Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Kingunge Ngombale-Mwiru aliwataka Marais wastaafu na Mawaziri Wakuu wastaafu nchini kuingilia mvutano wa kisiasa unaoendelea sasa kuhusu Ukuta kutafuta muafaka kwa Rais Magufuli.
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu alisema viongozi wakuu wastaafu ambao ni marais na mawaziri wakuu wamekuwa wakimshauri Rais katika masuala mbalimbali.
“Kweli tuko kimya lakini ukimya huo usitafsiriwe kuwa hatumshauri Rais sisi kama viongozi wastaafu, lakini haifanyiki kwenye vyombo vya habari,” alisema Jaji Warioba.
Jaji Warioba alisema badala ya kumjibu Kingunge ni vyema kumuachia Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi awakutanishe viongozi wa vyama vya siasa kujadili hali hiyo kwa lengo la kupata muafaka.
Hata hivyo, alisema ni wajibu wa Watanzania wote kuhakikisha wanalinda hali ya amani nchini badala ya kuliona jambo hilo linamhusu Rais John Magufuli pekee au mtu mwingine yeyote. “Tumsaidie msajili katika hili, hili sio tatizo la mtu mmoja bali ni la nchi nzima tusimuachie Rais,” alisema Jaji Warioba.
Aidha, alisema jambo ambalo linafanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa la kuandaa majadiliano ni jambo jema zaidi na kwamba yakifanyika mambo mengine yanaweza kuleta madhara kwa wananchi.
Jaji Mutungi hivi karibuni alipozungumza na vyombo vya habari aliwatoa hofu wananchi kuwa hakutakuwa na uvunjifu wa amani kutokana na sintofahamu inayoendelea nchini baina ya vyama vya siasa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu Cleopa Msuya alisema serikali imetoa mwongozo wake watu wauzingatie na siyo kufanyika mazungumzo.
Alisema viongozi wa vyama vya upinzani waliotangaza operesheni hiyo kama wana hoja za msingi waseme ili zipatiwe ufumbuzi, lakini siyo kuvunja miongozo iliyowekwa makusudi.
“Tukae tuzungumze na Rais tunazungumza nini? Kama una watoto wako umeweka miongozo wengine hawataki kufuata mnazungumza? Kama wana tatizo waseme kuna moja, mbili, tatu, sasa waache wapambane na dola,” alisema Msuya na kuongeza kuwa Rais Magufuli anatosha, aachwe afanye kazi zake kwa uhuru bila kuingiliwa na watu wengine.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ambaye pia alikuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa alipozungumza na gazeti hili jana alisema mazungumzo ni jambo zuri kuliko maandamano. Lowassa alisema ushauri wa Kingunge wa viongozi wastaafu kufanya mazungumzo na Rais Magufuli kwa lengo la kumshauri juu ya hali ya kisiasa inavyokwenda ni wa busara.
“Ushauri wa Mzee Kingunge ni wa busara sana na mimi naona viongozi wa zamani tukae tufanye mazungumzo na Rais kuliko kufanya maandamano,” alisema Lowassa.
SOURCE: Habarileo
Tufanye kazi kwanza,siasa baadae.
ReplyDeleteKuna uchama pia dhidi ya hawa vigogo ingawa wanajaribu.wengi viongozi wapo ccm na wanamaslahi kichama pia.huu ni ukweli.
ReplyDeleteKuna uchama pia dhidi ya hawa vigogo ingawa wanajaribu.wengi viongozi wapo ccm na wanamaslahi kichama pia.huu ni ukweli kwani wao ni binadamu kama sisi si miungu hawa.
ReplyDelete