Katika magonjwa yanayosumbua wanawake wengi na watoto nchini hivi sasa ni ugonjwa unaoathiri njia ya mkojo U.T.I (Urinary Tract Infection).
Wakati wanawake wengi wanaougua ugonjwa huu wakihangaika kila siku kupata tiba yenye usahihi, wataalamu wa afya wanasema unapojiimarisha mwilini kwa muda mrefu huathiri figo.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi kutoka hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dk Cyriel Massawe anasema, tatizo hili hujitokeza pale mlango wa njia ya haja ndogo unaposhambuliwa na bakteria ambao husambaa na wasipotibiwa mapema, huenea hadi kwenye figo na athari zake ni mbaya.
“Bakteria hawa hupatikana ndani ya sehemu za siri za mwanamke, bakteria hao wakiwa ndani ya uke hawana madhara kabisa, lakini pindi uke unapopata mchubuko bakteria hawa huanza kuathiri kibofu cha mkojo na mtu kuanza kupata madhara,” anasema na kuongeza:
Wanawake wanapata UTI kwa urahisi sana kuliko wanaume kwa sababu mirija ya mkojoya mwanamke ni mifupi ambayo huruhusu bacteria kuingia kwa urahisi tofauti na ya mwanaume.
Vyanzo vya UTI
Dk Masawe anasema kuna vyanzo vingi vinavyosababisha ugonjwa huu, ikiwamo matumizi ya maji machafu wakati wa kujisafisha au kuoga huweza kuweka bakteria kwa urahisi na mwanamke kupata UTI.
Uchafu wa vyoo umetajwa kuwa sababu nyingine, kwani matumizi ya vyoo ambavyo ni vichafu huweza kusababisha mwanamke kupata UTI kwa sababu ndani ya choo kuna bakteria wengi ambao wanaweza kusababisha UTI.
Anasema kufanya ngono mara kwa mara ni tatizo kubwa ambalo ndilo linafanya wanawake wengi kupata UTI siku hizi, kwani wakati wa ngono msuguano huwa mkubwa ambao hufanya bakteria kutoka kupitia majimaji ya ukeni na kuingia katika njia ya mkojo.
“Mwanamke ambaye anafanya ngono mara kwa mara yuko kwenye hatari ya kupata UTI kuliko yule ambaye hafanyi ngono mara kwa mara. Pia matumizi ya nguo za ndani za mitumba bila kufua husababisha kwa urahisi mwanamke kupata UTI,” anasema.
Hata hivyo anasema tatizo kubwa limetajwa kuwa kemikali, “kemikali zinawaathiri wanawake wengi siku hizi, kutumia sana kemikali hasa kwenye vipodozi ambavyo kemikali hizi kwa kuwa ni sumu huenda hadi kwenye kibofu na kuchubua kibofu na hapo ndipo tatizo hilo huanza.”
Wataalamu wamesisitiza kwamba wengi wamekuwa na tabia ya kubana mkojo kwa muda mrefu, lakini matokeo ya tabia hii ni kupata UTI.
Dalili za UTI
Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na mtu kusikia haja ya kukojoa kila wakati na kusisimka wakati wa kujisaidia, kusikia maumivu, kutoa mkojo mchafu na hata kutoa haja ndogo iliyochanganyika na damu.
Mwili kuchoka mara kwa mara, homa za mara kwa mara, kichwa kuuma mara kwa mara, kubanwa na mkojo halafu ukienda kukojoa unakuta mkojo kidogo, maumivu wakati wa kukojoa na kiuno kuuma.
Unaweza kuikinga UTI kwa njia mbadala
Mkurugenzi wa Kituo cha huduma ya ushauri nasaha, lishe na afya COUNSENUTH, Mary Materu anasema, kwa kawaida kila ugonjwa una tiba mbadala, siyo lazima kwenda hospitali.
