Takukuru yafafanua soo la Aveva

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), imefunguka rasmi sababu za kumshikilia na kumweka ndani Rais wa Simba, Evans Aveva.

Aveva alishikiliwa tangu juzi Jumatano na kulala ndani kwenye Kituo cha Polisi cha Urafiki jijini Dar kabla ya kutolewa kwa dhamana Alhamisi huku chanzo cha yote kikiwa ni baada ya Takukuru kubaini alifanya uchepushaji wa fedha za mauzo ya fowadi, Emmanuel Okwi walizolipwa Simba na Etoile du Sahel dola laki tatu ambazo zilitolewa kwenye akaunti ya klabu na kuhamishiwa kwenye akaunti yake kabla ya kuanza kusambazwa huku nyingine zikihamishiwa katika akaunti moja ya nchini Hong Kong.

Msemaji wa Takukuru, Tunu Mlei ameliambia Championi Jumamosi kuwa kutokana na mazingira hayo, walihisi uwepo wa rushwa hivyo kuanza kuchunguza.

Tunu amefunguka huku akisisitiza kuwa iwapo atabainika na makosa katika sheria ya uchepushwaji, anaweza kufunguliwa mashtaka mahakamani.

“Kwa sasa bado tunaendelea na uchunguzi na kwa mujibu wa sheria zetu haziniruhusu kusema nini kinaendelea kwenye uchunguzi,” alisema.

“Muda wa kuwachunguza itategemea. Kuna process (mchakato) zake. Kwa sasa tupo katika sheria No.11 kifungu cha 29 ya mwaka 2007 inayohusu uchepushwaji wa fedha, tukimaliza uchunguzi kazi yetu ni kupeleka faili kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka nchini, ndiye mwenye kuamua kesi iende mahakamani ama la.”

Akafunguka zaidi kuwa kwa sasa wanafanya kazi na Serikali ya Hong Kong.
“Kama unavyojua uchunguzi unahusishwa na nje ya nchi kwa kuwa kuna hela zimekwenda Hong Kong, hivyo tunashirikiana na serikali ya huko kujua zilikwenda kufanya kitu gani,” aliongeza.
Tunu amesema iwapo uchunguzi utabaini kuna mazingira ya rushwa, sheria itachukua mkondo wake lakini sheria ya uchepushaji wa hela pia ina adhabu yake.

“Kama nilivyosema tupo kwenye sheria ya uchepushaji, ambayo pia ina adhabu yake lakini siwezi kuisema maana vifungu vinaweza kuongezeka kulingana na uchunguzi utakavyofungua mambo mengine,” alisema Tunu.

Licha ya mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage kusisitiza Etoile du Sahel kuilipa Simba fedha hizo muda mrefu, viongozi chini ya Aveva wamekuwa wakiruka kimanga wakisema bado hela hiyo haijaingia kwenye akaunti zao.

Simba ilimuuza Okwi mwaka 2013 wakati wa utawala wa Mwenyekiti Ismail Aden Rage, hata hivyo hakukaa sana kabla ya kwenda SC Villa ya Uganda, kisha Yanga kabla ya kurejea Simba ambako alikaa msimu mmoja kabla ya kuuzwa kwa dola 110,000 kwenda SonderjyskE ya nchini Denmark, mwaka juzi.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ndiyo maana waukimbilia uongozi katika team za mpira shauri kuna deal kama hizo za kujilimbikizia pesa kwenye account zao binafsi nje ya nchi siyo yeye tu bali wapo wengi wenye tabia na ubinafsi kama huo wao wananeemeka wachezaji wapo vile vile kimaisha duh!

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad