SERIKALI imewasilisha Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 ya Sh trilioni 29.53, ambayo nguvu kubwa imewekwa katika kukusanya mapato kwa kulinda viwanda vya ndani na kubana matumizi ya serikali ili kuelekeza sehemu kubwa ya matumizi katika maeneo ya vipaumbele.
Katika bajeti hiyo, bidhaa za lazima zinazogusa maisha ya wananchi ikiwemo mafuta ya petroli na dizeli pamoja na ushuru wa barabara na maji ya kunywa, havijaguswa huku bidhaa za starehe kama bia, sigara, soda, juisi na nyingine kama nguo za mitumba, huduma za kupanga nyumba na uhamishaji fedha kwa simu, vikipandishwa kodi, huku kiinua mgongo cha wabunge, kufutiwa msamaha wa kodi.
Aidha, makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi, ikiwemo mapato ya taasisi za udhibiti kama Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Mafuta (EWURA), Shirika la Viwango (TBS), Jeshi la Polisi (Trafiki) na mamlaka nyingine za udhibiti, sasa yatapelekwa moja kwa moja katika Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo mahitaji yao ya fedha yatatolewa na Wizara ya Fedha na Mipango, badala ya kujigawia kutokana na bakaa ya mapato waliyokusanya.
Aidha, maduka ya kutoa huduma katika majeshi, yamefutiwa kodi rasmi na badala yake, Serikali inajipanga kuongeza posho kwa askari, ili iwasaidie kukidhi mahitaji yao, huku taasisi za umma na ofisi zote za Serikali, zikipigwa marufuku kufanya biashara na mzabuni asiyetumia mashine za kodi za kielektroniki (EFD’s).
Kodi juu
Katika bidhaa zilizoongezewa ushuru na kodi ni pamoja na vinywaji baridi, kutoka Sh 55 kwa lita mpaka Sh 58, huku ushuru wa forodha katika maji ya matunda (juisi) yanayotumia matunda yanayozalishwa hapa nchini, ukipanda kidogo kutoka Sh 10 mpaka 11 kwa lita. Juisi zinazotokana na matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini, ushuru wake pia umepanda kutoka Sh 200 kwa lita hadi Sh 210 kwa lita.
Bia, vilevi, mvinyo
Kwa upande wa bia, serikali imependekeza bia inayotokana na nafaka ya hapa nchini, ambayo haijaoteshwa kama kibuku, ushuru upande kutoka Sh 409 kwa lita mpaka 430.
Bia zingine, ushuru wake pia umepanda ambao sasa utatoka Sh 694 mpaka 729 kwa lita, huku bia zisizo na kilevi, ikiwa ni pamoja na vinywaji vya kuongeza nguvu, ushuru ukipanda kutoka Sh 508 kwa lita mpaka Sh 534.
Kwa upande wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu zilizolimwa nchini kwa kiwango cha asilimia 75, ushuru wake umepanda kutoka Sh 192 kwa lita mpaka Sh 202.
Ushuru wa mvinyo unaotengenezwa na zabibu zilizolimwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 kutoka Sh 2,130 kwa lita mpaka Sh 2,237. Vinywaji vikali, havikuachwa nyuma maana ushuru umepanda kutoka Sh 3,157 mpaka Sh 3,315.
Sigara
Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kwa tumbaku ya hapa nchini kwa kiwango angalau asilimia 75 kutoka Sh 11,289 hadi Sh 11, 854 kwa kila sigara 1,000.
Kwa upande wa sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kwa tumbaku ya nchini kwa angalau asilimia 75, ushuru juu kutoka Sh 26,689 hadi Sh 28, 024 kwa kila sigara 1,000.
Sigara zenye sifa tofauti na hizo, ambazo hazina vigezo hivyo vya tumbaku ya ndani, ushuru wake umepanda kutoka Sh 48,285 hadi Sh 50,700 kwa kila sigara 1,000.
Katika tumbaku ambayo iko tayari kutengenezwa kuwa sigara, ushuru wake umeongezeka kutoka Sh 24,388 hadi Sh 25,608 kwa kilo huku ushuru wa sigara aina ya Sigar ukibaki kuwa asilimia 30.
Vilainishi, gesi asilia, simu juu
Katika mafuta ya kulainisha mitambo, ushuru umepanda kutoka Sh 665.50 kwa lita hadi Sh 699 kwa lita, huku ushuru wa grisi za kulainisha mitambo, ukipanda kutoka senti 75 kwa kilo, hadi senti 79 kwa kilo.
Gesi asilia pia ushuru umepanda kutoka senti 43 kwa futi za ujazo mpaka senti 45 kwa futi za ujazo.
Kuhusu viwango vya ushuru wa kuhamisha fedha kwa kutumia simu, serikali imependekeza kutoza ushuru wa asilimia 10, kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma wa simu, katika kutuma na kupokea fedha, badala ya ushuru huo kutozwa tu katika kutoa fedha.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, kwa utaratibu wa sasa, baadhi ya kampuni zinazotoa huduma zimetumia mwanya wa kuhamisha sehemu kubwa ya ada hizo kwenye kupokea fedha na hivyo kuwa nje ya wigo wa kodi.
Ulaji wa wabunge, hisa
Kwa upande wa kiinua mgongo cha wabunge wakati wa kustaafu, sasa kitatozwa kodi kila mwisho wa muhula wa miaka mitano ili kujenga misingi ya usawa na haki katika utozaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa.
Aidha, mapato yote yatokanayo na hisa katika kampuni mbalimbali sasa yatatozwa kodi, baada ya kufutwa kwa msamaha kwa waliokuwa wakimiliki hisa chini ya asilimia 25.
Kodi ya mishahara
Katika kodi inayokatwa katika mishahara (P.A.Y.E), imepunguzwa kutoka asilimia 11 mpaka tisa kwa wafanyakazi wanaopata mshahara wa kuanzia Sh 170,000 lakini hauzidi 360,000. Kwa wanaopata zaidi ya 360,000 lakini haizidi 540,000, watakatwa Sh 17,100 pamoja na asilimia 20 ya kiasi kinachozidi Sh 360,000.
Kabla ya hapo walikuwa wakikatwa Sh 20,900 na asilimia 20 ya kiasi kinachozidi Sh 360,000.
Wanaopata zaidi ya Sh 540,000 lakini haizidi Sh 720,000, watakatwa Sh 53,100 pamoja na asilimia 25 ya kiasi kinachozidi 540,000.
Kabla ya hapo, walikuwa wakikatwa Sh 56,900 na hiyo asilimia 25 ya kiasi kilichozidi 540,000. Kwa wanaopata zaidi ya Sh 720,000 wao watakatwa Sh 98,100 pamoja na asilimia 30 ya kiasi kinachozidi Sh 720,000.
Kabla ya hapo, walikuwa wakikatwa Sh 101,900 pamoja na asilimia 30 ya kiasi kilichozidi Sh 720,000.
Kodi za nyumba
Serikali pia imependekeza malipo ya kupanga nyumba, nayo yatozwe kodi ambayo haikuweka kiwango, ila imependekeza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato, apewe mamlaka ya kukadiria kiwango cha chini na cha juu cha mapato yapatikanayo na pango ili yatozwe kodi.
Kodi za nyumba, usajili magari, pikipiki
Mbali na mapato ya kodi za nyumba, Serikali imependekeza kupandisha ushuru wa kusajili magari na pikipiki kutoka Sh 150,000 hadi Sh 250,000 kwa kila gari na kutoka Sh 45,000 hadi Sh 95,000 kwa kila pikipiki.
Kwa watumiaji wa namba binafsi za magari, ada sasa itapanda kutoka Sh milioni 5 kila baada ya miaka mitatu mpaka Sh milioni 10.
Kodi ya majengo
Aidha, kodi za majengo sasa hazitakusanywa na halmashauri, badala yake TRA ndiyo inayopewa mamlaka hayo ya kukadiria, kukusanya, kuhifadhi na kuiwakilisha katika halmashauri husika.
Mbali na TRA kupewa mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo, serikali pia imependekeza kupunguza misamaha ya kodi za majengo ili majengo mengi zaidi yaingizwe katika orodha ya kulipa kodi.
Ulindaji wa Viwanda
Saruji aina ya (HS Code 2523.29.00) zinazotoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ushuru wake wa forodha umepandishwa kutoka asilimia 25 mpaka asilimia 35 ili kulinda saruji inayozalishwa nchini dhidi ya ushindani wa bei ya saruji kutoka nje ya nchi.
Kwa bidhaa za chuma ikiwemo mabati kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, nazo ushuru umetoka asilimia 0 mpaka 10, ili kulinda uzalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini, huku bidhaa za nondo kutoka nje nazo zikipandishwa kodi kutoka asilimia 10 mpaka 25, kwa nia ya kulinda viwanda vya ndani.
Nyavu za kuvua samaki kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ushuru wake umepanda kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 huku vichujia vya vilainishi na petroli kutoka nje ya nchi vikiongezwa ushuru kufikia asilimia 25 kutoka asilimia 10, ili kulinda bidhaa za ndani.
Sukari, ngano, mitumba, mafuta ya kula
Katika sukari, serikali imekusudia kupunguza msamaha wa kodi na hivyo waagizaji wa bidhaa za sukari kutoka nje watalazimika kuanza kulipa ushuru wa asilimia 15 kutoka asilimia 10, huku ikitarajiwa kuongezeka zaidi na kuwa asilimia 20 mwaka 2017/18 na asilimia 25 mwaka 2018.19, ili kulinda viwanda vya ndani.
Kwa upande wa ngano kutoka nje, ushuru umepunguzwa kutoka asilimia 35 mpaka 10, kwa kuwa nchi za Afrika Mashariki hazina uwezo wa kuzalisha kulingana na mahitaji.
Kwa upande wa nguo na viatu vya mitumba Serikali imepandisha ushuru kutoka dola za Marekani 0.2 mpaka dola za Marekani 0.4 kwa kilo, kwa nia ya kudhibiti nguo hizo lakini pia imetangaza kujiandaa kuzuia uingizaji wake.
Kwa upande wa mafuta ya kula kutoka nje nayo ushuru umepanda kutoka asilimia 0 mpaka 10 kwa mafuta ghafi ya kula, ili kuimarisha kilimo cha mbegu za mafuta na viwanda vya ndani.
Tozo za pamba, kahawa, korosho
Miongoni mwa tozo zilizofutwa kuondoa kero kwa wananchi ni mchango kwa kila kiwanda cha kuchambua pamba wa Sh 450,000 na ada ya vikao vya halmashauri wakati wa kujadili wafanyabiashara wa pamba ya Sh 250,000.
Kwa upande wa kahawa, Serikali imefuta ada ya leseni ya kusindika kahawa ya dola za Marekani 250, huku ushuru wa kusafirisha korosho wa Sh 50 kwa kilo, ukifutwa.
Tozo zingine zilizofutwa katika korosho ni ushuru wa chama kikuu cha ushirika Sh 20 kwa kilo, gharama za mtunza ghala Sh 10 kwa kilo, kikosi kazi cha kufuatilia masuala mbalimbali Sh 10 na makato ya unyaufu.
Pia Serikali imepanga kuendelea kufuta tozo nyingine zinazokatwa na halmashauri, wakala na mashirika katika mazao ya wakulima, baada ya kufanya tathmini za kina.
Maduka kambi za jeshi
Serikali imependekeza kufuta msamaha wa kodi uliokuwa ukitolewa katika maduka na migahawa maalumu kwa ajili ya askari wa majeshi, kutokana na msamaha huo kutumiwa vibaya na kupoteza mapato ya serikali na badala yake, askari watapata posho mpya juu ya posho ambazo wamekuwa wakipewa.