KAMPUNI ya Mbowe Imebakiza Siku Moja Kulipa Deni la Billioni 1.3/= Kwa NHC

KAMPUNI ya Mbowe Hotels Limited (MHL) imebakiwa na siku ya leo tu, kuwa tayari imelipa deni la Sh bilioni 1.3 ya kodi, ambalo inadaiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili  kujinasua katika hatari ya kuondolewa katika jengo la shirika hilo, lililopo katika makutano ya mitaa ya Mkwepu na Indira Gandhi (Makunganya) jijini Dar es Salaam.

Jengo hilo ni maarufu kutokana na kuendesha shughuli mbalimbali za starehe na burudani kutokana na kuwepo kwa Club maarufu ya Billicanas.

Hatua hiyo inatokana na notisi mbili zilizotolewa; moja na Shirika la Nyumba la Taifa Juni 24, mwaka huu, ikitishia kuvunja makubaliano a mkataba wa ukodishaji wa jengo hilo, na kufuatiwa na notisi ya Kampuni ya Udalali wa Mahakama ya Fosters, ambazo zote zinamalizika muda wake leo.

Hata hivyo, jitihada za gazeti hili za kupata maelezo ya kampuni hiyo ya udalali wa Mahakama jana ili kujua hatua zitakazochukuliwa baada ya kuisha kwa muda huo leo, zilishindikana jana. Chanzo cha uhakika kililiambia gazeti hili kuwa kampuni hiyo ya MHL inayomilikiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ilikuwa haijalipa deni hilo.

Mbowe alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari mwishoni mwa wiki, akilihusisha deni hilo na masuala ya kisiasa, kwa madai kuwa suala hilo linakuzwa na kupotoshwa ili kumnyamazisha katika harakati za kisiasa, bila kukiri uwepo wa shauri baina ya pande hizo mbili juu ya deni hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Mchechu, alithibitisha kuwepo kwa mpango wa kuiondoa kwa nguvu kampuni ya Mbowe katika jengo hilo, alipozungumza na gazeti hili, akizungumzia masuala mbalimbali ya shirika hilo katika ujenzi wa nyumba za makazi ili kuunga mkono mpango wa serikali wa kuhamishia makao makuu mkoani Dodoma.

“Ni kweli kwamba tumemkabidhi mpangaji wetu huyo (Mbowe) notisi ya kumuondoa. Kampuni ya Hoteli za Mbowe ni miongoni mwa wateja wetu watatu ambao ni wadaiwa sugu wa kodi ya pango kwa wateja binafsi nchini,” alisema Mchechu.

Mchechu alisema suala hilo ni la kibiashara na halina uhusiano wa aina yoyote na masuala ya kisiasa, kama ilivyodaiwa na Mbowe alipozungumza na vyombo vya habari hivi karibuni.

“NHC haina uhusiano na masuala ya kisiasa wala kujihusisha nayo, hatuna uhusiano wowote na masuala ya Umoja wa Kupambana na ‘Udikteta’ (UKUTA). Namuomba Mbowe atambue kuwa hili suala ni la kibiashara na si vingine,” alisema Mchechu.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa NHC na MHL, wamekuwa na mgogoro wa muda mrefu kutokana na kampuni hiyo kushindwa kutekeleza makubaliano ya kimkataba ya ukodishaji wa jengo hilo, ulioingiwa na pande hizo mbili mwaka 1997.

Kutokana na mzozo huo, Februari 16, mwaka jana, Shirika hilo la Nyumba liliandika barua kwa Kampuni ya MHL kuijulisha azma yake ya kuvunja mkataba huo kutokana na kukiukwa.

Chanzo cha habari cha kuaminika, kililiambia gazeti hili kwamba hatua hiyo ya NHC kuandika notisi ya kuvunja mkataba, ilitokana na Kampuni ya Mbowe kushindwa kujibu na kusaini hati mpya ya makubaliano ya namna ya ukodishaji wa jengo hilo uliowasilishwa kwa kampuni hiyo Januari 18, 2015.
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mna lenu
    Mbona hamtaji wizara za serikali
    Kila kukicha Mbowe
    Tumechoka
    Kama kudaiwa hata serikali ya Tanzania inadaiwa matirion kibao
    Fyuuuuuuuu

    ReplyDelete
    Replies
    1. SASA HAPO UMEANDIKA NINI??? HUELEWEKI

      Delete

Top Post Ad

Below Post Ad