“Unaweza kuudhibiti au kuponya ugonjwa huu kwa kunywa maji mengi pamoja na juisi itokanayo na matunda halisi, iwapo utawahi kabla tatizo halijawa sugu. Kwa maana nyingine, unaweza kujikinga na ugonjwa huu kwa kuwa na mazoea ya kunywa maji ya kutosha kila siku. Ukinywa maji ya kutosha yatakufanya uende haja ndogo kila mara na kwa njia hiyo wale bakteria watakuwa wakitoka na hatimaye kuisha kabisa,” anasema Materu.
Aidha, anasema njia nyingine ya kuudhibiti ugonjwa huu ni kunywa maji mengi au kwenda haja ndogo mara baada ya kufanya tendo la ndoa, kitendo hiki husaidia kuwaondoa mapema bakteria wote ulioambukizwa wakati wa kujamiiana na mwenzio.
“Katika hali ya kawaida, ugonjwa wa UTI hutoweka ndani ya siku tatu mara baada ya kuanza kutumia tiba asili ya kunywa maji mengi na juisi ya matunda halisi, iwapo ugonjwa utaendelea kuwepo baada ya siku hizo, hiyo itakuwa na maana ugonjwa wako umeshakomaa na hivyo hauwezi kutibika kwa tiba hii ya nyumbani,” anasema na kuongeza:
“Katika hali kama hii, utakuwa huna njia nyingine isipokuwa kwenda hospitalini na kuonana na daktari ambaye atakufanyia uchunguzi na kukupatia dozi sahihi ambayo utatakiwa kuizingatia bila kukosa. Uamuzi huu ni muhimu hasa kama unasikia maumivu makali ambayo yanaweza kuwa yanasababishwa na kuathirika kwa figo,” anasema Materu.
Dk Massawe anasema kwa kawaida tiba ya kidaktari kwa ugonjwa huu huhusisha matumizi ya dawa kali za ‘antibiotics’, ambazo watu wengi wanazikimbia kutokana na athari zake za baadaye (side effects).
Lakini ni muhimu kufuata ushauri wa daktari na kumaliza dozi ili kuepuka uwezekano wa kurejea kwa ugonjwa, tena kwa kasi kubwa.
Unaweza kujikinga na UTI
Mkurugenzi kutoka Kituo cha Afya Tiba cha Neema Herbalist & Nutritional Foods Clinic Dk Africanus Boniface anasema, ili kujiepusha na ugonjwa huu, suala la usafi na kuwa na tabia ya kunywa maji ya kutosha ni jambo muhimu sana.
“Hakikisha unajisafisha vizuri mara baada ya kwenda haja na kubadilisha mara kwa mara nguo yako ya ndani, hasa kwa akina mama,” anasema na kuongeza: “Vile vile usikae na haja ndogo kwa muda mrefu, nenda kajisaidie mara nyingi kadri unavyosikia kufanya hivyo. Kitu cha mwisho cha kuzingatia kwa mgonjwa wa UTI ni kupunguza unywaji wa pombe na vinywaji vingine vyenye sukari, kwa sababu sukari ni chakula cha bakteria hivyo kwa kuendelea kunywa kinywaji chenye sukari kutaifanya hali kuendelea kuwa mbaya, “ anasema Dk Boniface.
Anasema ugonjwa huu ni rahisi kuuepuka kwa mtu anayependa kunywa maji ya kutosha na kunywa juisi halisi kila siku.
Vyakula vinavyokukinga na UTI
Dk Boniface anasema, katika kuudhibiti ugonjwa huu, pendelea kula vyakula au vinywaji vyenye kiwango kikubwa cha vitamini C, ambayo utaipata kwenye matunda ya aina mbalimbali yakiwemo machungwa, mboga za majani n.k.
“Jiepushe na ulaji wa vyakula vya ‘kupaki’ kama vile ‘chizi’, chokoleti na bidhaa nyingine zilizotengenezwa kutokana na maziwa. Pia jiepushe na ulaji wa vyakula vyenye viungo vingi kama pilau, epuka vinywaji vyenye ‘caffeine’, kilevi na sigara na mwisho achana na vinywaji kama soda na vinavyofanana na soda,” anasema.