Rais Magufuli Awaweka Majaribuni Wakuu wa Wilaya 20

Baada ya Rais John Magufuli kufanya uteuzi wa wakuu wa wilaya 139, homa sasa imehamia kwa wakuu wa wilaya 20 ambazo zinakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kukabiliwa na migogoro mingi ikiwamo matatizo ya maji, njaa na mapigano ya wakulima na wafugaji.

Changamoto inayowafanya wakuu hao kukalia kuti kavu iwapo watashindwa kupambana kikamilifu na changamoto hizo inatokana na vigezo vilivyowekwa na Rais Magufuli ambavyo alivitumia wakati wa kuwateua ambavyo ni migogoro ya ardhi, tatizo la elimu hasa upungufu wa madawati, njaa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Wakuu wapya ambao wanakabiliwa na mtihani huo ni pamoja na Mohamed Utali (Mvomero), Adam Mgoyi (Kilosa), Luteni Kanali Michael Mtenjele (Ngara), Rashid Taka (Ngorongoro), John Palingo (Kongwa), Tumaini Magessa (Kiteto), Josephat Maganga (Bukombe), Thobias Mwilapwa (Tanga), Glodius Luoga (Tarime), Asia Abdallah (Kilolo) na Godwin Gondwe (Handeni).

Wangine ni Mrisho Gambo (Arusha), William Paul (Mbeya), Vumilia Nyamoga (Chamwino), Alexander Mnyeti (Arumeru), Sauda Mtondoo (Kilindi), Mary Onesmo (Nyamagana), Idd Kimanta (Monduli), Juma Njwayo (Rufiji) na Aaron Mmbago (Mwanga).

Migogoro ya ardhi

Wakuu wa wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro wanakabiliwa na mtihani mkubwa wa kutatua migogoro isiyokwisha ya ardhi ambayo ilisababisha Dk Rajab Rutengwe avuliwe ukuu wa mkoa, baada ya mapigano kutokea mara mbili tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani Novemba mwaka jana na kusababisha vifo vya watu na idadi kubwa ya mifugo.

Mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Mvomero ambao umedumu kwa muda mrefu uliwalazimu, Mwigulu Nchemba wakati huo akiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene kwenda kujaribu kuutatua lakini suluhisho la kudumu halijapatikana.

Wilayani Kilosa, watu wanne walifariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa na kulazwa katika Kituo cha Afya cha Mtakatifu Joseph, Kata ya Dumila katika mapigano baina ya wakulima na wafugaji.

Migogoro ya ardhi pia iko wilayani Nyamagana ambako Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliunda kamati ya ushauri kuhusu kuhusika kwa maofisa ardhi kwenye migogoro hiyo. Chanzo cha migogoro hiyo kinaelezwa kuwa ni baadhi ya maofisa wa ardhi na tayari Waziri Lukuvi ameshachukua hatua mara mbili ya kuwasimamisha kazi watumishi wa idara hiyo wilayani hapo baada ya kupelekewa malalamiko na wananchi.

Mkoani Tanga, aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Mwantumu Mahiza wakati akimkabidhi ofisi mbadala wake, Martin Shigela alisema kuna migogoro sugu ya ardhi kwenye jiji la Tanga na wilaya za Kilindi na Handeni na kwamba kamati iliyoundwa kushughulikia tatizo hilo imeshamaliza kazi na dawa imeshapatikana.

Hata hivyo, pamoja na maelezo hayo, migogoro ya ardhi ni tatizo kubwa mkoani Tanga na kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara ya kutokuwa na imani na kamati ilivyofanya kazi hiyo ya kutafuta dawa ya migogoro isiyokwisha baina ya wafugaji na wakulima, pia ugomvi wa mipaka ya vijiji mikoa ya Tanga na Manyara.

Wilaya nyingine zenye migogoro ya aina hiyo ya muda mrefu ni Ngara, Ngorongoro, Bukombe, Kiteto na Kongwa. Katika Wilaya ya Ngorongoro kuna migogoro ya ardhi yenye sura tofautitofauti. Kuna mgogoro wa ardhi kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro wanataka waruhusiwe kulima kilimo cha kujikimu; kuna mgogoro kati ya wananchi, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) na kampuni za wawekezaji wa utalii na wahamiaji haramu. Tarafa ya Loliondo – hasa vijiji vya Ololosokwan, Oloipir, Soit Sambu na Enguserosambu; kuna mgogoro kati ya wananchi na wahamiaji haramu kutoka Kenya, Tarafa ya Sale hasa vijiji vya Kisangiro, Oldonyosambu, Tinaga, Yasimdito, Digodigo, Sale, Pinyinyi, Mageri, Magaiduru nako kuna migogoro ya ardhi baina ya kijiji na kijiji.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Taka alisema atahakikisha anakaa pamoja na pande zote zinazokinzana kwenye migogoro ya ardhi ili kutatua tatizo hilo.

Huko Ngara, mkuu wa wilaya hiyo, Luteni Kanali Mtenjele atakuwa na changamoto ya mgogoro ulioanza mwaka 2008 wilaya hiyo ilipoanza kuvamiwa na wafugaji maarufu kama Wahima waliotoka Wilaya ya jirani ya Karagwe baada ya kufukuzwa na Serikali. Baadhi ya wafugaji hao walitoka nchi ya jirani ya Rwanda. Mwaka 2009 mifugo ilizidi kuongezeka na maeneo ya malisho kuwa finyu na kusababisha wafugaji kuanza kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima na kusababisha mgogoro mkubwa.

