CHADEMA katika dhana ya kumtikisa Rais wa Tanzania

Msingi wa kichwa cha mada yangu ipo kwenye kitabu cha Uongozi Wetu Na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa mwaka 1994 na Mwl. Nyerere wakati taifa letu lilikuwa linakabiliwa na changamoto kadhaa za kihistoria ambazo ndizo zilimfanya kuingilia kati na kuandika kijitabu hiki ambacho kilikuwa kama nasaha, onyo, na usia kwa Watanzania.

Mwl. Nyerere alisema, ‘’ huwezi kumtikisa Rais wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe. Ni vizuri jambo hili likatamkwa wazi wazi na likaeleweka sawa sawa’’.

Maneno ya Mwl.Nyerere yanatupeleka kwenye Sura ya Pili ya Katiba ya Tanzania 1977 Ibara ya 33(2) inayosema,‘’Rais atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu’’.

Ukubwa na umuhimu wa madaraka ya Rais wa Tanzania umeelezwa kwa kirefu katika sura ya pili kuanzia Ibara ya 33 mpaka 46.

Akiandikia gazeti la “The London Observer” mwaka 1963, mwaka mmoja tu tangu kuanzishwa kwa nafasi ya ‘Rais Mtendaji’ nchini, Mwl. Nyerere, aliwahi kukiri kuhusu madaraka makubwa ya Rais Kikatiba akisema: “Katiba yetu inatofautiana na ile ya Amerika kwa sababu inamwezesha Rais kutenda kazi bila kuulizwa ulizwa [wala kuwajibishwa] mara kwa mara...Matakwa yetu si kudhibiti mwendo wa mabadiliko ya kijamii.

“Tunataka kiongeza mwendo (Rais) chenye nguvu kuweza kuvunja umasikini na vizuizi vilivyo ndani ya jamii…kusema kweli, Katiba (hii) inanifanya dikteta kwa kigezo chochote kile cha kidemokrasia,” alisema Mwalimu Nyerere.

Pamoja na kuachana na Katiba ya 1962 na kuandika Katiba ya 1977 ambayo mpaka sasa ina mabadiliko 14 lakini mabadiliko hayo hayajaondoa ukweli kuwa Katiba bado ina msingi unaomfanya Rais wa Tanzania kuwa kiongeza mwendo chenye nguvu kuweza kuvunja umasikini na vizuizi vilivyo ndani ya jamii na pia nguzo kuu ya nchi . Kama ilivyo nguzo kuu ya nyumba, kumtikisa Rais wa Tanzania ni kuitikisa Tanzania.

Mikutano na maandamano ‘’yasiyo na kibali’’ yaliyopangwa na CHADEMA kufanyika nchi nzima ni kama kumtikisa Rais wa Tanzania kwa sababu yatafanyika kinyume cha kauli yake.

Rais Magufuli hawezi kubadilisha kauli yake. Historia ya utendaji wake inaonyesha si mmoja wa viongozi wanaobadilisha badilisha misimammo yao. Sina uhakika zaidi kuhusu CHADEMA kwa sababu historia inaonyesha hawaeleweki kwenye misimamo. Kumbuka dhana ya kubadili gear angani

Swali la kujiuliza, kwa kiwango gani Rais atatikisika siku ya Septemba mosi na mtikisiko huo utaitikisa Tanzania kwa kiwango gani?

Je, mtikisiko huo kama utatokea utajenga precedence gani katika mstakabali wa siasa za Tanzania?

Nini itakuwa hatima ya CHADEMA kisiasa kama wataufyata au kubadilisha gear angani?

Ninaamini wataalam wa Impact Analysis wanaweza kunielewa vizuri.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mnauthibitisho gani kama hawa ni wanachadema na si watu wanaojifanya chadema kama wakati wa Uchaguzi.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad