Msajili: Rais Magufuli Hajazuia Kufanya Siasa

MSAJILI wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi ametetea kauli ya Rais John Magufuli kuhusu kufanya siasa wakati huu na kwamba alichotaka kiongozi huyo wa nchi ni ushirikiano kutoka kwa wanasiasa wenzake ili kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema Rais Magufuli, katika kauli yake ile hakumaanisha kuzuia shughuli za siasa nchini isipokuwa alieleza kuwa hatakuwa tayari kuona siasa zinakwamisha mikakati ya kuwapelekea wananchi maendeleo yao.

Jaji Mutungi alisema hayo Dar es Salaam jana, alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kauli ya Rais Magufuli ya kuwataka watu kuacha siasa za hovyo hadi mwaka 2020 utakapofanyika uchaguzi mkuu mwingine, ili muda uliopo wautumie kuijenga nchi.

“Watu wametafsiri tofauti kauli ya Rais, lakini ni kwamba alikuwa akiomba ushirikiano wa wanasiasa wenzake na wadau wote wa siasa kuleta maendeleo… kwa hiyo kabla ya kukosoa kauli ni vyema ukafanya utafiti siyo kuibeba na kuitafsiri kwa mrengo tofauti,” alisema .

Alisema siyo kwamba Rais anapinga siasa isipokuwa anapingana na wanasiasa ambao ni pingamizi katika kuleta maendeleo na muda wote wamejikita katika siasa bila kuangalia namna ya kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.

Alisema wapo watu walioitafsiri tofauti hotuba aliyoitoa juzi Rais Magufuli, hivyo wananchi wanapaswa kuwa watafiti na kuweka maslahi ya nchi huku akiwataka wanasiasa kuwa wavumilivu na kutumia muda wao kutafakari jambo kabla ya kuzungumza.

“Rais alikuwa akijaribu kuwasihi wanasiasa kuangalia namna ya kujikita kwenye siasa ya maendeleo ya jamii kwa ujumla na kuachana na siasa za kupinga maendeleo,” alisema.

Alisema dhamira ya Rais ni kuwaletea maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla na vyama vinapaswa kufuata utaratibu wa kuwasilisha taarifa kwa msajili na si kusubiri hadi vyombo vya habari kutoa taarifa.

Mutungi alisema vyama vya siasa vimekuwa vikitaka demokrasia nchini, hivyo kabla ya vyama kufikiria demokrasia kitaifa, hivyo viongozi wake waanze kuangalia suala hilo kwenye vyama vyao na si kuimba, kwani wapo wanaofanya ndivyo sivyo.

Alisema mtu anapotetea jambo, kwanza anapaswa kulitekeleza kwa vitendo huku akibainisha demokrasia kutotokea nchini endapo demokrasia ndani ya vyama vya siasa kuwa ni shida.

Jaji huyo alisema bado kuna kazi kubwa huku akibainisha yapo mambo mengi yanayotokea nchini huku akitegemea ushirikiano wao na kuwataka wanasiasa kuwekeza katika kufanya upembuzi wa mambo kabla ya kutamka au kuyatenda.

Naye Msajili Msaidizi, Kitengo cha gharama za Uchaguzi na Elimu kwa Umma, Piencia Kiure alisema ni vyama vitatu tu kati ya 22 ndivyo vimewasilisha taarifa ya gharama za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.

Mwisho wa kuwasilisha gharama hizo ni leo. Alivitaja vyama vilivyowasilisha gharama za uchaguzi kuwa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF).

Alifafanua kuwa, mgombea atakayeshindwa kuwasilisha gharama za uchaguzi utahukumiwa kifungo kisichozidi mwaka mmoja au faini isiyozidi Sh milioni mbili au vyote kwa pamoja.

Aidha, chama kitakachoshindwa kuwasilisha gharama za uchaguzi katika kipindi kilichowekwa adhabu yake ni faini isiyozidi Sh milioni tatu na kutoruhusiwa kushiriki uchaguzi hadi watakapofanya marejesho.
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Msajili wa vyama amekua msemaji/mtetezi wa kauli za rais?

    ReplyDelete
  2. Wanasiasa wengi wa upinzani wanapenda na wanakusudia kupotosha mambo, ili mradi waonekane na wasikike kwenye media. Hakuna cha maana wanachokifanya zaidi ya kujaribu kuikosoa CCM na viongozi wake

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad