Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kampuni ya Sportfive imetoa haki zote kwa Azam TV kuonyesha mechi zote za Yanga za Kombe la Shirikisho Afrika zitakazofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Azam wataonyesha mchezo wa kesho kati ya Yanga na TP Mazembe baada ya kupewa kibali cha kurekodi na kuonyesha mchezo huo na Sportfive au Lagardere Group ya Ufaransa.
Sportfive inayomiliki haki zote za matangazo ya televisheni ya mashindano mbali ya CAF mwaka jana ilisaini mkataba mwingine wa miaka 12 ijayo (2017-2028) kuendelea kutangaza na kumiliki haki za matangazo kwa mashindano makubwa ya Afrika, ikiwamo Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Lagardere Group baada ya kukubaliana na CAF imekuwa ikitoa nafasi kwa kampuni nyngine ya Afrika ikiwamo Azam kurekodi mechi hizo bila ya malipo yoyote, lakini wamekuwa wakiwapa nafasi ya kuonyesha mechi katika nchi husika pekee.
Azam inayolalamikiwa na Yanga kwa kuonyesha mchezo huo, watakuwa na bahati ya kutazamwa pande zote Afrika kupitia chaneli ya Sportfive.
Awali, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro alilalamikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuibariki Azam kurusha matangazo ya mchezo huo.
Lakini kwa mkataba huo, imeonekana wazi kuwa TFF hawana lolote la kufanya kutokana na CAF kusaini mkataba wa haki za runinga na Sportfive, hivyo Yanga sasa wanatakiwa kuwa wapole kwani suala hilo halipo Azam kwa sasa.
Hata hivyo, jana TFF imetoa tahadhari kwa viongozi na mashabiki wa Yanga wenye nia ya kufanya vurugu dhidi ya warusha matangazo ya televisheni moja kwa moja mechi ya Yanga dhidi ya TP Mazembe.
“TFF ikiwa msimamizi mkuu wa soka nchini inawajibika na mara moja inachukua nafasi hii kuwatahadharisha baadhi ya viongozi wa
Yanga, wanachama na mashabiki wao kutofanya vurugu kwani ni kinyume cha kanuni ya mashindano na mikabata ya udhamini katika hatua hii,” ilisema taarifa ya TFF.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa CAF inamiliki haki zote za habari na masoko ngazi ya makundi na jaribio lolote la kukwamisha matangazo ya biashara au utengenezaji na urushaji wa televisheni na shughuli nyingine za CAF au wakala aliyeteuliwa shirikisho hilo kutaigharimu klabu mwenyeji si kwa kutozwa faini tu, lakini hata kuondolewa katika mashindano.