Wakili maarufu nchini Alberto Msando amechambua maagizo ya utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambayo amekuwa akiyatoa, likiwemo suala la uvutaji hadharani wa sigara na shisha.
Tangu alipoapishwa Machi mwaka huu, Makonda amekuwa akitoa maagizo mbalimbali na mikakati yake ya kutaka kulipanga upya jiji ili kuwe na maeneo maalum ya gereji, majumba ya maduka makubwa, maeneo ya kuuza magari tofauti na huduma nyinginezo. Mengine ni kuondoa ombaomba jijini, kutaka wasiovaa kofia ngumu kwenye bodaboda washtakiwe kwa kutaka kujiua, kuhakikisha mitaa inakuwa safi, kuondoa mashoga, kufungwa maeneo yanayofanya biashara ya shisha, kuondoa majengo yasiyo na maegesho, kutatua changamoto za elimu na barabara.
Lakini Msando anachambua mikakati hiyo, akionekana kushauri kuwa elimu itumike zaidi kwa kuwa maamuzi mengine yanahitaji nchi kutunga sheria, kitu ambacho hakitawezekana ndani ya siku saba.
Akichambua maagizo hayo huku akitolea mfano wa ombaomba, Msando anahoji katika uchambuzi wake aliouweka kwenye ukurasa wa facebook, kama bado wapo au wamerudi katika baadhi ya maeneo. Anasema huenda wengi wao hawakusikia matangazo kwenye televisheni au magazeti.
Alisema sababu za ombaomba hao kutoka huko walikokuwa kuja Dar es Salaam hazijaisha na ikiwa wataondoka Dar, si kwa sababu wameyachoka maisha ya kuombaomba bali kwa sababu hawatakiwi na mamlaka.
Alihoji itakuwaje ikiwa wataondoka Dar es Salaam na kwenda Morogoro au Kibaha mjini na kuendelea kuomba?
“Nadhani tatizo bado litabaki,” anasema akipendekeza mikakati iandaliwe kote wanakotoka na watakakopokewa.
Akizungumzia usafi wa mitaa, mwanasheria huyo anasema bado ni changamoto kwa kuwa kuna maeneo bado machafu.
“Hatuwezi kufanikiwa kama tabia ya uchafu haitakoma katika ngazi za familia na mitaa. Usafi na uchafu ni tabia. Ni mazoea. Watoto wafundishwe shuleni na nyumbani kuwa wasafi. Tujenge Tabia,” anashauri.
Kuhusu ushoga, Msando anasema sheria iko wazi kwamba hilo ni kosa la jinai na adhabu yake ni kifungo, lakini shida ni jinsi ya kuwakamata na kuwachukulia hatua. “Hatuwezi kutumia vigezo vya mavazi na mwendo. Kosa siyo kusema mimi shoga. Tunahitaji kuangalia hili kwa mapana. Lazima tuzipige vita,” anasema.
Msando anasema ukamataji wa watu wasiovaa kofia ngumu una changamoto zake kutokana na askari wa barabarani nao kufanya makosa hayo.
“Juzi nilimwona trafiki amemkamata dereva wa bodaboda, halafu akapanda hiyo pikipiki bila kuvaa helmet. Sasa nikajiuliza, huyu trafiki naye akamatwe na trafiki mwingine kwa kosa la kutaka kujiua? Hili kosa lipo kisheria?”anahoji.
Mwanasheria huyo anasema usalama wa raia ni jukumu la awali la raia mwenyewe na anayekufa au kupata ulemavu ni raia mwenyewe.
“Ni vyema kumwelimisha huyu raia mwenyewe, aogope na aache kupanda bodaboda bila kuvaa kofia. Akielewa wala hatuhitaji watu magerezani,” anasema.
Pia, Msando aligusia suala la uvutaji wa shisha na kusema kuwa hiyo ni tabia ambayo vijana wengi wanaiga kwa kufuata mkumbo, wanaona sifa na usasa zaidi, hasa wanafunzi wa vyuo.
“Ndani ya siku saba tutakuwa tumepitisha sheria kupiga marufuku? Unadhani jambo kama hili linakuwa” anahoji Msando.
Kweli kwa mambo yanayotakiwa kukomeshwa au kuzuiwa kulingana na sheria.. hizo sheria zitungwe kwanza. Tusikurupuke. Mambo mengine yanatendwa kwa ajili ya umaskini na kukosa elimu. Ondoa umaskini na elimisha kwanza. Kupiga viboko na kamata kamata ni hatua zisizodumu. Makonda hili mbona jambo liko wazi huo ni?
ReplyDelete