MSANII mkongwe wa Muziki wa Kizazi Kipya aliye katika majaribu makubwa ya matumizi ya madawa ya kulevya, hivi sasa anadaiwa kuwa full kicheko kufuatia mabadiliko makubwa ya afya yake tangu alipoanza kupata matibabu katika kituo cha wahanga wa ‘sembe’, Sober House kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani.
Kwa mujibu wa bosi wa kituo hicho, Karim Bhanji, Ray C hivi sasa yupo vizuri tofauti na zamani na kwamba kwa jinsi anavyoendelea, hali yake inazidi kutengemaa.
Ray-new“Unajua tatizo kubwa kwa Ray C ilikuwa kwamba alikuwa anapatiwa matibabu bila uangalizi wa kutosha. Ingawa alikuwa akinywa dawa, lakini kilichokuwa kinatokea ni kuwa anakwenda Mwananyamala kunywa dawa halafu anarudi nyumbani, huko mtaani anakutana tena na watu walewale anaendelea kutumia.
“Lakini kwa kuja hapa, baada ya dawa anadhibitiwa, hatoki hivyo hapati nafasi ya kujaribu tena kutumia unga, nina imani hali yake itaimarika kadiri muda unavyoenda,” alisema Bhanji na kuongeza kuwa akiwa kituoni, Ray C ameshaanza kuandika baadhi ya mistari ya Bongo Fleva.
Ray C alipelekwa katika kituo hicho na wasamaria wema Juni 18, mwaka huu, baada ya video kusambaa mitandaoni, ikimuonesha akiokolewa na polisi baada ya kudaiwa kutaka kujidhuru kutokana na kuzidiwa na matumizi ya madawa ya kulevya.
Kituo hicho cha Sober House pia kiliwahi kumpokea Mbongo Fleva mwingine, Chid Benz ambaye hata hivyo hakukaa kwa muda mrefu.