Maalim Seif kutinga Mahakama ya ICC leo Kuwashitaki Viongozi wa Serikali

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema katibu wake mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad leo atakwenda katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) kuwashtaki viongozi wa Serikali kwa madai walitumia mamlaka yao vibaya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kisha kuwatesa, kuwakamata na kuwapiga wafuasi wa chama hicho bila makosa.

Chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar, kimesema taratibu zote za kufungua mashtaka hayo zimeshakamilika, ikiwa ni pamoja na kuweka wakili.

Mei 22 mwaka huu, chama hicho kilizindua ripoti yake ya uvunjwaji wa haki za binadamu Zanzibar wakati wa uchaguzi huo na kutangaza azma yake ya kwenda ICC kuwashtaki Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema mpango huo umekamilika na Maalim Seif ambaye yuko nje ya nchi kwa ziara ya kueleza alichodai ‘figisufigisu’ zilizotokea katika uchaguzi mkuu, ataweka wazi kila kitu kilichotokea na jinsi ukiukwaji wa demokrasia ulivyoshika kasi nchini.

Mazrui alimtuhumu IGP Mangu kuwa anatumiwa na CCM kuwakamata viongozi wa CUF ili wasitimize azma yao ya kueleza ukweli wa yaliyotokea katika uchaguzi, huku akimtaka afute azma yake ya kumkamata Maalim Seif kwa maelezo kuwa “ataitumbukiza Zanzibar kwenye machafuko”.

Siku tano zilizopita, IGP Mangu wakati akihojiwa na Azam TV alisema Jeshi la Polisi wakati wowote litamburuza mahakamani Maalim Seif kwa kuhamasisha uchochezi Zanzibar. Iwapo CUF itatekeleza azima hiyo, itakuwa tukio la kwanza kwa Tanzania kupeleka viongozi wake kwenye mahakama hiyo.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na naibu wake, William Ruto wameshafikishwa huko, lakini kesi dhidi yao zilikosa nguvu na kuondolewa.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Salim Jecha Salim alifuta matokeo ya rais, wawakilishi na madiwani Oktoba 28, mwaka jana siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa mbio za urais.

CUF ilidai kuwa ilishinda uchaguzi huo na Jecha alipotangaza uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu, chama hicho kilijitoa na hivyo CCM kushinda viti vyote.

Mazrui ambaye aliambatana na viongozi wengine wa chama hicho alisema: “Mpango wa kuishawishi dunia kuwachukulia hatua wahusika wote wa ukiukwaji wa haki za binadamu na uvunjwaji wa demokrasia uko palepale, hautasitishwa kwa vitisho vyovyote.

 “Lengo ni kuhakikisha unyama dhidi ya raia wasio na hatia unakomeshwa na uzingatiwaji wa sheria za nchi unatamalaki. Tunawaambia polisi kuwa tumechoshwa na figisufigisu maana zitazaa timbwiri.”

Mazrui alisema wanaotaka kuzuia mpango wa CUF kueleza ukweli na kwenda ICC, wanaandaa utaratibu wa kumkamata Maalim Seif aliyedai; “Ni kipenzi cha Wazanzibari”, akisisitiza kuwa jambo hilo ni hatari kwa sababu litaivuruga Zanzibar.

Akifafanua zaidi kile alichokiita mikakati ya CCM kupitia kwa IGP Mangu kuficha ukweli, Mazrui alidai kuwa polisi wamekuwa wakiwakamata wanachama wa CUF mara kwa mara.

"Niongeavyo hapa wanachama zaidi ya 400 wa CUF wamekamatwa na wengine wapo nje wa dhamana,” alisema.

Alisema ni jambo la ajabu kuona IGP Mangu akishindwa kutoa kauli yoyote baada ya Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DDCI), Salum Msangi kuwatishia mawakili kuwatetea wananchi wanaokamatwa kwa tuhuma  mbalimbali.

Alisema viongozi wa CUF hawatatishwa wala kunyamazishwa katika kudai haki ya ushindi wa Wazanzibari kutokana na uamuzi wao wa uchaguzi mkuu.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Shaweji Mketto alisema endapo IGP Mangu ataendelea kuwatisha viongozi wa CUF, watajipanga kwenda kumtembelea ofisini kwake.

IGP Mangu ajibu
Alipoulizwa kuhusu kauli za CUF, IGP Mangu alisema tayari ameshatoa msimamo wa Jeshi la Polisi na walichokifanya viongozi wa chama hicho ni kumjibu tu.

“Ukipendwa sana ukafanya uhalifu tukuache? Tukikutuhumu unafanya makosa tutakukamata hatuwezi kuogopa umaarufu wako,” alisema huku akisisitiza kuwa jalada kuhusu Maalim Seif lipo kwa DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka).

“Umesema hao CUF wamesema kuna wanachama wao wamekamatwa, sasa wamekueleza hao wanachama ni kina nani?… kama wamekamatiwa Zanzibar wapo maofisa wa polisi wa mikoa wanaoweza kuzungumzia hilo huko Zanzibar.”

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema: “CCM hatuwezi kujiingiza katika hoja za IGP na CUF tumewaachia wenyewe. Kwa sasa tupo katika maandalizi ya kuhakikisha Rais (John) Magufuli anashinda kwa kishindo kuwa mwenyekiti wa CCM.” Alisema chama hicho hakina sababu ya kutumia Jeshi la Polisi kukandamiza wanachama na viongozi wa CUF.

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Polisi wa Tanzania
    Jifunzeni toka polisi wa USA
    Kwanini mna kuwa wana siasa
    Katiba mpya only solution

    ReplyDelete
  2. wewe ulio andika hayo maneno ni msenge au nini

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad