Dewji alivyojipanga kufanikisha mikakati ya JPM kuingiza Tanzania uchumi wa kati

Miongoni mwa mambo yanayoifanya Tanzania kuwa masikini ni watu wengi kutokuwa na kipato cha uhakika na cha kutosheleza mahitaji muhimu kwa maisha.

Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa utafiti uliofanyika mwaka 2014 umebaini nguvu kazi ya Taifa ni watu milioni 22.3 kati ya idadi ya Watanzania wanaokadiriwa kufikia milioni 45.

Kati ya nguvu kazi hiyo ya watu milioni 22.3, wenye ajira ni 20 milioni na wasio na shughuli yoyote ya kuingiza kipato ni milioni 2.2.

NBS inasema kuwa kwa kadri uchumi wa Tanzania unavyokua ndivyo na idadi ya watu wasio na ajira inavyopungua.

Takwimu nyingine zinaonyesha kuwa kila mwaka vijana 850,000 wanamaliza masomo na kuingia katika soko la ajira na miongoni mwao asilimia tano ndio wanaofanikiwa kupata ajira kwenye sekta rasmi. Wengi wao hubakia wakizurura mijini kutafuta ajira miaka kadhaa na miongoni mwao pia hujiunga katika sekta isiyo rasmi, wakijihusisha na shughuli za ujasiriamali.

Rais John Magufuli amekuwa akihimiza shughuli za kiuchumi ili kuisukuma Tanzania katika uchumi wa kati, ambao Watanzania wengi watakuwa na ajira na vipato vizuri.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuhimiza uwekezaji, kufufua viwanda na kuhamasisha ukuaji wa viwanda vya ndani kwa kudhibiti uingiaji wa bidhaa kutoka nje.

Rais Magufuli anaona wazi kuwa sekta ya uzalishaji nchini inasuasua. Lengo lake ni kuona sekta ya uzalishaji viwandani inachangia zaidi ya asilimia 15 ya pato la Taifa na kuongeza asilimia 40 ya ajira nchini. Katika mkutano na wafanyabiashara wakubwa nchini, Dk Magufuli aliwahakikishia kuwa Serikali yake itakuwa bega kwa bega nao katika kuhakikisha uchumi wa nchi unakua.

Katika kuhakikisha kuwa Watanzania wanafaidika na kukua kwa uchumi, amekuwa akiisafisha Serikali yake juu ya vitendo vya rushwa, ufisadi na uzembe katika uwajibikaji.

Wakati wafanyabiashara wakihimizwa kushirikiana bega kwa bega na mikakati ya Serikali ya kuinua uchumi na kupambana na umaskini, Mfanyabiashara Mtanzania, bilionea mdogo Zaidi Afrika, Mohammed Dewji ameahidi neema kwa Watanzania.

Mtandao wa Forbes; unaoandika taarifa za watu bilionea duniani, unamnukuu Dewji akisema kuwa anatarajia kuzalisha ajira 100,000 kabla ya kufikia 2020.

Katika mpango huo wa ajira, anasema nafasi nyingi zitachukuliwa na Watanzania. Mpaka sasa Dewji kupitia kampuni zake ameajiri Watanzania 28,000.

Mfanyabiashara huyo ambaye amefanikiwa kutunukiwa zawadi mbalimbali kutokana na umahiri wake kibiashara, akifanikisha mpango huo atatoa ajira 100,000.

“Ninatarajia kuwekeza Dola 500 milioni (sawa na Sh1.1 trilioni) katika kipindi cha miaka minne ijayo. Mkakati huo utawezesha ajira zaidi ya 500,000 katika bara la Afrika katika kipindi kinachoishia 2021 na wengi wao watakuwa ni Watanzania,” Dewji ananukuliwa na mtandao huo.

Dewji ambaye sasa ana umri wa miaka 41, ni mmoja wa wafanyabiashara wanaomiliki kampuni binafsi zinazokuwa kwa kasi nchini na eneo la Afrika Mashariki na Kati.

Mfanyabiashara huyu chini ya kampuni zake zilizo chini ya MeTL anamiliki viwanda 35 vinavyojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali katika sekta ya kilimo, nishati, mafuta, huduma za fedha, simu za mikononi, miundombinu, mashamba makubwa, usafirishaji na usambazaji.

Mpaka sasa Kampuni za MeTL zinatoa ajira inayofikia asilimia mbili katika sekta binafsi, hali inayomfanya Dewji kushika nafasi ya pili ya chombo kilichoajiri Watanzania wengi baada ya Serikali.

Ili kuhakikisha MeTL inatoa nafasi nyingi za ajira nchini, Dewji anasema tayari amechukua hatua mbalimbali za kufanikisha mpango huo.

Miongoni mwa mipango hiyo anaitaja kuwa ni kupanua na kuongeza wigo wa miradi kwenye kampuni zake kama vile kuongeza mitaji, kupanua maeneo ya kazi, kuchochea ufanisi na thamani.

Mwaka jana, Mtandao wa Forbes ulimtangaza Dewji kuwa mfanyabiashara wa mwaka kutokana na umahiri wake kibiashara ambao uliomfanya kuwa bilionea mdogo kuliko wote Afrika.

Umahiri wake pia kwenye biashara barani Afrika ulimfanya apate pia tuzo mwaka 2012 na kumfanya ang’ae zaidi mbele ya mabilionea wakongwe Afrika.

Miongoni mwa mabilionea wakongwe Afrika ni James Mwangi ambaye ni Mkurugenzi wa Benki ya Equity Kenya, Akinwumi Adesina (Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika) na Aliko Dangote (mfanyabiashara tajiri zaidi Afrika anayejishughulisha na uzalishaji wa saruji).
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad