Mtoto Happiness John Mkazi wa Seliani Arusha aliyefanyiwa upasuaji kwenye moyo na kupandikiziwa kifaa cha kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo (pacemaker), ameanza mazoezi.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto, Sulender Kuboja aliyeshiriki upasuaji huyo alisema jana kuwa hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri na wameanza kumfanyia mazoezi mepesi.
Dk Kuboja alisema kwa kawaida mgonjwa yeyote aliyefanyiwa upasuaji anapaswa kufanyiwa mazoezi mepesi na kwamba kwa mtoto, mazoezi anayofanyiwa ni ya kukaa, kusimama na kutembea kidogo.
“Hali yake inaonekana kuendelea vizuri sana... nimetoka kumfanyia vipimo muda mfupi uliopita kifaa kile kinafanya kazi vizuri na maendeleo yake yanaridhisha sana,” alisema Dk Kuboja.
Alisema mtoto huyo anaweza kuongea na hata kula chaku- la, hali aliyosema inaonyesha nafuu nzuri kwake.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Elitruda Malley alisema anaridhishwa na maendeleo ya afya ya mwanaye kwa kuwa tangu afanyiwe upasuaji huo juzi, hali yake imeonekana kuimarika kwa haraka.
Mama huyo alisema tangu awekewe kifaa hicho, mwanaye amekuwa mchangamfu, hali aliyosema inamtia moyo na kumpa matumaini makubwa.
“Ingawa yupo kwenye oxygen, lakini namshukuru Mungu kwani anaonekana anapata nafuu nzuri, anatabasamu na kuongea vizuri kabisa na ana furaha sana, shauku yake ni apone ili aende shule kama watoto wengine,” alisema Malley.
Aliongeza kuwa mtoto huyo amekuwa akila vizuri na kumpa moyo kwani mwili wake unaonekana kuwa na nguvu na afya nzuri.
“Madaktari wapo karibu wakifuatilia afya ya mtoto kwa ukaribu, wanampa chakula, wanamfanyia mazoezi ya kukaa na kushuka chini, anaonekana kuwa na nguvu na mwenye maendeleo mazuri. "
Alisema jambo linalompa faraja ni kuona jinsi madaktari wote wanaomuhudumia mtoto huyo wanavyofanya kazi hiyo kwa upendo na bidii.
Juzi, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ilifanikiwa kumpandikiza mtoto huyo mwenye umri wa miaka mitano kifaa cha kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo (pacemaker) kinachoendeshwa kwa betri.
Hayo ni mafanikio ya pili kwa taasisi hiyo ya kisasa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati baada ya Mei 24 na 25, mwaka huu kufanikisha operesheni kwa wagonjwa 18 bila kuusimamisha moyo.
Ina tia moyo sana. Wahusika wawajali na kuwapa madaktari STAHIKI ZAO ili basi waweze kufanya kazi zao kwa moyo. BILA KUSAHAU KUWA MADAKTARI HAO NI MAZAO YA WALIMU, HIVYO WALIMU NAO TUWAPENDE, WAANGALIWE KWA JICHO LA PILI.
ReplyDelete