Tatizo kama hilo limekuwa sugu katika Wilaya ya Bukombe. Kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu na hivi karibuni agizo lililotolewa na Nchemba kabla ya kuhamishwa kutoka Wizara ya Kilimo kwenda Mambo ya Ndani, kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bukombe kushirikiana na wafugaji kuwaondoa wafugaji wanaodaiwa kuvamia na kulisha mifugo yao katika Pori la Akiba la Kigosi Muyowosi, huenda lisifanikiwe.

Hiyo ni kutokana na wafugaji hao kutangaza kutokuwa na imani na mwenyekiti wa kamati hiyo, aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo, Amani Mwenegoha. Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Kanda ya Ziwa (Chawakazi), Juvenary Mulashani alisema wafugaji hao hawako tayari kufanya kazi na Mwenegoha kwa madai kuwa hawatendei haki.

Mkoani Dodoma ukiacha Wilaya ya Chamwino ambayo imekuwa ikikabiliwa na njaa, Kongwa kumekuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji ambao pia umekuwa ukihusisha Wilaya ya Kiteto iliyopo mkoani Manyara na kusababisha mgongano kwa wanasiasa.

Mgogoro wa wakulima na wafugaji katika wilaya hizo mbili umekuwa wa muda mrefu na uliingia kwenye Bunge la Kumi hasa baada ya kusababisha mauaji upande wa Kiteto lakini yakihusisha wakazi wa Kongwa kiasi cha kusababisha mbunge wao, Job Ndugai, ambaye sasa ni Spika wa Bunge, kulalamika bungeni dhidi ya uongozi wa Wilaya ya Kiteto. Katika Mkoa wa Arusha, kuna migogoro ya ardhi kwenye wilaya za Monduli na Arumeru na jitihada za kuitatua hazijafanikiwa kuikomesha kabisa. Monduli kulikuwa na migogoro ya ardhi ya mashamba kutokana na maofisa ardhi kugawa ovyo viwanja. Wilayani Arumeru, hasa eneo la Meru, kuna migogoro ya ardhi baina ya wamiliki wakubwa na vijiji.

Wilayani Rufiji kuna mgogoro ambao ulianza mara baada ya wafugaji waliokuwa katika Bonde la Ihefu mkoani Mbeya kuhamishwa na Rufiji ikafanywa kuwa moja ya maeneo ya kufikia wafugaji hao.

Mei, 2012 kulizuka vurugu katika Kata ya Ikwiriri zilizosababisha watu kujeruhiwa na mali kuharibiwa, ikiwa ni pamoja na kuvunjwa kwa nyumba za wafugaji baada ya mkulima mmoja wa Kijiji cha Muyuyu kudaiwa kuuawa na wafugaji.

Uhaba wa chakula

Kwa upande wa njaa, wakuu wa Wilaya za Kilolo hasa Isimani mkoani Iringa, Chamwino (Dodoma) na Rorya (Mara) pamoja na Kilindi mkoani wa Tanga watalazimika kufanya kazi ya ziada kukabiliana na changamoto hiyo ambayo imekuwa ikisumbua katika maeneo hayo mara kwa mara.

Changamoto za kisiasa

Kwa wilaya za Arusha na Mbeya, wakuu wa wilaya hizo watakumbana na mihemko ya kisiasa kutokana na kuwa na wafuasi wengi na wakereketwa wa vyama vya upinzani.

Gambo ambaye amekuwa kada wa CCM, atakumbana na joto la kisiasa kutoka kwa wana Chadema wakiongozwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kama ilivyokuwa kwa Magessa Mulongo wakati huo akiwa mkuu wa mkoa huo.

Hata hivyo, huenda Gambo ameshasoma alama za nyakati kwani katika ukurasa wake wa Facebook jana aliweka picha akiwa na Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro na kusema; “Leo nimekutana na Meya wa Jiji la Arusha, Mhe Calist Lazaro. Huyu ni rafiki yangu wa siku nyingi. Ni matumaini yangu tutashirikiana kuacha uongozi unaoacha alama! Arusha ni yetu sote!”

Kama ilivyo Arusha, wilayani Mbeya nako kuna siasa za mihemko na tayari Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla ameshakumbana na joto lake pale aliposusiwa kikao na madiwani pamoja na meya wa jiji kwa kutokuwataarifu kuwapo kwa mkutano kuhusu Soko Kuu la Mwanjelwa.

Wadau wazungumza

Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa akizungumzia wakuu wa wilaya hizo alisema ili wafanikiwe kututatua migogoro ya ardhi wanapaswa kukaa pamoja na wahusika ili kuijua historia ya migogoro na chanzo chake.

“Wasiende moja kwa moja kushughulikia migogoro ya ardhi bila kuwahusisha wananchi na wadau. Ni lazima washirikishe pande zote ili wajue pa kuanzia katika utatuzi,” alisema Ole Ngurumwa.

Mwanasheria wa Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Wafugaji (Pingos), Emmanuel Serengi aliwataka wakuu hao wa wilaya kusoma mazingira na kusikiliza maoni ya pande zote zinazohusika katika migogoro.

“Wasisahau kufanya kazi kwa uadilifu na watambue taasisi za kimila zilizopo katika eneo lenye mgogoro ili kurahisisha majukumu yao ya utatuzi,” alisema.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba aliwataka wakuu hao wa wilaya kufanya kazi kulingana na sheria zilizopo bila kuingilia wengine.

Alisema Sheria ya Ardhi, namba tano ya mwaka 1999, inaeleza utaratibu wa kushughulikia migogoro ya ardhi akisema inamtambua mkurugenzi wa manispaa husika kuwa ni mtumiaji na mpangaji wa ardhi.

“Likitokea tatizo lolote katika ardhi mkurugenzi ndiyo ana wajibu wa kulitatua kupitia maofisa wake wa ardhi walioko chini yake,” alisema Kibamba.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad