JESHI la Polisi Laendelea Kuikaba Chadema, Mahafali Mengine ya CHADEMA Yatawanywa

Jeshi la Polisi mkoa Kilimanjaro jana liliwatawanya wahitimu wa vyuo vikuu kupitia umoja wa Chadema (Chaso), waliokuwa wamekusanyika mjini Moshi kwa ajili ya mahafali yao.

Dalili za ‘kibano’ hicho zilianza kuonekana asubuhi wakati polisi na askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) wakiwa wamejihami kwa mabomu ya machozi, walipozingira hoteli ya Keys inayomilikiwa na Philemon Ndesamburo.

Hoteli hiyo iliyopo maeneo ya Kwa Alfonsi nje kidogo ya mji wa Moshi, ndipo ambako mahafali hayo ambayo yalikuwa yahusishe wahitimu 70 kutoka vyuo vikuu vinne yalikuwa yafanyike.

Wanafunzi hao ni kutoka Chuo Kikuu cha Mwenge (Mwekau), Chuo cha Kikuu cha Ushirika Moshi (Mocu), Chuo Kikuu cha Masoka na Chuo Kikuu cha Tiba KCMC (KCMU Co).

Hata hivyo, polisi wakiwa na magari yaliyokuwa yakipeperusha bendera nyekundu, walivamia hoteli hiyo na kuwataka wahitimu hao kutawanyika kwa amani, kwa vile mikusanyiko ya aina hiyo imezuiwa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chadema (Bavicha) mkoani Kilimanjaro, Dickson Kibona alilaani tukio hilo akisema hakukuwa na sababu yoyote ya kuzuia mahafali hayo.

“Wamezuia bila sababu yoyote na hii inakiuka misingi ya kidemokrasia, Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa,” adai Kibona.

Kibona alidai kama isingekuwa kuhofia maslahi ya kibiashara ya Hoteli ya Keys ambapo kulikuwapo pia watalii, wangegoma kuondoka kwa kuwa hawakuvunja sheria yoyote ya nchi.

Mmiliki wa hoteli hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo, alisema ndiye aliyewashauri vijana hao kutawanyika kwa amani na kuwataka wasibishane na polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alisema polisi walipata taarifa kuwa wahitimu hao wangekuwa na mkutano wa kisiasa ambao ulijificha kwa mwavuli wa mahafali.

“Tumewaita viongozi wao na kuwaeleza kuwa mikutano yote ya kisiasa imezuiwa na watawanyike. Walituelewa na wakatawanyika, lakini sisi bado tunaendelea kuimarisha doria mitaani,” alisema.

Hili ni tukio la pili kwa wanachama wa Chaso kutawanywa na Polisi ambapo juzi katika hoteli ya African Dream mjini Dodoma, wahitimu wa vyuo vikuu mjini Dodoma nao walitawanywa na FFU.

Mkuu wa Idara ya Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema Chadema inaendelea kuhifadhi kumbukumbu za matukio yote yanayoendelea nchini, ili kujenga ushahidi utakaojitosheleza pindi itakapoonekana ni mwafaka kuchukua hatua zaidi.

Alifafanua kuwa chama hicho kinatambua hila zinazofanywa na Serikali kwa kulitumia Jeshi la Polisi, na kuwa wanatambua amri zinazotolewa na watendaji wa chama tawala kupitia wakuu wa mikoa na wilaya.

Alisema wanao ushahidi wa matukio yote utakaotumika muda wowote, watakapoamua kuishtaki Serikali ndani au nje ya nchi.

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mkoani Moshi Chadema wana ajenda ya kuweka kumbukumbu wanavyo dai.. Je mnnaelewe kuwa uchaguzi ulisha malizika na chama tawala na serikali yake imeshika hatamu za uongozi na wana Watumikia Wananchi??

    Kwa Taarifa yenu.. Activity zenu za Siasa zingoje wakati wa kampeni huko 2020
    any activity during this period.. kwanya mjue itakuwa ni kinyume na malengo na nia ya kuleta Maendeleo tuliyo yaweka sisi .. Na hatima yake ni kwamba hatuto kubali kuona mnataka kuleta myumbisho wa ukweli na mwelekeo ... Tunakwambieni wakati wa kampeni ukikaribiwa kuanza mtapewa Taarifa ili mfanye kampeni na siyo sasa.... Chaso / Maso / Mbaso / Mbweso / wato wa Cdm kokote ..Hapa Kazi Tu

    ReplyDelete
  2. Uchaguzi na Kampeni zake ni sawa na Uchafu.. Tunapenda Kuwattarifu kuwa Muda Huo umesha sitishwa baada ya Nchi kupata Serikali... Hivi sasa Ni wakati wa serikali Kufanya Yake... Vurugu sisizo ambatana na mwelekeo wa Ujenzi wa Taifa ni Lazima zisitishwe na Kuwachwa Mara Moja.. Na nyote muhakikishe kuwa Ada zenu za Biashara na leseni zenu zimelipiwa ipasavyo kutusaidia ukusanyaji wa mapato ya ndani.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad