Mapya yaibuka: Aliyemweka Mtanzania rehani kwa Bil 1.5 atajwa


Baada ya gazeti la Mtanzania hivi karibuni kuibua taarifa ya kijana Adamu Akida anayeshikiliwa na kundi la maharamia nchini Pakistani, kutokana na kudaiwa kuwekwa rehani ughaibuni na kaka yake aitwaye Juma Neti, mkazi wa Kunduchi jijini Dar es Salaam, mapya yaibuka.

Kijana huyo ambaye ni mkazi wa Magomeni Mtaa wa Chemchem na Idirsa, inasemekana aliwekwa rehani kwa ghamara ya Dola za Marekani 700, 000, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.5 za Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ndugu wa karibu wa Mtanzania huyo zinasema kuwa, Adamu aliwekwa rehani na kaka yake aitwaye Juma Neti akitakiwa kulipa fedha za unga (mihadarati) aliochukua.

“Aliyesababisha yote hayo ni Adamu kwa sababu ndiye aliyekwenda naye Pakistani kwa kisingizio kwamba fedha zinapatikana kwa urahisi huko,” alisema ndugu huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Wakati hayo yakiendelea, jana usiku askari polisi walivamia nyumba ya Juma Neti kwa ajili ya kumkamata kwa tuhuma za kuuza dawa za kulevya.

Nyumba hiyo ambayo ipo Kunduchi, maeneo ya Ununio, Manispaa ya Kinondoni, ilivamiwa na askari hao baada ya gazeti hili kuanza kuripoti uwepo wa Mtanzania nchini Pakistani anayeshikiliwa na kundi hilo la maharamia.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, alipopigiwa simu kuzungumzia tukio hilo hakupokea na hata alipoandikiwa ujumbe mfupi wa maneno, hakuujibu.

Pamoja na Neti kutaka kukamatwa jana, taarifa zinasema polisi wamekuwa wakimtafuta kwa muda mrefu kutokana na tabia yake ya kujihusisha na biashara hiyo bila mafanikio.

Taarifa zaidi zinasema kwamba, Neti amekuwa na utajiri wa kutisha kwa kuwa miaka michache iliyopita, alikuwa na maisha ya kaiwada ingawa sasa anaonekana kuwa miongoni mwa Watanzania wenye ukwasi mkubwa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, hivi karibuni Neti aliingia ubia na kampuni moja ya Kenya baada ya kuwekeza Dola za Marekani 400,000, sawa na zaidi ya Sh milioni 800 za Tanzania.

Mmoja wa watu wa karibu na Mtanzania huyo anayeshikiliwa ambaye hakutaka kutaja jina lake, aliiambia MTANZANIA, kuwa Adamu ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya Akida na alikuwa anaishi Magomeni Dar es Salaam, Mtaa wa Sunna.

Mtoa taarifa huyo, alisema kwamba alipondooka nchini miezi minane iliyopita, aliacha mke na kwamba baba yake kwa sasa anaishi Mlingotini Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Mtoa taarifa huyo anazidi kueleza kuwa, Adamu ni kinyozi maarufu eneo la Magomeni, Mtaa wa Idrisa na pia ni mtunzi na msomaji mzuri wa kaswida aliyekulia katika Madrasat Damba iliyopo Mtaa wa Chemchem.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad