi ya kupata ajali na badala yake anaeleza kuwa alikatwa viungo hivyo na watu huku akimtaja kwa jina mmoja wao na jinsi alivyomfikisha katika eneo la tukio alikookotwa.
Herieth anaomba msaada wa serikali, taasisi na wasamaria wema wenye moyo wa kusaidia kutokana na mateso anayoyapata Lucas ambayo yanachangiwa na umaskini wake ili kumpatia matibabu kwani kila siku analazimika kusafirishwa hadi Hospitali ya Wilaya Magunga kwa matibabu baada ya kuruhusiwa Bombo.
“Mimi siamini kama mwanangu amekatwa viungo na treni kwa sababu hakuna mguu wala mkono uliookotwa, kunguru gani anaweza kubeba mguu na mkono? Mbona mtoto anawataja watu waliomkata na kwenda kumtupa relini?” alihoji mama huyo.
Kijana huyo alisema alichukuliwa na mtu Hale wilayani Korogwe na kusafiri naye hadi Tanga Mjini kwa pikipiki ambapo baada ya kumfanyia unyama huo, mtu huyo akiwa na mwenzake walimtelekeza relini.
Lucas anaomba msaada kwa kuwa maisha anayoishi ni magumu na anakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo matibabu na kujikimu kimaisha kwani mama yake hawezi majukumu hayo kutokana na kutokuwa na uwezo.
Aliyeguswa na habari hii anaweza kumsaidia Lucas kupitia simu namba 0715824043 au
0754824043.