Marekani imeitaka Uturuki kujizuia baada ya jaribio la mapinduzi lililozimwa siku ya Ijumaa ambapo maelfu ya maafisa wa kijeshi wamekamatwa.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni nchini Marekani John Kerry ameutaka utawala nchini Uturuki kuheshimu sheria wakati wa uchunguzi wao kuhusu mapinduzi hayo.
Kerry amesema kuwa madai kwamba Marekani ilihusika katika mapinduzi hayo inasababisha madhara kwa uhusiano kati ya washirika hao wawili wa NATO.
Mapema kupitia kwa hotuba yake, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitoa wito kwa rais Obama kumrejesha nchini humo kiongozi wa kidini raia wa Uturukli anayeishi nchini humo Fethullah Gulen ambaye analaumiwa kwa kupanga mapinduzi hayo.
Marekani inasema kuwa Uturuki ni lazima ithibitishwa hayo kabla ya uamuzi wa kumrejesha Gulen kufanyika.
Mapema nchini Uturuki maelfu ya watu walijitokeza wakiimba na kupeperusha bendera ya taifa katika barabara za mji wa Istanbul na Ankara kumuunga mkono rais Erdogan.
Bustani nyingi mjini Istanbul zilijaa watu waliokuwa wakiimba wakisema kuwa ardhi yao na demokrasia haviwezi kuchukuliwa na jeshi.
Serikali imetawaka wafuasi wake kusalia katika bustani kuu usiku kucha. Mashirika kadha ya ndege yalirejea safari zao kwenda Istanbul Jumamosi jioni.