Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anatarajia kupanda ulingoni Agosti 27 kuzichapa na bondia Francis Cheka katika pambano la kuhamasisha usafi jijini Dar es salaam.
Akizungumza jijini Dar, Cheka amesema kampuni yake ya Cheka promosheni imeandaa pambano hilo ili kuunga mkono jitihada za Makonda katika zoezi zima la usafi.
“Siwezi kujua mkuu wa mkoa maandalizi yake ambayo amejiandaa lakini siku zote namuogopa mtu ambaye anaamua mapambano na mtu anayejua ngumi, ila namheshimu mkuu wa mkoa, kupitia mkuu wa mkoa ambapo wao ndiyo wametangaza usafi na sisi tusupport usafi katika nchi yetu,”, alisema.
Cheka aliongeza kuwa kutakuwa na mabondia kutoka Kenya, Uganda na Malawi.
Aidha Cheka amesema zoezi la kuhamasisha mabondia kushiriki katika usafi litakuwa endelevu katika mikoa mingine ikiwa ni Arusha, Morogoro, Dodoma na Mwanza.
Kwa upande mwingine, Afisa michezo ofisi ya mkuu wa mkoa, Adolf Ally, aliwataka watu wengine kuiga mfano wa Cheka katika kampeni yao ya ‘Usijifanye mstaarabu kuwa mstaarabu.’