Ackson Tulia wa Bunge Ametenda Uovu

DK. Tulia Akson, naibu spika wa Bunge, amefanikiwa kuvuna aibu. Ni kule kukubali kwake kusimamia uamuzi wa kufukuza wabunge saba wa upinzani katika Bunge la Jamhuri, anaandika Saed Kubenea.

Miongoni mwa waliofukuzwa, ni Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki na mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni; Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini, na Godbless Lema, mbunge wa Arusha Mjini.

Wengine ni Esther Bulaya, mbunge wa Bunda Mjini; Pauline Gekul, mbunge wa Babati Mjini, na John Heche, mbunge wa Tarime Vijijini.

Baadhi yao walishitakiwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Wengine wamesomewa mashitaka na kuhukumiwa bila hata kusikilizwa.
Wengine walishitakiwa na wakaweza kujitetea, lakini wakiwa wamezuiwa kuwakilishwa na mawakili, kama ambavyo kanuni za Bunge zinaelekeza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ni George Mkuchika, kada mashuhuri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tayari uamuzi huu uliosimamiwa na Dk. Tulia umeanza kupingwa ndani na nje ya Bunge.
Hata hivyo, naibu spika hakutoa nafasi ya kusikiliza hoja tofauti. Miongoni mwa hoja hizo ni zifuatazo:

Kwanza, kazi ya kamati ya haki, kinga na madaraka ya Bunge, ni kuchunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala yote ya haki, kinga na madaraka ya Bunge.

Kazi hizi zimetajwa kwenye kanuni ya 4(1) (a) na (b) ya nyongeza ya nane ya kanuni za kudumu za Bunge, toleo la Januari 2016.

Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, katika suala hili, haikutimiza majukumu yake kama ilivyoelekezwa na Bunge.

Imetenda kazi zake kwa njia ya kibaguzi. Haikufungulia mashitaka wabunge wa CCM wanaotuhumiwa kufanya vurugu bungeni siku hiyo.

Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za bunge, kwa kutumia picha za video zilizowasilishwa mbele ya kamati, baadhi ya wabunge wa CCM, wanaonekana wakifanya vurugu, ikiwamo kuongea bila utaratibu na bila ruhusa ya kiti cha spika.

Wengine wametumia lugha isiyoruhusiwa ndani ya Bunge.
Vile vile, baadhi ya wajumbe walipohoji sababu za watuhumiwa kutofikishwa mbele ya kamati, mwenyekiti hakutaka kusikiliza.
Hata ripoti iliyosomwa bungeni haikueleza hoja za wajumbe wengine wa kamati kushinikiza wabunge wote wanaoonekana kwenye kumbukumbu hizo wafikishwe mbele ya kamati ya Bunge.
Hivyo, kamati ilipokea maelekezo ya spika ya kuchunguza mwenendo wa wabunge, kinyume cha Katiba, kanuni za Bunge na sheria za nchi.

Pili, wajumbe walio wachache walipinga pendekezo la kamati la kutoa onyo la jumla kwa wabunge wote wa upinzani; kwamba ikitokea mbunge yeyote wa upinzani ametenda kosa jingine, atachukuliwa hilo ni kosa lake la pili.

Huku ni kukiuka haki na utoaji wa haki. Yawezakane adhabu kugusa wabunge wote wa upinzani, wakati wengine hawakushitakiwa, hawakutuhumiwa na wala hawakupata fusra ya kujitetea?
Kamati inawezaje kutumia maneno, “baadhi ya wabunge,” lakini papo hapo ikahukumu wabunge wote wa upinzani?

Wala spika hakuelekeze uchunguzi wa ziada dhidi ya wabunge wengine walioonekana kwenye video iliyowasilishwa mbele ya kamati. Ameishia kung’ang’ana na wabunge wa upande mmoja tu – upinzani.

Tatu, wabunge saba wa upinzani wamehukumiwa kinyume cha kanuni ya 74(3)(a) za kanuni za Bunge.

Sehemu ya sita kwenye ukurasa wa 53 kanuni ya 74 inaeleza aina ya kosa. Ikiwa mbunge aliyeshitakiwa ametenda kosa la kwanza, mbunge huyo atazuiwa kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi 10.

Aidha, kanuni inasema, “ikiwa hilo ni kosa lake la pili au zaidi, mbunge huyo atazuiwa kuhudhuria vikao visivyozidi 20.”

Baadhi ya wabunge wamehukumiwa kutohudhuria mikutano miwili ya Bunge – mkutano wa Bunge la bajeti unaondelea sasa na mkutano ujao wa Bunge.

Wala ndani ya kanuni, hakuna utaratibu wa kutuhumu makosa ya jumla. Kuna utaratibu wa kuwapo maelezo ya kina kwa kila kosa na kwa kila anayetuhumiwa na wakati kosa limetendeka. Kamati ilituhumu kwa jumla na bila kuzingatia matakwa ya kanuni.

Nne, naibu spika hakuzingatia mapendekezo ya wajumbe wachache walioshauri kuwa kabla ya uamuzi kufikiwa na Bunge, ni muhimu watuhumiwa wakapewa fursa ya kujitetea mbele ya wabunge wenzao.

Ni kama ilivyofanyika kwenye Bunge la Tisa, ambapo Zitto alipewa fursa ya kujitetea mbele ya Bunge zima kabla ya azimio juu ya adhabu yake kufikiwa.

Ni wakati wa sakata la mkataba wa Buzwagwi, ambako Zitto alituhumiwa kusema uongo bungeni. Baadaye ikafahamika kuwa kilichoitwa “uongo” na watawala, kilikuwa kweli tupu.
Naibu spika hakusikiza hoja zote hizo. Hakusikiliza, si kwa sababu alikuwa na hoja. Hapana. Ni hulka yale ile ile ya ubabe na kutaka kufurahisha waliompa cheo. Basi!

Kwa mfano, kanuni ya 5 (1) ya kanuni za kudumu za Bunge inaelekeza spika, katika kutekeleza majukumu yake, kuzingatia uamuzi wa maspika waliotangulia.

Katika Bunge la Tisa, aliyekuwa spika wake, Samwel Sitta, aliruhusu wajumbe wawili wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Christopher Ole Sendeka na Anne Kilango Malecela, kuwasilisha maoni yao mbadala bungeni.

Ni pale kamati ilipokuwa ikijadili shauri lililofunguliwa na Dk. Reginald Mengi dhidi ya aliyekuwa mbunge wa Mkuranga, Adam Malima.

Kilango na Sendeka waliruhusiwa kusoma maoni yao mbele ya Bunge zima.
Naye Sitta baada ya kusoma maoni ya Kilango na Sendeka alifikia hitimisho, kwa kukubaliana na maoni ya wajumbe wawili dhidi ya kundi la wajumbe waliowengi.
Sitta alifikia uamuzi huo kutokana na mazingira ambayo yalitawala kuanzia usikilizaji wa kesi, utoaji ushahidi hadi uandishi wa hukumu.

Mengi alilalamika kuwa Kamati iliyokuwa chini ya Juma Nhunga na makamu wake, Willison Masilingi, isingemtendea haki.

Alisema kwamba kulikuwa na mazingira ya mhimili wa utawala (executive) kuingilia mhimili wa Bunge (legislature), jambo ambalo ni kinyume cha utawala bora na mgawanyo wa madaraka.
Alidai kuwa aliyekuwa waziri mkuu wakati huo, Edward Lowassa, alimshauri ajitoe katika kesi hiyo, kwa kuwa wabunge wamehongwa na mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini.
Philimon Ndesamburo, aliyekuwa mmoja wa wajumbe wa kamati, alijiuzulu katikati ya shauri kwa kile alichoita, “kamati kuhongwa.”

Ili kuondoa utata, Sitta alimwandikia barua Ndesamburo ili kufafanua tuhuma alizoporomoshea wabunge na Bunge.

Katika barua yake kwa Sitta, tarehe 24 Januari 2007, Ndesamburo aliendelea kusisitiza kuwapo kwa rushwa na shinikizo kutoka kwa watawala serikalini.

Sitta alieleza katika uamuzi wake aliosoma bungeni tarehe 8 Februari 2007, kwamba amezingatia matokeo ya uchunguzi na ushauri wa kamati; ushauri wa wajumbe wawili waliotoa mawazo tofauti – Sendeka na Kilango – na uchambuzi na ufafanuzi wa kilichoelezwa na Ndesamburo.
Sitta hakutaka kukubaliana na maoni ya walio wengi. Alikataa. Aliridhika kuwa uamuzi huo ulitolewa kwa jazba na ulilenga kuwapo kwa nia mbaya.

Alisema kwamba maneno ya Malima dhidi ya Mengi bungeni yalimuathiri mfanyabiashara huyo na yalikuwa na athari kubwa ya kumgonganisha na viongozi wakuu wa nchi.

Katika saka hili la sasa, ukweli ulio dhahiri ni kwamba naibu spika aliamua kwa nia mbaya. Hakutaka kutafsiri vema kanuni za bunge.Hakutaka kuona maslahi ya wengi katika hoja za wabunge.
Naibu spika ameshindwa kuunganisha hekima na kanuni. Matokeo yake, ameibuka na uamuzi ambao badala ya kuunganisha bunge umelipasua katikati.

Source:Mwanahalisionline
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Saed Kubenea na Mwanahalisi, Udaku tumefurahii kutuletea huu mwono wa Kubenea..Baada ya Kuisoma picha na mawazo ya Mwandishi ni kutuletea Hisia ambayo amejaribu kuangalia yaliyotokea huku nyuma na kujaribu kutuletea hoja kuwa kuna baadhi ya mwendo ambao ungepaswa kuangaliwa zaidi. Ameshindwa kujitambua na kutambua kuwa hatima iko wazi na inajulikana na hata sisi Watanzania tumeshachoka nao hawa Waheshimiwa Uchwara yeye akiwa mmoja wapo.. Amejaribu kuvisha lawama ambazo hazima mshiko ile aweze kuleta chembe cchembe za kutufanya tuweze kutafakari.. Yeye na wapotoshaji wenzake wanazitumia hizi mbinu ambazo napenda kutaarifu kwamba kwa hii Tanzania yetu Mpya zimeshapitwa na Wakati.. Huko awali tuliweza kubabaishwa na watu wa aina zenu lakini katika Awamu yetu hii ya Tano na Tanzania yetu hii na Serikali yetu hii yenye Azma kubwa ya kuleta Maendeleo kwa nchi na wananchi wake Wazaleondo.. Tunakwambiaeni karibuni kama mna Nia ya kushiriki kikamilifu kuiletea nchi maendeleo ila kama ni wavivu kwa kuleta mivutano.. Tungeoba muendelee Mapumzikoni Muwawache Wachapa Kazi Wafanye Kazi huku mkiwa ni washangiliaji huko BENCHI... Nadhani mnajielewa na Mnanielewa.. Hapa Kazi Tu.

    ReplyDelete
  2. Hivyo hivi vichwa vya Habari Mnavipata wapi??

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad