Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, alihoji kwa nini mabenki yametoa matangazo ya kuanza kutoza kodi hiyo, wakati hata kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo hazijatolewa.
Kidata alisema pamoja na kupitishwa kwa sheria hiyo bungeni, lakini muongozo unaotokana na kanuni bado haujatolewa, ndio maana TRA imeshindwa kuelewa kwanini taasisi hizo zimetoa taarifa zao kwa wananchi.
Kutokana na hali hiyo ya kutoa matangazo ya kutekeleza sheria hiyo, wakati kanuni za kutekeleza sheria yenyewe hazijatolewa, Kidata alisema kumeonekana dalili za nia ovu.
“Tangu lini mmeona benki au taasisi ya fedha inaanza kutoa matangazo ya utekelezaji wa sheria za serikali? Hii ni kwa sababu ya nia ovu.
“Kuna taarifa ambazo si za kweli zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa VAT itatozwa kwenye amana ya mwenye fedha kwenye benki. Hii si kweli,” alisema Kidata.
Usahihi wa kodi
“Juzi Bunge la Tanzania lilipitisha marekebisho ya sheria hiyo ya mwaka 2014 kuanzia Julai mosi mwaka huu kwenye huduma za kifedha kwa kurekebisha kifungu cha 13 cha jedwali la msamaha wa kodi, lakini taasisi hizo zimekuwa zikipotosha umma,” alisema.
Alisema kutokana na upotoshaji huo, TRA imeamua kueleza ukweli kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo, ili kuondoa utata na upotoshaji unaohusu utekelezaji wa sheria hiyo.
Kidata alisema sheria hiyo inalenga kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia 18, kwenye ada ambazo benki zinatoza wateja wake katika huduma mbalimbali zitolewazo na benki au taasisi za fedha.
“Ukweli ni kuwa kiasi cha VAT kitakachotozwa ni asilimia 18 ya kiasi cha gharama ya huduma iliyotolewa na benki au taasisi yoyote ya fedha na si kwa mteja,” alisema.
Akitolea mfano suala hilo, Kidata alisema kama ada ya huduma ya benki ambayo mteja ametozwa ni Sh 1,000, VAT itakayotozwa kwenye kiasi hicho ni Sh 152.50 tu na benki kubaki na Sh 847.50 na si kuwaongezea wananchi mzigo.
“Kiwango hiki cha Sh 152.50 ndicho kitakachorejeshwa serikalini na benki au taasisi ya fedha baada ya kupunguza VAT iliyolipwa kwenye manunuzi ambayo yamefanywa kwa benki au taasisi ya fedha husika. Kwa mujibu wa sheria hii, VAT haitatozwa kwenye riba inayotozwa na benki kwenye mikopo,” alisema.
Alisema kuna maelezo yametolewa na moja ya benki hapa nchini kuwa mtumiaji wa huduma za kifedha, atatakiwa kulipia kwa fedha taslimu kama muamala husika haukupitia kwenye akaunti na kuongeza kuwa taarifa hiyo siyo sahihi, kwa kuwa ukusanyaji wa VAT husika, utafanywa kwa njia ile ile ambayo gharama za huduma za kifedha zinakusanywa sasa.
Kidata alisema TRA itatoa maelekezo ya namna utoaji wa risiti za kielektroniki utakavyofanyika, ili kuwezesha mabenki au taasisi za kifedha kutimiza matakwa ya kisheria ya VAT ya mwaka 2014 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.
“Hivyo tunazitaka benki na taasisi za fedha zilizoamua kwa makusudi kutoa taarifa zisizo sahihi kwa umma, kuacha mara moja vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
“Kimsingi benki na taasisi za fedha zinazohusika zinaagizwa kurekebisha mara moja taarifa walizokwishazisambaza ili zibebe maudhui sahihi ya marekebisho ya sheria hii,” alisema.
Barua BoT
Alisema katika hatua za awali, tayari wamewapa maelekezo Benki Kuu (BoT) ambayo ni msimamizi wao mkuu, ihakikishe hicho kinachofanyika kinasitishwa na hatua mbalimbali za kisheria zitachukuliwa.
“Mwanzo benki na taasisi hizo za fedha zilikuwa zikichukua tozo yote wanayotoza, hivyo sasa tumewataka katika hiyo hiyo waliyokuwa wakichukua, ndiyo watoe kodi na si kumuongezea mwananchi mzigo kwa sababu kila kodi ina msingi wake na si kila kodi inapopanda, imlenge mwananchi. Sisi tumelenga hiyo hiyo wanayotoza,” alisema.
Alitoa mwito kwa mtu yeyote mwenye uhakika kuwa ameongezewa makato na benki au taasisi za fedha kwa madai ya utekelezaji wa sheria hiyo, atoe taarifa ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe.
Bora mwanga umepatikana. Maana wanasiasa uchwara walishaanza upotoshaji WA hili ili sisi wananchi tuweze kuwaamini kwa Hilo.. Ufafanuzi Ni mzuri na elekevu..na mmeweza kuweka mlango wazi WA malalamiko ikiwa Kuna aliyefanyiwa kinyume na huu maelekezo na ufafanuzi..Tuko vizuri tena pamoja Sana..Hapa kazi Tu
ReplyDelete