Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam wameanza kudhibiti vitendo vya mauaji kwa kupitia wapangaji na wenye nyumba kulazimika kuingia mikataba itakayoambatana na picha ya mpangaji.
Wamewataka wenye nyumba wanapotengeneza mikataba waweke picha za wapangaji wao na nakala zipelekwe kwenye ofisi za Serikali za mitaa kwa ajili ya usalama.
Hatua hiyo imekuja baada ya jeshi hilo kubaini kuwa kila linapokwenda kuwakamata watuhumiwa wanakoishi linakosa taarifa kamili kutoka kwa wenye nyumba wao.
Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema jana kuwa utafiti unaonyesha wanapowafuatilia watuhumiwa, wengi wao huwa wamechukua chumba kimoja ambacho hukaa miezi miwili hadi mitatu na baadaye wanahamia kwenye nyumba nyingine.