Mnyika Ajibu Kuhusu Taarifa za Kumkataa Lowassa, Kuhama Chadema

Baada ya kuenea kwa uvumi kuwa Naibu Katiba Mkuu wa Chadema, John Mnyika anataka kuachana na chama hicho, kiongozi huyo ameibuka na kukanusha akisema: “Hakuna kitu kama hicho na wala sina mpango wa kuhama.”

Mnyika alisema hayo jana alipopigiwa simu ili azungumzie taarifa hizo. Mbunge huyo wa Kibamba alisisitiza kwamba huo ni uzushi.

Habari za kujiuzulu kwa Mnyika zilianza kusambaa katika vyombo vya habari kwa mara ya kwanza mwaka 2013 baada ya aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kufukuzwa uanachama.

Wakati huo, uvumi ulienea kwenye mitando kwamba amejivua nyadhifa zake zote na kwamba ameshakabidhi barua yake kwa katibu mkuu wakati huo, Dk Willibrod Slaa.

Habari hizo zilijirudia mara baada ya Dk Slaa kutangaza kujivua nyadhifa zake zote ndani ya chama hicho huku akipinga hatua yake ya kumtangaza Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa nafasi ya urais.

Licha ya kushindwa kujitokeza hadharani kukanusha wala kuthibitisha tetesi hizo, Mnyika alionekana kuendelea na shughuli zake za kisiasa kama kawaida.

Uvumi wa tatu uliibuka mwishoni mwa wiki iliyopita safari hii ilidaiwa kueleza msimamo wake kuhusu Lowassa kupitishwa na Chadema na kisha Ukawa kuwania urais ikidaiwa kwamba anataka kiongozi huyo ahojiwe na kuchukuliwa hatua kutokana na ushiriki wake katika kashfa ya Richmond.

Habari hiyo iliyoibua hisia za wengi ilimnukuu Mnyika akisema: “Msimamo wangu haujabadilika kama ambavyo niliwahi kusema nikiwa mkurugenzi wa vijana wa Chadema tarehe 25 Februari 2008 na kipindi chote nikiwa Mbunge wa Ubungo…. Hivyo nategemea kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi Lowassa ndiye atakuwa wa kwanza. Siwezi kusaliti msimamo wangu bora nipoteze ubunge wangu.”

Katika mwendelezo wake, baadaye uvumi mwingine uliibuka kwamba baadhi ya viongozi wa chama hicho walionekana nyumbani kwa Mnyika wakimsihi asichukue uamuzi huo.

Hata hivyo, hakuna kiongozi yeyote wa Chadema aliyewahi kuzungumzia suala hilo kabla ya hivi karibuni, Ofisa Habari Mwandamizi wa Chadema, Tumaini Makene kutoa taarifa ya kukanusha akisema huo ni mradi wa kutengeneza uongo unaofadhiliwa na watu kwa ajili ya kukisumbua chama na Watanzania akisema wakati habari hizo zinaenezwa, Mnyika alikuwa akifanya shughuli za chama.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad