Maswali Tisa Kuenguliwa kwa DC Dakika za lala Salama Ikulu

Uteuzi wa kimakosa wa Emile Yotham Ntakamulenga kuwa mkuu wa wilaya (DC) uliofanywa na Ikulu na kutenguliwa dakika za mwisho katika hafla ya kuapishwa, umeibua maswali mengi kuliko majibu.

Juzi, Rais John Magufuli alikutana na wateule wake 142 wakiwamo wakuu wa mkoa watatu na 139 wa wilaya na mpaka anakamilisha kuwaapisha wakuu wa mikoa; si yeye wala wasaidizi wake waliyejua kosa lililofanyika.

Takribani saa 72 baada ya kutangazwa kwa orodha ya wateule hao Juni 26, hakuna aliyekuwa anajua kuwa Ntakamulenga hakuwa miongoni mwa wanaohitajika. Wajumbe wote wa kamati ya uteuzi hawakujishughulisha kuhakiki orodha hiyo.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kiprotokali wamehoji juu ya umakini wa aliyekuwa akiandika kila jina lililopitishwa na kama alitekeleza wajibu wake na kujiridhisha kuwa idadi ya wateule ililingana na wilaya zilizopo.

Wanahoji, hivi aliyeandaa mialiko hakushtuka? Je, aliyewapigia simu wahusika? Je, wote wawili, Ntakamulenga aliyekosewa na Nurdin Babu aliyestahili walialikwa?

Maswali mengine ni kama DC aliyestahili amekumbukwa na kualikwa, kwa nini asiyestahili hakujulishwa mapema asifike?

Huenda aliyekosea ni aliyekuwa anaorodhesha baada ya kamati husika kujiridhisha na sifa, historia na uchapakazi na kila mteule au aliyetoa mialiko, hasa kama alijifungia peke yake.

Endapo kosa lilianzia kwenye kuorodhesha, uwezekano wa kuwaalika wateule wote wawili usingekuwapo, badala yake kosa lingerekebishwa mapema na jina la Mkuu wa Wilaya ya Serengeti lingekuwa moja, kama ilivyotokea Ikungi na Rombo.

Kama Ntakamulenga aliruhusiwa kuingia katika lango la Ikulu, akakaguliwa na wahusika kujiridhisha kuwa ni mmoja kati ya wageni waalikwa, wadadisi wanasema kosa limetoka juu ya ngazi hiyo.

Mpaka mshehereshaji alipowataka wote waliohudhuria hafla hiyo waketi kwenye viti vyao, hakuna aliyeshtuka. Ntakamulenga alishuhudia wakuu wa mikoa wakiapishwa. Akapiga picha ya pamoja ambayo itaendelea kuwapo kwenye kumbukumbu za matukio ya Rais Magufuli.

Kati ya waliojiuliza maswali hayo ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba aliyesema: “Ntakamulenga anastahili kufidiwa ili kumpunguzia machungu ya kudhalilishwa,” na kuongeza: “Haiwezikani mtu amevaa na suti yake halafu anafanyiwa vile. Hakuomba kufika pale.”

Vilevile, alikosoa njia iliyotumika kumuondoa ukumbini akisema haikuwa ya kistaarabu. “Ni udhalilishaji. Serikali haikuwa makini.”

Alionyesha shaka yake juu ya umakini wa wasaidizi wa Rais Magufuli hasa kwa muda uliotumika kupitia sifa kabla ya kuwapata wateule hao.

Tofauti na Dk Bisimba, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Milline Mbonile alisema kwenye barua za watumishi wengi wa Serikali kuna kipengele cha kutekeleza majukumu watakayopangiwa na wakuu wao wa kazi.

Kwa kipengele hiki; “Hakuna kosa lolote, kilichofanywa ni afadhali kuliko kama angeapishwa.”

Alifafanua kuwa kuna uwezekano kwamba mtu alipenyeza jina hilo kinyume na kanuni zilizopo.

Mhadhiri mwandamizi wa chuo kikuu hicho, Dk Benson Bana alisema tukio hilo ni funzo la kuhakiki taarifa kabla ya kuzitangaza: “Watendaji wawe makini ili Serikali isitoe taarifa zenye makosa.”
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Sasa wewe ni muhubiri,kilicho tokea ni mambo ya siasa sio dini. Kitu cha muhimu katika maisha ya binadamu ni afya njema,mambo mengine yatatokea baadae.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad