Msanii Godfrey Tumaini au Dudubaya ameonesha mfano jinsi ya kuwa baba bora, kwa kuzungumza na mtoto wake kuhusu maambukizi ya magonjwa ya zinaa, na jinsi ya kujikinga na magonjwa hayo kwa kutumia condom.
Akizungumza na Planet Bongo ya East Africa Radio, Dudubaya amesema huwa anazungumza na kijana wake kwa kuwa hataki apate magonjwa ya zinaa na kufa mapema kabla yake.
"Mwezi wa 12 mwaka jana ndiyo nilikuwa naye alikuwa amefunga shule kwa hiyo kujiandaa kwenda form one, nilichomwambia siku moja mpaka washkaji walicheka maskani, nikamwambia dogo sikiliza, najua sasa hivi we unajisikia, sasa kama unajisikia unajua kuna kitu kinaitwa condom!?
akaniambia yah, unajua kuitumia!? akasema hapana, nikamwambia unajua kuna magonjwa kama gono, kuna kaswende na UKIMWI, na sipendi utangulie wewe kufa mimi nikabaki, ni bora mimi nife wewe ndo uje kuwa mrithi wangu", alisema Dudubaya.
Dudubaya aliendelea kusema kuwa wazazi wengi sasa hivi hawazungumzi na watoto wao na hatimaye watoto wanaingia kwenye mambo yasiyofaa, na mwisho wazazi huwalaum na kuwachukulia hatua watoto, kwa makosa ambayo wameyasababisha wenyewe.
"Mtoto anapofikia kujisikia haina sababu ya kumfungia geti, na ndiyo maana unakuta kuna watoto wanapata maambukizi ya magonjwa kama UKIMWI, kumbe we mzazi hukuongea na mwanao,
mzazi unatakiwa uzungumze na mwanao umwambie hivi na hivi, kwa mfano kama mjini hapa watoto kibao wanaharibika na madawa ya kulevya, kwa sababu mzazi huzungumzi na mtoto", Alisema Dudubaya.