SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati na Madini inatarajia kuboresha uzalishaji wa umeme nchini na hivyo kuondoa kabisa mgawo wa umeme nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Nishati, Dk Juliana Pallangyo alipotembelea banda la Wizara ya Nishati na Madini katika Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa nishati ya umeme, serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwamo kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye sekta hiyo na ili kuchochea uanzishwaji wa viwanda vitakavyochangia ukuaji wa uchumi nchini.
Akielezea mikakati ya serikali katika uboreshaji wa huduma ya umeme nchini, Dk Pallangyo alisema kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Tatu, serikali itaendelea kusambaza umeme vijijini ikitoa kipaumbele kwa vijiji ambayo havikuwepo kwenye REA Awamu ya Pili.
Alisema uwepo umeme wa uhakika vijijini utachochea uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo, uboreshaji wa huduma za jamii na hivyo kupunguza wimbi la vijana kukimbilia mijini kutafuta ajira.
Aidha, alisema serikali imebuni vyanzo vingine kama vile upepo, gesi jotoardhi, jua na kuwataka wawekezaji kujitokeza katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo hivyo utakaoingizwa kwenye Gridi ya Taifa na kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme.