Serikali imejikuta katika wakati mgumu wakati wa upitishaji wa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2016, baada ya wabunge kupinga baadhi ya hatua zilizochukuliwa katika muswada huo.
Jana, Bunge lilitumia zaidi ya saa mbili kupitisha muswada huo huku mvutano ukiibuka katika nyongeza ya mapendekezo ya ununuzi wa dawa na vifaatiba kufanywa kwa dharura na kupinga kwa kamati za fedha na mipango, kuondolewa katika kusimamia mchakato wa zabuni kwenye halmashauri.
Mashambulizi hayo yaliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia na wabunge Joseph Kakunda (Sikonge), Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini) na Andrew Chenge wa Bariadi Magharibi (), kiasi cha kumfanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju kukubali baadhi ya mapendekezo ya Bunge kwa shingo upande.