Mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Chanel Ten mkoani hapa, Daudi Mwangosi, Pacificus Simoni ametoa ushahidi wake mbele ya mahakama na kuieleza kuwa alilazimishwa kusaini ungamo mbele ya mlinzi wa amani bila kujua nini kilichoandikwa.
Alidai kuwa baada ya kutoka kuhojiwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) na Ofisa wa Makosa ya Jinai ya Mkoa (RCO), akifananishwa na picha ya gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012 alipokana siyo yeye, alipelekwa kwenda kufanya ungamo kwa mlinzi wa amani, Frola Mhelela ambaye alikuwa shahidi namba tatu.
Alidai wakati anakwenda kwa mlinzi wa amani alisindikizwa na Staff Sajent Erick, ambaye alikuwa ameshika bahasha na kumkabidhi kwa mlinzi huyo.
Mtuhumiwa huyo alidai mlinzi huyo alitoa karatasi na kuisoma kisha baadaye alimuambia aisaini, naye bila kuhoji alisaini ile karatasi kwa sababu ilitoka kwa kiongozi wake ambaye ni RCO, Nyegesa Wankyo.
Katika kesi hiyo wakili wa utetezi, Rwezaura Kaijage aliiomba Mahakama kwamba mawakili wa upande wa Jamhuri wataleta majumuisho ya mwisho leo.
Hata hivyo, upande wa jamhuri ambao uliongozwa na wakili Sunday Hyera, ulisema hawana pingamizi lolote juu ya upande wa utetezi baada ya kukaa na kukubalina kwa pande zote mbili saa nane mchana watawasilisha majumuisho hayo.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Dk Paulo Kihwelo alisema Mahakama imekubali ombi la wakili wa utetezi kuleta majumuisho, huku Juni 27 wakisikiliza maoni ya wazee wa baraza kwa ajili ya kupanga hukumu.