Upelelezi wa kesi ya kina Masamaki bado haujakamilika


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepiga kalenda kesi inayomkabili Kamishna wa Kodi na Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki  na wenzake  hadi Agosti 23, mwaka huu baada ya upande wa Jamhuri kudai upelelezi wake bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Alidai kuwa upande wa Jamhuri unaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Shahidi alisema dhamana ya washtakiwa inaendelea na kesi hiyo itatajwa tena Agosti 23, mwaka huu.

Mbali ya Masamaki, washtakiwa wengine ni, Haroun Mpande wa kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta ICT TRA Msimamizi Mkuu Kitengo cha Ushuru wa Forodha  ICD Azam, Eliachi Mrema,  Mchambuzi  Mwandamizi  wa Masuala ya Biashara  TRA,  Hamis Omary , Meneja wa Oparesheni  za Usalama na Ulinzi  ICD, Raymond Adolf Louis  na Meneja wa Azam ICD, Ashrafu Khan .

Washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Juni Mosi na Novemba 17, 2015 walikula njama kwa kuidanganya serikali.

Washtakiwa hao, wanadaiwa kudanganya kuwa  Makontena 329 yaliyopo katika Bandari Kavu ya Azam (AICD) yalitolewa baada ya kodi zote kufanyika wakati wakijua si kweli.

Katika shitaka la pili,  wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho hicho jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kutimiza majukumu yao na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 12.7 bilioni.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ndio yale yale uchunguzi hauja kamilika na masamaki anakijiji bado mnachunguza Tu?

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad