Polisi jana walipiga kambi kwa saa saba kwenye geti la nyumba ya Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, wakitaka kumkamata bila ya mafanikio.
Polisi hao walikuwa kama wageni wa askofu huyo wakisubiri wafunguliwe geti, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:10 jioni walipoamua kuondoka wakitumia gari aina ya Toyota Landcruser lenye namba za kiraia, ambalo kwa muda wote huo lilikuwa limeegeshwa pembeni mwa geti hilo.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha takriban miezi 16, kwa askari wa jeshi hilo kwenda nyumbani kwa askofu huyo na kushinda mbele ya nyumba yake kwa saa kadhaa, kabla ya kuondoka bila ya kumtia nguvuni.
Tukio hilo pia linatokea wakati kukiwa kumesambaa mkanda unaotoa sauti ya Askofu Gwajima, ikizungumzia kitendo chake cha kuamua kumuunga mkono Rais John Magufuli na kumshutumu Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ikiitaka afikishwe mahakamani kwa yote yaliyofanyika wakati wa utawala wake ambayo Rais wa sasa anayashughulikia.
Jana, mbele na nyuma ya gari hilo kulikuwa na askari waliokuwa wamevalia kiraia, kila mmoja akionekana kama anafanya shughuli tofauti, lakini wote wakionekana kuwa na lengo moja; kusubiri kufunguliwa lango la nyumba ya Askofu Gwajima.
Mbele ya nyumba walikuwapo askari watatu na raia wawili, mmoja mwanamke na mwingine mwanamume ambao baadaye ilibainika kuwa walikuwa wamezuiwa na askari hao baada ya kuonekana wakitokea mlango wa nyuma wa nyumba hiyo.
Mwandishi alishuhudia mwanamke huyo akiitwa na askari aliyekuwa ndani ya gari na kuonywa kuepuka kutumika, kisha akarudishiwa simu yake ambayo walikuwa wakiishikilia.
Raia hao walisema, walifika kwenye nyumba hiyo kwa ajili ya kufanya tathmini ya matengenezo na baada ya kumaliza walipokuwa wanatoka wakakutana na askari hao na kukamatwa.
Askari hao wasikika wakisemezana kuwa kuna taarifa zinasambazwa kwenye simu kuwa nyumba ya kiongozi huyo wa kiroho, ambaye aliibuka kuwa maarufu mwishoni mwa mchakato wa Katiba Mpya, imezingirwa, wakati hakukuwa na kitu kama hicho.
Pia, askari hao walisikika wakieleza kushangazwa na kitendo cha wenyeji kutowafungulia geti hilo ili waingine.
“Mtu kama huna tatizo; ni raia mwema. Una sababu gani ya kukataa kufungua mlango? Afungue akutane na sisi wageni wake,” alisema mmoja wa askari hao wakati wakiongea baina yao.
“Tumekuja bila silaha, tunataka kuzungumza naye, hataki kufungua mlango, anataka nini sasa?” alihoji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alipoulizwa alisema hajatuma askari yeyote nyumbani kwa Gwajima.
“Wapigie makamanda wengine kwa sababu si kila anayeishi Kinondoni amefanya kosa Kinondoni,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema wanamuhitaji askofu huyo.
“Kama uko na Gwajima mwambie tunamuhitaji.” Alipoulizwa wanamuhitaji kwa sababu gani, Kamanda Sirro alisema: “Tumepata clip (mkanda) inayosemekama ni ya kwake. Tunamtaka athibitishe kama hayo maneno ni ya kwake. Na kama ni yeye ameyasema, anaelewa nini kuhusu kile alichokizungumza kwa sababu hayo maneno ni ya kichochezi. Tupo kwenye uchunguzi .”
Askofu Gwajima si mgeni wa matukio kama hayo dhidi ya mamlaka.
Mwaka 2012 aliingia kwenye mzozo na Jeshi la Polisi baada ya kijana mmoja kudai amejisalimisha kanisani kwake kutubu, baada ya kushiriki kwenye tukio la kumteka kiongozi wa madaktari, Dk Steven Ulimboka.
Hata hivyo, Askofu Gwajima aliekeza kuwa kijana huyo hakuwahi kufika kwenye kanisa hilo, wala kukutana naye na kwamba taarifa hizo zililenga kuchafua kanisa lake.
Mwaka 2015, Askofu Gwajima aliingia kwenye mgogoro mwingine na Jeshi la Polisi baada ya mkanda wa sauti ya mahubiri kanisani kwake kutoa maneno yaliyoonekana kukashifu msimamo wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo dhidi ya tamko la maaskofu wa Jukwaa la Wakristo la kuwataka waumini wao wasipige kura ya maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Katika sakata hilo, Askofu Gwajima alifunguliwa shtaka la kutoa lugha ya matusi dhidi ya Kardinali Pengo, na kushindwa kuhifadhi silaha na risasi wakati akiwa hospitalini.
Kabla ya kufunguliwa mashtaka hayo, askari walizingira nyumba yake kwa takriban saa saba, lakini hawakufanikiwa na siku iliyofuata kiongozi huyo alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam.
Akiwa huko aliugua na baadaye kulazwa. Polisi walitangaza kukamata watu 15 wakiwatuhumu kuwa walikuwa na mpango wa kumtorosha na kukamata silaha hiyo pamoja na risasi walizodai walizikuta kwenye gari.
Polisi Wamuwinda Askofu Gwajima Kwa Masaa 7 Bila Mafanikio, Ni Baada ya Kusambaa kwa Video Akimsema Vibaya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete
2
June 17, 2016
Tags
Gwajima.. Upo? nakama upo tafadhali tutembelee haraka iwezekanavyo. Ili tupate maelezo yako.
ReplyDeletewenye kuleta fujo wote wakamatwe watiwe ndani tena na adhabu kali hivo kweli hawa wana akili nchi ina amani wanataka kuvuruga amani serekali isiwachie kabisa we need peace wote maaskof driver muuza sokoni yeyeyote yule
ReplyDeleterumande ndio maskani yao