"MIMI Aboud Jumbe Mwinyi, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunibariki kuzaliwa ndani ya Uislamu na namuomba aniruzuku kufa na kufufuliwa ndani ya Uislamu".
Hayo ni sehemu ya yaliyomo katika Wasia wa Rais Mstaafu wa wa Zanzibar Alhaj Aboud Jumbe ambaye hivi sasa ametimiza umri wa miaka 80.
Akiwa na akili timamu kabisa Mzee Jumbe ameandika wasia huo wiki hii ambao nakala zake zimesambazwa kwa watu mbalimbali likiwemo gazeti hili.
Wasia huo wenye kuashiria kutahadharisha juu ya yale yanayoweza kuja kufanywa kinyume na ridhaa yake, umekuja siku chache baada ya kifo cha Rais mwingine Mstaafu wa Zanzibar Sheikh Idris Abdul Wakil.
"Ni matumaini yangu kwamba kama Mwenye Enzi Mungu alivyonirehemu kuwa Muislamu, atanijaalia nikifa kukoshwa, kuvishwa sanda, kutiwa katika jeneza, kusaliwa na kuzikwa kwa mujibu wa sunna ya Mtume Muhammad (sa.w.)", umeagiza wasia huo uliosainiwa kwa niaba
yake na Msaidizi wake Bwana Abubakar.
Agizo hilo linahusisha pia jeneza lake kutofunikwa bendera ya Taifa au ya CCM, kuwepo na utabaka katika kubeba jeneza na ufukiaji wa kaburi.
Akiwashuhudisha Mufti wa Zanzibar, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Naibu Kadhi Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Sharrif Juneid, Masheikh wengine na wanawe, Alhaj Jumbe amesisitiza kuwa kufanyiwa si ombi bali ni haki yake kama binadamu, kama Muislamu na kama Mtanzania.
Amesema haki ya uhuru wa kuabudu imeelezwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 19 (1) na (2).
Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu mtu anapokufa ni haramu kwa ndugu au jamaa zake kuomboleza kwa nyimbo, kunyoa vipara, kuvaa vitambaa au nguo nyeusi wala kulia kupita kiasi.
Aidha, imesuniwa kuwafariji (taa'zia) wafiwa kwa muda wa siku mbili tu.
"Atta'azia marrataan" ameagiza Mtume (s.a.w) akiwa maana ya kuwafariji wafiwa ni mara (siku) mbili.
Katika wasia wake Alhaj Jumbe amesema maana ya kuumbwa mauti na uhai sababu na lengo lake ni kuwafanyia wanaadamu mtihani kupimwa miongoni mwao mwenye vitendo vizuri.
"Nikiwa hai, dhamana ya vitendo vyangu inaniangukia mimi mwenyewe, nikifa dhamana ikiwa vitendo vyema au vibaya nitakavyofanyiwa itawaangukia waandalizi, watendaji na wenye kushiriki katika vitendo hivyo", amesisitiza mzee huyo aliyekuwa pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akimshudisha Mwenyezi Mungu katika wasia huo amekataa maziko yake kufanywa kinyume na taratibu za Kiislamu.
"Sitaki bendi, sitaki mizinga, sitaki maombolezo wala lolote lingine lenye hata chembe ya kufuru", ameandika kwa mkazo mzee huyo.
Aidha, amewaapiza kwa kumshuhudia Mwenyezi Mungu wale watakaojaribu kufanya kinyume na anavyoagiza.
"Sitaki hivyo nikiwa hai, nitakapoondoka katika dunia Mwenye Enzi Mungu anatosheka kuwa shahidi wangu, duniani na akhera", mzee Jumbe amemaliza wasia wake alioutanguliza aya ya Qur'an isemayo "Enyi wenye kuamini, mcheni Mwenyezi Mungu vile ipasavyo waja kumcha, wala msife ila Ilhali ni miongoni mwa Waislamu. (3:101)
--
Chanzo: islamtanzania.org
webmaster@islamtanzania.org
Jamii Forums