JUKWAA la burudani linafahamu kuhusu hali aliyonayo Mbongo Fleva, Rashid Makwiro ‘Chid Benz, ‘unga’ unamtesa na kumfanya kuporomoka kwa kiwango kikubwa kutoka kileleni kwa ubora hadi kuwa mtu anayeonewa huruma, kwa sababu hali yake kiafya imetetereka kiasi cha kuhitaji msaada, Wikienda linakupa zaidi.
Ingawa kipindi cha nyuma aliwahi kukana kwa nguvu zote juu ya matumizi ya unga (madawa ya kulevya), lakini siku zote maradhi hayajifichi na hatimaye, Chid Benz aliibuka hadharani na kuomba msaada kutoka kwa wadau, ili angalau awezeshwe kuachana na utumiaji wa unga, kitendo ambacho kilipokelewa kwa mikono miwili na wadau wa burudani.
Chid anakuwa msanii mwingine mkubwa, anayesukumwa nje ya ‘game’ kutokana na kuathirika na madawa hayo, akifuata nyazo za Rehema Chalamila ‘Ray C’ na aliyekuwa mwandani wake, Lord Eyez.
Kati ya watu waliojitokeza kumpa msaada ni pamoja na Hamis Taletale ‘Babu Tale’ ambaye ni meneja wa muda mrefu wa Kundi la Tip Top Connection lakini kwa sasa pia yupo katika benchi la viongozi ndani ya Lebo ya Wasafi (WCB).
Tale na Mbongo Fleva, Kalama Masoud ‘Kalapina’ walimpeleka Chid katika kituo cha kuwasaidia waathirika wa madawa ya kulevya ‘Sober House’ kilichopo Bagamoyo, Pwani ambako alipokelewa na uongozi katikati ya Machi, mwaka huu na akawa tayari kukabiliana na changamoto zilizopo mbele yake ili mradi aachane na ‘ujinga’ huo unaowapoteza vijana wengi.
Tale aliuambia umma kupitia baadhi ya vyombo vya habari kwamba, atakuwa tayari kuhakikisha Chid anarejea katika ubora wake. Lakini kule Sober House, msanii huyo alikaa siku 28 tu, akang’ang’ania kuondoka siku ambayo meneja huyo alikwenda kumtembelea.
Waandishi wa makala haya walidokezwa kuhusu kutokuwepo kwa Chid kule Sober, wakafunga safari hadi huko ambako uongozi wa kituo hicho ulikiri kuondoka kwa msanii huyo kabla ya muda aliostahili. Meneja wa kituo hicho, Tumaini Majira alisema angalau angekaa miezi mitatu ingesaidia.
Baada ya habari ile kutoka, takriban wiki mbili baada ya Chid kuondoka katika kituo hicho, Babu Tale alikuja juu akikanusha kuhusu msanii huyo kutoroka matibabu licha ya ukweli kuwa kabla ya habari hiyo kuandikwa, yeye kama mtu aliyempeleka, alipigiwa simu na kuombwa maoni yake,
lakini alikataa kusema lolote akidai kwa sasa hataki kusema, muda muafaka ukifika atafunguka.
Kuna vitu viwili hapa, kwanza Babu Tale alikaa kimya bila kuwataarifu Watanzania ambao awali alikuwa ‘laini’ ya mbele kupitia ‘media’ kusema juu ya nia yake ya kumsaidia Chid.
Kabla ya habari ya kutoroka Sober kuripotiwa na Global Publishers, wadau walikuwa wakijua msanii huyo anaendelea na matibabu.
Sijui ni kwa nini Tale alificha juu ya Chid kuondoka Bagamoyo kabla ya wakati? Kibaya zaidi, akatumia nguvu kubwa kukanusha kuhusu kutoroka, akipingana na meneja wa kituo hicho, aliyeongea kitaalam. Babu Tale aliuambia umma kuwa, msanii huyo hakutoroka, isipokuwa muda aliokaa ndiyo aliotakiwa!
Shame on him! Hakuna mwathirika wa unga wa kiwango cha Chid aliyewahi kutumia dawa za kumsaidia kuwa fiti kwa siku 28 kisha akawa sawa.
Lakini achana na hilo, habari mpya ni kwamba, baadhi ya wasomaji wetu walitaka kujua hali ya Chid kwa sasa baada ya kuwepo kwa madai kwamba, amerejea katika matumizi ya unga. Hivyo, ili kupata ukweli, gazeti hili lilitaka kujua, likatumia mbinu zote kumtafuta ili kuzungumza naye, lakini Babu Tale alifanikisha kwa kiwango kikubwa Chid Benz kutokupatikana!
Wikienda linaamini katika nguvu ya media, linajua endapo wadau watajulishwa kuhusu kinachoendelea kwa msanii wao, wapo ambao wangeweza kumsaidia kama kweli amerejea katika matumizi, kama Babu Tale ameshindwa.
Meneja huyo wa Tip Top, hataki Chid Benz ahojiwe, hataki msanii huyo ajieleze kwa sababu hata ukimpata ‘mkorofi’ huyo kwenye simu yake ya mkononi, anakwambia Babu Tale amemkataza kuongea chochote na media.
Baadhi ya wasanii waliozungumza na Wikienda juu ya nyendo za Babu Tale, walisema jamaa anataka kumtumia Chid ili kujinufaisha. Kwamba, kwa kuwa msanii huyo kwa sasa hajiwezi, anatumia udhaifu wake ili amuongoze, atengeneze wimbo, amfanyie ‘kavareji’ katika media anazozijua yeye, arudi upya halafu yeye ‘apige’ hela.
“Jamaa anajifanya ameukamata huu muziki kwa sasa, anataka kila mtu amnyenyekee. Awafanyie haohao sisi wengine tupo katika muziki kabla yeye hajaja mjini, tunakomaa na kitaeleweka,” alisema msanii mmoja mkongwe wa Hip Hop akimzungumzia Tale huku akiomba jina lake lihifadhiwe.
Alhamisi iliyopita, Wikienda lilimsaka Chid kwa siku nzima lakini hakupatikana licha ya kufika kwenye saluni moja iliyopo Magomeni ambayo gazeti lilitonywa kuwa, huwa anapatikana hapo.
Baadhi ya watu kwenye eneo hilo la saluni, walisema Chid hupatikana hapo na Tale hivyo wa kutafutwa zaidi ni meneja huyo.
Wikienda lilimpigia Babu Tale ambaye alitoa mwongozo atafutwe kesho yake, Ijumaa mchana. Kesho hiyo ilipofika, alipigiwa simu lakini akaomba apigiwe baadaye.
Wikienda lilimpigia hiyo baadaye, akaomba muda tena akisema atakuwa amekutana na Chid. Baada ya muda alioomba, akapigiwa, sasa hakupokea simu na wala hakujibu meseji.
Cha ajabu, mmoja wa vyanzo vya Wikienda kwenye saluni hiyo alipiga simu na kusema, Chid na Babu Tale wapo kwenye saluni hiyo lakini wanajiandaa kutimka.
Mpaka Ijumaa inakatika, Tale hakuwa ametoa ushirikiano wowote kwa Wikienda. Hakusema kwamba hajaonana na Chid na wala hakusema kwamba hataki Chid azungumze na vyombo vya habari.
Chanzo:Global Publishers