Yanga itakuwa dimbani Jumanne ijayo kuwavaa TP Mazembe katika mechi ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho Afrika linaloandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), hofu kubwa ya timu hiyo ni sehemu ya ulinzi wa pembeni beki ya kulia na beki ya kushoto.
Beki kisiki wa kulia wa Yanga Juma Abdul.
Yanga pengine inaweza kuendelea kutaabika katika nafasi ya ulinzi wa pembeni hii ni baada ya wachezaji wawili wanaocheza nafasi hiyo, Haji Mwinyi na Oscar Joshua wote wakiwa katika hatari ya kuikosa mechi hiyo, hivyo Yanga ipo katika wakati mgumu wa nani acheze nafasi hiyo.
Mwinyi Haji Mngwali yeye ana kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mchezo uliopita wa michuano hiyo dhidi ya MO Bejaia ya Algeria wakati Joshua ana maumivu ya nyama za paja, ambayo pia aliyapata katika mchezo huo.
Lakini pamoja na hali hiyo habari njema kwa Yanga ni kwamba, Joshua tayari aliripotiwa kuanza mazoezi mepesi wakiwa huko kambini mjini Antalya, Uturuki ambako timu hiyo ambayo imerejea nchini hii leo kwa mafungu mafungu ilikuwa imejichimbia kujiandaa na mechi dhidi ya TP Mazembe.
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesema: “Joshua anaendelea vizuri na tayari alifanya mazoezi mepesi kwa ajili ya kujiandaa na mechi na Mazembe wakiwa huko Uturuki na wanategemea ataendelea hivyo kwa siku mbili akiwa hapa nchini ambako Jumamosi wamefanya mazoezi mepesi jioni ambayo yanaendelea kesho jumapili na jumatatu.
Aidha Hafidh akaongeza kusema kuwa “Bado hajajua hatma ya Joshua kama atacheza au hatocheza mechi na Mazembe, hivyo kila kitu kitajulikana ikiwa imebaki siku moja kabla ya mchezo wao baada ya daktari wa timu ya Yanga Edward Bavo kutoa ripoti yake”.
Joshua alipata majeraha hayo usiku wa Jumapili iliyopita dakika ya 32 katika mchezo dhidi ya MO Bejaia mjini Bejaia, Algeria ambapo ilibidi atolewe na nafasi yake kuchukuliwa na Mwinyi. Katika mchezo huo, Yanga ilifungwa goli 1-0.
Kwa upande wa nafasi ya beki ya kulia ambayo imekuwa ikushikiliwa kwa umahili na beki Juma Abdul ambaye alikuwa majeruhi japo kwa sasa ameanza mazoezi mepesi ufukweni lakini nafasi hiyo imekuwa haiwapi hofu sana Yanga kwakuwa mabeki wengi walionao wanaweza kumudu nafasi hiyo japo si kama ilivyo kwa Juma Abdul ambaye amekuwa mtengenezaji mkubwa wa mashambulizi kutokea pembeni huku akipiga krosi za hatari na zakusababisha mabao mengi ya Yanga katika michuano mbalimbali msimu huu.
Nafasi hiyo ya beki wa kulia kama Abdul asipopata nafuu basi inaweza kuzibwa na mabeki kama Mbuyu Twite, Pato Ngonyani na Kelvin Yondani lakini pia kisiki mwingine Hassan Ramadhan Kessy kutoka Simba kama atapata kibali basi anaweza akawa ndiyo mkombozi wa Yanga katika nafasi hiyo.
Kwa Yanga huo utakuwa mchezo wa pili wa Kundi A kwao, baada ya Jumapili kufungwa 1-0 na wenyeji Mouloudia Olympique Bejaia Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia Jumapili katika mchezo wa kwanza.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa watatu kutoka nchi tatu tofauti kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
Hao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.